Kumbukumbu

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34

Kumbukumbu 1


1 Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng'ambo ya Yordani barani, katika Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu.
2 Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea.
3 Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na Bwana ya kuwaamuru;
4 alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei;
5 ni ng'ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema,
6 Bwana, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;
7 geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.
8 Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.
9 Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu.
10 Bwana, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi.
11 Bwana, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi.
12 Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na mateto yenu?
13 Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya kabila zenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu.
14 Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilonena ni jema la kufanya.
15 Basi nikatwaa vichwa vya kabila zenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, maakida ya elfu elfu, na maakida ya mia mia, na maakida ya hamsini hamsini, na maakida ya kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya kabila zenu.
16 Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye.
17 Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.
18 Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya.
19 Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama Bwana, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea.
20 Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi Bwana, Mungu wetu.
21 Tazama, Bwana, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike.
22 Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.
23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila.
24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza.
25 Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa Bwana, Mungu wetu, ni nchi njema.
26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la Bwana, Mungu wenu;
27 mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu Bwana ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza.
28 Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki.
29 Ndipo nikawaambieni, Msifanye hofu, wala msiwache.
30 Bwana, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu;
31 na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua Bwana, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa.
32 Lakini katika jambo hili hamkumwamini Bwana, Mungu wenu,
33 aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonyesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.
34 Bwana akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema,
35 Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,
36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata Bwana kwa kila neno.
37 Na Bwana alinikasirikia mimi kwa ajili yenu, akasema, Wala wewe hutaingia humo;
38 Yoshua mwana wa Nuni asimamaye mbele yako ndiye atakayeingia; mtie moyo; kwa kuwa yeye atawarithisha Israeli.
39 Tena, wadogo wenu, mliosema watakuwa mateka, na wana wenu, wasiokuwa leo na maarifa ya mabaya wala mema, ndio watakaoingia, nao ndio nitakaowapa, nao wataimiliki.
40 Na ninyi basi geukeni, mshike safari yenu, mwende jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu.
41 Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya Bwana, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na Bwana. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani.
42 Bwana akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu.
43 Basi niliwaambia, msinisikize, bali mliasi amri ya Bwana, mkajikinai, na kukwea mlimani.
44 Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma.
45 Mkarudi mkalia mbele za Bwana; Bwana asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu.
46 Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.

Kumbukumbu 2


1 Ndipo tukageuka, tukashika safari yetu kwenda jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia Bwana; tukawa kuizunguka milima ya Seiri siku nyingi.
2 Bwana akanena, akaniambia,
3 Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini.
4 Nawe waagize watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa Esau waketio Seiri; nao watawaogopa; basi jiangalieni nafsi zenu sana;
5 msitete nao; kwa maana sitawapa katika nchi yao kamwe, hata kiasi cha kukanyaga wayo wa mguu; kwa kuwa nimempa Esau milima ya Seiri kuwa milki yake.
6 Nunueni vyakula kwao kwa fedha, mpate kula; na maji nayo nunueni kwao kwa fedha, mpate kunywa.
7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, amekubarikia katika kazi yote ya mkono wako; amejua ulivyotembea katika jangwa kubwa hili; miaka arobaini hii alikuwa nawe Bwana, Mungu wako; hukukosa kitu.
8 Basi tukapita kando yao ndugu zetu wana wa Esau, waketio Seiri kutoka njia ya Araba, kutoka Elathi na kutoka Esion-geberi. Tukageuka tukapita njia ya bara ya Moabu.
9 Bwana akaniambia, usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki.
10 (Walioketi humo hapo kale ni Waemi, nao ni watu wakubwa, wengi, warefu, mfano wa Waanaki;
11 na hawa nao wadhaniwa kuwa majitu kama Waanaki;lakini Wamoabi huwaita Waemi.
12 Na Wahori nao walikuwa wakikaa Seiri hapo kale, lakini wana wa Esau waliwafuata; wakawaangamiza mbele yao, wakakaa badala yao; kama alivyofanya Israeli nchi ya milki yake aliyopewa na Bwana.)
13 Sasa basi ondokeni, mkakivuke kijito cha Zeredi. Nasi tukakivuka kile kijito cha Zeredi.
14 Na siku tulizokuwa tukienda kutoka Kadesh-barnea hata tulipovuka kijito cha Zeredi, zilikuwa ni miaka thelathini na minane; maana, hata walipokwisha kuangamizwa watu wa vita kutoka kati ya marago, kizazi chao chote, kama walivyoapiwa na Bwana.
15 Tena mkono wa Bwana ulikuwa juu yao ili kuwaangamiza, kuwatoa kati ya marago, hata walipokoma.
16 Basi ikawa, walipokwisha angamizwa kwa kufa watu wote wa vita kati ya watu,
17 Bwana aliniambia, akasema,
18 Hivi leo ivuke Ari, mpaka wa Moabu;
19 na utakaposongea kuwaelekea wana wa Amoni, usiwasumbue wana wa Amoni, wala usishindane nao; kwa kuwa sitakupa katika nchi ya hao wana wa Amoni kuwa milki yako; kwa sababu nimewapa wana wa Lutu iwe milki yao.
20 (Nchi hiyo nayo yadhaniwa kuwa ni nchi ya Warefai, hapo kale Warefai walikaa humo; lakini Waamoni huwaita Wazamzumi;
21 nao ni watu wengi, wakubwa, warefu, kama Waanaki; lakini Bwana aliwaangamiza mbele yao; wakawafuata wakakaa badala yao;
22 kama vile alivyowafanyia wana wa Esau, waliokaa Seiri, alipowaangamiza Wahori mbele yao; wakawafuata, wakakaa badala yao hata hivi leo;
23 na Waavi waliokuwa wakikaa katika vijiji mpaka Gaza waliangamizwa na Wakaftori waliotoka Kaftori, na hawa wakakaa badala yao.)
24 Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano.
25 Hivi leo nitaanza mimi kutia utisho wako na kuhofiwa kwako juu ya watu walio chini ya mbingu kila mahali, watakaosikia uvumi wako, na kutetemeka, na kuingiwa na uchungu kwa sababu yako.
26 Nikatuma wajumbe kutoka bara ya Kedemothi kwenda kwa Sihoni mfalme wa Heshboni na maneno ya amani, kusema.
27 Nipishe katikati ya nchi yako; nitakwenda kwa njia ya barabara, sitageuka kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto.
28 Nawe uniuzie chakula kwa fedha nile; unipe na maji kwa fedha, ninywe; ila unipishe katikati kwa miguu yangu, hayo tu;
29 kama walivyonifanyia hao wana wa Esau waketio Seiri, na hao Wamoabi waketio Ari; hata nivuke Yordani niingie nchi tupewayo na Bwana, Mungu wetu.
30 Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni hakutuacha kupitia kwake; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, alimfanya mgumu roho yake, akamtia ukaidi moyoni mwake, apate mtia mkononi mwako kama alivyo hivi leo.
31 Kisha Bwana akaniambia, Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako; anza kuimiliki, upate kuirithi nchi yake.
32 Ndipo Sihoni alipotutokea juu yetu yeye na watu wake wote, kupigana huko Yahasa.
33 Bwana, Mungu wetu, akamtoa mbele yetu, tukampiga yeye na wanawe, na watu wake wote.
34 Tukatwaa miji yake yote wakati huo, tukaharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na wadogo; tusimsaze hata mmoja;
35 ila ng'ombe zao tuliwatwaa kuwa mawindo yetu, pamoja na nyara za miji tuliyoitwaa.
36 Kutoka Aroeri iliyo katika ukingo wa bonde la Arnoni, na huo mji ulio ndani ya bonde, mpaka kufika Gileadi, hapakuwa na mji uliokuwa mrefu kutushinda; Bwana, Mungu wetu, aliiweka wazi yote mbele yetu; ila nchi ya wana wa Amoni hukuisongelea;
37 upande wote wa mto wa Yaboki, na miji ya nchi ile ya milimani, na kila mahali alipotukataza Bwana, Mungu wetu.

Kumbukumbu 3


1 Ndipo tukageuka, tukakwea njia ya Bashani; na Ogu, mfalme wa Bashani, akatutokea juu yetu, yeye na watu wake wote, kuja kupigana huko Edrei.
2 Bwana akaniambia, Usimwogope; kwa kuwa nimemtia mkononi mwako, yeye na watu wake wote na nchi yake; nawe utamtenda mfano wa ulivyomtenda Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni.
3 Basi Bwana, Mungu wetu, akamtia mikononi mwetu na Ogu mfalme wa Bashani, na watu wake wote; tukampiga, asisaziwe cho chote.
4 Tukatwaa miji yake yote wakati huo; hapakuwa na mji tusiotwaa kwao miji sitini, nchi yote ya Argobu, ndio ufalme wa Ogu ulio katika Bashani.
5 Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma marefu, na malango, na makomeo, pamoja na miji isiyokuwa na maboma, mingi sana.
6 Tukaiharibu kabisa, kama tulivyomfanya huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, kwa kuharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na watoto.
7 Lakini wanyama wote wa mji, na nyara za miji, tulitwaa kuwa mawindo yetu.
8 Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng'ambo ya Yordani, tokea bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni;
9 (na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri);
10 miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani.
11 (Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho je! Hakiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni mikono kenda,na upana wake mikono minne,kwa mfano wa mkono wa mtu)
12 Na nchi hiyo tuliitwaa ikawa milki yetu, wakati huo; tokea Aroeri iliyo kwenye bonde la Arnoni, na nusu ya nchi ya milima ya Gileadi, na miji iliyokuwamo, niliwapa Wareubeni na Wagadi;
13 na nchi ya Gileadi iliyobaki, na Bashani yote, maana huo ufalme wa Ogu niliwapa nusu ya kabila ya Manase; nchi yote ya Argobu, nayo ndiyo Bashani yote. (Na nchi hii yaitwa nchi ya Warefai.
14 Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.)
15 Na Makiri nilimpa Gileadi.
16 Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni;
17 na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya matelemko ya Pisga, upande wa mashariki.
18 Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii mwimiliki, basi vukeni ng'ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa.
19 Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa;
20 hata Bwana awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na Bwana, Mungu wenu, ng'ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa.
21 Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda Bwana, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda Bwana kila ufalme huko uvukiako.
22 Msiwache, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.
23 Nikamnyenyekea Bwana wakati huo, nikamwambia,
24 Ee Bwana Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu?
25 Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng'ambo ya Jordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni.
26 Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili.
27 Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani.
28 Lakini mwagize Yoshua umtie moyo mkuu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye.
29 Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.

Kumbukumbu 4


1 Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.
2 Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo.
3 Macho yenu yameona aliyoyatenda Bwana kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, Bwana, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako.
4 Bali ninyi mlioambatana na Bwana, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo.
5 Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.
6 Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.
7 Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?
8 Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
9 Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;
10 siku ile uliyosimama mbele za Bwana wako huko Horebu, Bwana aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao.
11 Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu.
12 Bwana akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.
13 Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.
14 Bwana akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.
15 Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile Bwana aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;
16 msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,
17 mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,
18 au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;
19 tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo Bwana, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.
20 Bali Bwana amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.
21 Tena Bwana alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo Bwana, Mungu wenu, iwe urithi.
22 Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema.
23 Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la Bwana, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na Bwana, Mungu wenu,
24 kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.
25 Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, na kumtia hasira;
26 nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa.
27 Na Bwana atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na Bwana.
28 Na huko mtatumikia miungu, kazi za mikono ya watu, miti na mawe, ambao hawaoni, wala hawasikii, hawali, wala hawanusi.
29 Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.
30 Na wakati uwapo katika mashaka, ukiisha kupatwa na mambo haya yote, siku za mwisho, utamrudia Bwana, Mungu wako, na kuisikiza sauti yake;
31 kwa kuwa Bwana, Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia.
32 Maana uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili?
33 Je! Watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife?
34 Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu?
35 Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye.
36 Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto.
37 Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi,
38 ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nchi yao iwe urithi, kama ilivyo leo.
39 Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine.
40 Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.
41 Ndipo Musa akabagua miji mitatu ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;
42 ili kwamba amwuaye mtu apate kukimbilia huko, amwuaye jirani yake pasipo kujua, wala hakumchukia tangu hapo; ili apate kuishi akimbiliapo mmojawapo miji hiyo;
43 nayo ni hii, Beseri ya barani iliyo katika nchi tambarare, kwa Wareubeni; na Ramothi iliyo Gileadi, kwa Wagadi; na Golani iliyo Bashani, kwa Wamanase.
44 Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii;
45 haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri;
46 ng'ambo ya Yordani, katika bonde lililoelekea Beth-peori, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni ndiye aliyepigwa na Musa na wana wa Israeli, walipotoka Misri;
47 wakaishika nchi yake, ikawa milki yao, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, ndio wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;
48 toka Aroeri, iliyo juu ya ukingoni pa bonde la Arnoni, hata mpaka mlima wa Sioni (nao ndio Hermoni),
49 na Araba yote iliyo ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, hata mpaka bahari ya Araba, chini ya matelemko ya Pisga.

Kumbukumbu 5


1 Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda.
2 Bwana, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu.
3 Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai.
4 Bwana alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto;
5 (nami wakati ule nalisimama kati ya Bwana na ninyi, ili kuwaonyesha neno la Bwana; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema,
6 Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
7 Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi.
9 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
10 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
11 Usilitaje bure Jina la Bwana, Mungu wako; maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure.
12 Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru.
13 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
14 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe.
15 Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.
16 Waheshimu baba yako na mama yako; kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
17 Usiue.
18 Wala usizini.
19 Wala usiibe.
20 Wala usimshuhudie jirani yako uongo.
21 Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.
22 Haya ndiyo maneno ambayo Bwana aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa.
23 Ikawa, mlipoisikia sauti ile toka kati ya giza, na wakati uo huo mlima ule ulikuwa ukiwaka moto, basi, mlinikaribia, naam, wakuu wote wa kabila zenu, na wazee wenu,
24 mkasema, Tazama, Bwana, Mungu wetu, ametuonyesha utukufu wake, na ukuu wake, nasi tunasikia sauti yake toka kati ya moto; mmeona leo ya kuwa Mungu husema na mwanadamu, naye akaishi.
25 Sasa basi, mbona tufe? Maana moto huu mkubwa utatuteketeza; tukiisikia tena sauti ya Bwana, Mungu wetu, tutakufa.
26 Maana katika wote wenye mwili ni nani aliyeisikia sauti ya Mungu aliye hai, akisema toka kati ya moto, kama vile sisi, asife?
27 Enenda karibu wewe, ukasikie yote atakayoyasema Bwana, Mungu wetu; ukatuambie yote atakayokuambia Bwana, Mungu wetu; nasi tutayasikia na kuyatenda.
28 Naye Bwana akasikia sauti ya maneno yenu mliyoniambia; Bwana akaniambia, Nimesikia sauti ya maneno ya watu hawa waliyokuambia; wamesema vema yote waliyosema.
29 Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao sikuzote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote sikuzote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele!
30 Enda uwaambie, Rudini hemani mwenu.
31 Lakini wewe, simama hapa karibu nami, nami nitanena nawe sheria zote, na amri na hukumu, utakazowafunza, wapate kuzifanya katika nchi niwapayo kuimiliki.
32 Tunzeni basi, mtende kama mlivyoamriwa na Bwana, Mungu wenu; msikengeuke kwa mkono wa kuume wala wa kushoto.
33 Endeni njia yote aliyowaagiza Bwana, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki.

Kumbukumbu 6


1 Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru Bwana, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki;
2 upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe.
3 Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.
4 Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
6 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;
7 nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.
8 Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.
9 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.
10 Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,
11 na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba;
12 ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.
13 Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.
14 Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;
15 kwani Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya Bwana, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.
16 Msimjaribu Bwana, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa.
17 Zishikeni kwa bidii sheria za Bwana, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza.
18 Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa Bwana; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia baba zako,
19 ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema Bwana.
20 Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N'nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza Bwana, Mungu wetu?
21 Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; Bwana, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu;
22 Bwana akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu;
23 akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu.
24 Bwana akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche Bwana, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo.
25 Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya Bwana, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

Kumbukumbu 7


1 Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe;
2 wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao;
3 binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake.
4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi.
5 Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.
6 Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.
7 Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote;
8 bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.
9 Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;
10 naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake.
11 Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende.
12 Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;
13 naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.
14 Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo.
15 Na Bwana atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.
16 Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa Bwana, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.
17 Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?
18 Usiwaogope; kumbuka sana Bwana, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;
19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje Bwana, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya Bwana, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.
20 Tena Bwana, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.
21 Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.
22 Naye Bwana, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu.
23 Ila Bwana, Mungu wako, atawatoa mbele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa.
24 Na wafalme wao atakutilia mkononi mwako, nawe utalipoteza jina lao litoke chini ya mbingu; hapana mtu atakayeweza kusimama mbele yako, hata utakapokwisha kuwaangamiza.
25 Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako;
26 na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.

Kumbukumbu 8


1 Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.
2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.
3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.
4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini.
5 Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo.
6 Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.
7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;
8 nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;
9 nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba.
10 Nawe utakula ushibe, utamshukuru Bwana, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa.
11 Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo.
12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;
13 na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;
14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;
15 aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu,
16 aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.
17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.
18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.
19 Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka.
20 Kama vile mataifa yale ambayo Bwana anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya Bwana, Mungu wenu.

Kumbukumbu 9


1 Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni,
2 watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki?
3 Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana.
4 Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako.
5 Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
6 Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.
7 Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana
8 Tena mlimkasirisha Bwana katika Horebu, Bwana akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.
9 Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.
10 Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.
11 Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Bwana alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano.
12 Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.
13 Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;
14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.
15 Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.
16 Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru Bwana.
17 Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu.
18 Nikaanguka nchi mbele za Bwana siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kwa kumkasirisha.
19 Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia Bwana kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiza wakati huo nao.
20 Bwana akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.
21 Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani.
22 Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia Bwana hasira.
23 Na wakati alipowatuma Bwana kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya Bwana, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake.
24 Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi.
25 Ndipo nikaanguka nchi mbele za Bwana siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa Bwana alisema atawaangamiza.
26 Nikamwomba Bwana, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.
27 Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao;
28 isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani.
29 Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Kumbukumbu 10


1 Wakati ule Bwana akaniambia, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, kisha uje kwangu huku mlimani, ukajifanyie na sanduku la mti.
2 Nami nitaandika juu ya hizo mbao maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, ulizozivunja, nawe uzitie ndani ya hilo sanduku.
3 Basi nikafanya sanduku la mti wa mshita, nikachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nikakwea mle mlimani, na zile mbao mbili mkononi mwangu.
4 Naye akaandika juu ya mbao mfano wa maandiko ya kwanza, zile amri kumi, alizowaambia Bwana huko mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano; Bwana akanipa.
5 Basi nikageuka nikashuka kutoka mlimani, nikazitia mbao ndani ya sanduku nililofanya; nazo zimo humo kama alivyoniamuru Bwana.
6 (Wana wa Israeli wakasafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani kwenda Mosera; Haruni akafa huko, akazikwa huko; na Eleazari mwanawe alitumika utumishi wa ukuhani badala yake.
7 Wakasafiri kutoka huko kwenda Gudgoda; wakatoka Gudgoda wakaenda Yotbatha, nayo ni nchi ya vijito vya maji.
8 Na wakati huo Bwana aliitenga kabila ya Lawi ili walichukue lile sanduku la agano la Bwana, wasimame mbele ya Bwana kwa kumtumikia, na kuwabarikia watu kwa jina lake, hata hivi leo.
9 Ndipo asiwe na fungu Lawi, wala urithi pamoja na nduguze; Bwana ndiye urithi wake, kwa mfano wa vile alivyomwambia Bwana, Mungu wako.)
10 Nikakaa mle mlimani kama hapo kwanza, siku arobaini usiku na mchana; Bwana akanisikiza wakati huo nao; asitake Bwana kukuangamiza.
11 Bwana akaniambia, Ondoka, ushike safari yako mbele ya watu; nao wataingia waimiliki nchi, niliyowaapia baba zao ya kuwa nitawapa.
12 Na sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;
13 kuzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?
14 Tazama, mbingu ni mali za Bwana, Mungu wako, na mbingu za mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo.
15 Tena, Bwana aliwafurahia baba zako, na kuwapenda, akawachagua wazao wao baada yao, naam, na ninyi zaidi ya mataifa yote kama hivi leo.
16 Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu.
17 Kwa maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.
18 Huwafanyia yatima na mjane hukumu ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi.
19 Basi, mpendeni mgeni, kwa sababu ninyi wenyewe mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
20 Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake.
21 Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako.
22 Baba zako walishukia Misri na watu sabini; na sasa Bwana, Mungu wako, amekufanya kama nyota za mbinguni kwa wingi.

Kumbukumbu 11


1 Kwa ajili hii mpende Bwana, Mungu wako, na kushika sikuzote mausia yake, na amri zake, na hukumu zake, na maagizo yake.
2 Nanyi leo jueni; kwa kuwa sisemi sasa na vijana vyenu, ambao hawakujua, wala hawakuona adhabu ya Bwana, Mungu wenu, ukuu wake, na mkono wake wa nguvu, na mkono wake ulionyoka,
3 na ishara zake, na kazi zake alizomfanya Farao mfalme wa Misri, na nchi yake yote, katikati ya Misri;
4 na alivyolifanya jeshi la Misri, farasi zao, na magari yao; na alivyowafunikiza maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwaandamia, na alivyowaangamiza Bwana hata hivi leo;
5 na mambo aliyowafanyia ninyi barani, hata mkaja mahali hapa;
6 na alivyowafanya Dathani, na Abiramu, wana wa Eliabu mwana wa Reubeni; nchi ilivyofunua kinywa chake, ikawameza, na walio nyumbani mwao, na mahema yao, na kila kitu kilichokuwa hai kikiwafuata, katikati ya Israeli yote;
7 lakini macho yenu yameiona kazi kubwa ya Bwana aliyoifanya, yote.
8 Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote niwaagizayo leo, mpate kuwa na nguvu, na kuingia mkaimiliki nchi mwivukiayo kuimiliki;
9 nanyi mpate kuzifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, ya kuwa atawapa wao na kizazi chao, nchi imiminikayo maziwa na asali
10 Kwa kuwa nchi mwingiayo kuimiliki, si mfano wa nchi ya Misri mlikotoka, uliyokuwa ukipanda mbegu zako humo na kuinywesheleza kwa mguu wako, kama shamba la mboga;
11 lakini nchi mwivukiayo kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua ya mbinguni;
12 nayo ni nchi itunzwayo na Bwana, Mungu wako; macho ya Bwana Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka.
13 Tena itakuwa, mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote,
14 ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako.
15 Nami nitakupa nyasi katika mavue yako kulisha wanyama wako wa mifugo, nawe utakula na kushiba.
16 Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu;
17 hasira za Bwana zikawaka juu yenu, naye akafunga mbingu kusiwe na mvua, wala nchi isitoe matunda yake; mkaangamia kwa upesi mtoke katika nchi nzuri awapayo Bwana.
18 Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu.
19 Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.
20 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako;
21 ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi Bwana aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi.
22 Kwa kuwa kwamba mtayashika kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye;
23 ndipo Bwana atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuwapita ninyi.
24 Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu.
25 Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; Bwana, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia.
26 Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana;
27 baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo;
28 na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.
29 Tena itakuwa, atakapokuleta Bwana, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali.
30 Je! Haiwi ng'ambo ya Yordani? Nyuma ya njia ya machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waketio katika Araba kuelekea Gilgali, kando ya hiyo mialoni ya More?
31 Kwani ninyi mtavuka Yordani mwingie kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, nanyi muimiliki na kuketi humo.
32 Nanyi angalieni mzifanye amri na hukumu zote niwawekeazo leo mbele yenu.

Kumbukumbu 12


1 Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa Bwana, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi.
2 Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;
3 nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.
4 Wala msimfanyie hivyo Bwana, Mungu wenu.
5 Lakini mahali atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko;
6 pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;
7 na huko mtakula mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia Bwana, Mungu wako.
8 Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama aonavyo vema machoni pake;
9 kwani hamjafikilia bado katika raha na urithi akupao Bwana, Mungu wako.
10 Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha Bwana, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama;
11 wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana.
12 Nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu.
13 Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;
14 bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.
15 Pamoja na haya waweza kuchinja nyama na kula ndani ya malango yako yote, kwa kufuata yote yatamaniwayo na roho yako, kwa mfano wa baraka ya Bwana, Mungu wako, aliyokupa; aliye tohara na asiye tohara ana ruhusa kula katika nyama hiyo, kama ya paa na ya kulungu.
16 Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji.
17 Usile ndani ya malango yako zaka ya nafaka zako, wala ya divai yako, wala ya mafuta yako, wala wazaliwa wa kwanza wa makundi yako, ya ng'ombe wala ya kondoo, wala nadhiri zako uwekazo zo zote, wala sadaka zako za hiari, wala sadaka ya kuinuliwa ya mkono wako;
18 lakini hivyo mtakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, wewe, na mwanao mume na mke, na mtumwa wako mume na mke, na Mlawi aliye ndani ya malango yako; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako, katika yote utakayotia mkono wako.
19 Jilinde nafsi yako usimwache Mlawi siku zote uishizo katika nchi yako.
20 Bwana, Mungu wako, atakapoongeza mpaka wako, kama alivyokuahidi, nawe utakaposema, Nataka kula nyama, kwa kuwa roho yako yatamani kula nyama; waweza kula nyama, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.
21 Na mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apaweke jina lake, pakiwa mbali nawe mno, ndipo utakapochinja katika kundi lako la ng'ombe na kondoo alilokupa Bwana kama nilivyokuagiza, nawe utakula ndani ya malango yako, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.
22 Kama vile aliwavyo paa na kulungu, ndivyo utakavyoila nyama hii; asiyekuwa tohara na aliye tohara wataila pia.
23 Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama.
24 Usiile; imwage juu ya nchi kama maji.
25 Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa Bwana.
26 Ila vitu vyako vitakatifu ulivyo navyo, na nadhiri zako, uvitwae ukaende mahali atakapochagua Bwana;
27 nawe zisongeze sadaka zako za kuteketezwa, nyama na damu, juu ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako; na damu ya dhabihu zako uimwage juu ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako, na wewe utakula nyama yake.
28 Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa Bwana, Mungu wako.
29 Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao;
30 ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo.
31 Usimtende kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto.
32 Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.

Kumbukumbu 13


1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako.
6 Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;
7 katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;
8 usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;
9 mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote.
10 Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
11 Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.
12 Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo Bwana, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa,
13 Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua;
14 ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako;
15 hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo, na wanyama walio humo, kwa makali ya upanga.
16 Na nyara zake zote uzikusanyie katikati ya njia yake; na mji uuteketeze kwa moto, na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa Bwana, Mungu wako; nao utakuwa magofu milele; usijengwe tena.
17 Kisishikamane na mkono wako kitu cho chote katika kitu kilichoharimishwa; ili ageuke Bwana na ukali wa hasira zake akurehemu, akuonee huruma, na kukufanya kuwa wengi, kama alivyowaapia baba zako;
18 utakaposikiza sauti ya Bwana, Mungu wako kwa kushika maagizo yake yote nikuagizayo leo, ufanye yaliyoelekea machoni pa Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu 14


1 Ninyi mmekuwa wana wa Bwana, Mungu wenu; msijitoje miili yenu, wala msifanye upaa katikati ya macho yenu kwa ajili ya aliyekufa.
2 Kwa kuwa u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, na Bwana amekuchagua kuwa watu wake hasa, kuliko mataifa yote yaliyo juu ya uso wa nchi.
3 Usile kitu cho chote kichukizacho.
4 Wanyama mtakaokula ni hawa ng'ombe, na kondoo, na mbuzi,
5 kulungu, na paa, na kongoni, na mbuzi wa mwitu, na paa mweupe, na pofu, na mbuzi wa mlima;
6 na kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, ukapasuka ukwato wake zikawa mbili, naye ni mnyama mwenye kucheua akatafuna tena, katika wanyama wote, ndiye mnyama mtakayemla.
7 Lakini, hawa msile katika wale wenye kucheua, na hao waliopasuliwa ukwato; ngamia, na sungura, na kwang'a, kwa kuwa hucheua, lakini hawakupasuliwa kwato, ni najisi kwenu;
8 na nguruwe, kwa kuwa amepasuliwa ukwato lakini hacheui, huyu ni najisi kwenu msile nyama zao, wala mizoga yao msiiguse.
9 Mtakula hawa katika wote walio majini; kila kilicho na mapezi na magamba mtakula;
10 na kila kisichokuwa na mapezi na magamba msile; ni najisi kwenu.
11 Mna ruhusa kula katika nyuni wote walio safi.
12 Lakini hawa msiwale; tai, na furukombe, na kipungu;
13 na kengewa, na kozi, na mwewe kwa aina zake;
14 na kila kunguru kwa aina zake;
15 na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake;
16 na bundi, na mumbi, na bundi mkubwa;
17 na mwari, na nderi, na mnandi;
18 na membe, na koikoi, kwa aina zake; na hudihudi, na popo.
19 Na wadudu wote watambaao wenye mabawa ni najisi kwenu; msiwale.
20 Mna ruhusa kula katika nyuni wote walio safi.
21 Msile nyamafu yo yote; waweza kumpa mgeni aliye ndani ya malango yako, ili apate kula; au kumliza mtu wa mataifa; kwa kuwa wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mamaye.
22 Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.
23 Nawe utakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng'ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wako, daima.
24 Na njia ikiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia Bwana, Mungu wako;
25 ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako;
26 na zile fedha zitumie kwa cho chote itakachotamani roho yako, ng'ombe, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako cho chote; nawe utakula huko mbele za Bwana, Mungu wako; tena furahi, wewe na nyumba yako;
27 na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe.
28 Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako;
29 na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.

Kumbukumbu 15


1 Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio.
2 Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana.
3 Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia.
4 Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa Bwana atakubarikia kweli katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;)
5 kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya.
6 Kwani Bwana, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.
7 Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini;
8 lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo.
9 Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako.
10 Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia Bwana, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako.
11 Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako.
12 Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.
13 Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu;
14 umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia Bwana, Mungu wako.
15 Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.
16 Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako;
17 ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo.
18 Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na Bwana, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.
19 Wazaliwa wa kwanza waume wote wazaliwao katika kundi lako la ng'ombe na la kondoo, uwatakase kwa Bwana, Mungu wako; usifanye kazi kwa mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wako, wala usimkate manyoya mzaliwa wa kwanza wa kundi lako la kondoo.
20 Utamla mbele za Bwana, Mungu wako, mwaka hata mwaka mahali atakapochagua Bwana, wewe na nyumba yako.
21 Lakini akiwa na kilema, akichechea, au akiwa kipofu, au mwenye kilema kibaya cho chote, usimsongezee Bwana, Mungu wako, sadaka.
22 Utamla ndani ya malango yako; wasio tohara na wenye tohara pia watakula, kama unavyokula paa na kulungu.
23 Pamoja na haya usile damu yake; uimwage nchi kama maji.

Kumbukumbu 16


1 Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie pasaka Bwana, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku Bwana; Mungu wako.
2 Nawe umchinjie pasaka Bwana, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua Bwana apakalishe jina lake.
3 Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako.
4 Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale cho chote usiku kucha hata asubuhi.
5 Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo Bwana, Mungu wako;
6 ila mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
7 Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.
8 Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa Bwana, Mungu wako, usifanye kazi yo yote.
9 Jihesabie majuma saba; tangu wakati uanzao kutia mundu katika mmea utaanza kuhesabu majuma saba.
10 Nawe sikukuu ya majuma umfanyie Bwana, Mungu wako, kwa kutoa sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayotoa kwa kadiri akubarikiavyo Bwana, Mungu wako;
11 nawe utafurahi mbele ya Bwana, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake.
12 Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa huko Misri; tena zishike amri hizi kwa kuzifanya.
13 Fanya sikukuu ya vibanda siku saba, utakapokwisha kuyakusanya yatokayo katika sakafu yako ya nafaka, na katika kinu chako cha divai;
14 nawe utafurahi katika sikukuu yako, wewe, na mwanao, na binti yako, na mtumwa wako, na mjakazi wako, na Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako.
15 Siku saba mfanyie sikukuu Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua Bwana; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, atakubarikia katika maongeo yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa.
16 Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.
17 Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa.
18 Weka waamuzi na maakida katika malango yako yote akupayo Bwana, Mungu wako, kwa hesabu ya kabila zako; nao wawaamue watu kwa maamuzi ya haki.
19 Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki.
20 Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.
21 Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako.
22 Wala usisimamishe nguzo; ambayo Bwana, Mungu wako, aichukia.

Kumbukumbu 17


1 Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.
2 Ikiwa ameonekana katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, upewayo na Bwana, Mungu wako, mtu mume au mke afanyaye yaliyo maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, kwa kuvunja maagano yake,
3 naye amekwenda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, au jua, au mwezi, au vilivyo katika jeshi la mbinguni vyo vyote, nisivyoagiza mimi;
4 ukiambiwa hayo nawe umeyasikia, ndipo utafute kwa bidii, na tazama, ikiwa ni kweli lina hakika jambo lile, kuwa yafanywa machukizo kama hayo katika Israeli;
5 ndipo umchukue nje malangoni kwako, yule mtu mume, au yule mwanamke, aliyefanya jambo lile ovu; ukawapige kwa mawe, wafe.
6 Huyo atakayeuawa na auawe kwa midomo ya mashahidi wawili, au mashahidi watatu; asiuawe kwa mdomo wa shahidi mmoja.
7 Mikono ya wale mashahidi na iwe juu yake kwanza kwa kumwua, kisha mikono ya watu wote. Uondoe vivyo uovu katikati yako.
8 Ikiwa limezuka neno lililo zito kukupita wewe, katika maamuzi kati ya damu na damu, na kati ya daawa na daawa, na kati ya pigo na pigo, nayo yashindaniwa katika malango yako; ndipo nawe uondoke, ukwee uende mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako;
9 uwaendee makuhani Walawi, na mwamuzi atakayekuwako siku hizo; uwaulize; nao watakuonyesha hukumu ya maamuzi;
10 nawe fanya sawasawa na hukumu watakayokuonyesha mahali hapo atakapochagua Bwana; nawe tunza kufanya kwa mfano wa yote watakayokufunza;
11 kwa mfano wa sheria watakayokufunza, na kwa mfano wa hukumu watakayokuambia, fanya vivyo; usigeuke katika hukumu watakayokuonyesha, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto.
12 Na mtu afanyaye kwa kujikinai, kwa kutomsikiza kuhani asimamaye hapo kwa kumtumikia Bwana, Mungu wako, au mwamuzi, na afe mtu huyo; nawe utauondoa uovu katika Israeli.
13 Na hao watu wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena kwa kujikinai.
14 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu;
15 usiache kumweka yule atakayechaguliwa na Bwana, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako.
16 Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa Bwana amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile.
17 Wala asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno.
18 Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi;
19 na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya;
20 moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kuume wala wa kushoto; ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe, katikati ya Israeli.

Kumbukumbu 18


1 Makuhani Walawi, kabila yote ya Lawi, wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli; watakula sadaka za Bwana zifanywazo kwa moto, na urithi wake.
2 Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.
3 Na hii itakuwa haki ya makuhani kwa watu hao wasongezao sadaka, ikiwa ni ng'ombe au kondoo wampe kuhani mkono, na mashavu mawili, na tumbo.
4 Malimbuko ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na manyoya ya kwanza ya kondoo zako, umpe.
5 Kwani Bwana, Mungu wako, amemchagua katika kabila zako zote, asimame atumike kwa jina la Bwana, yeye na wanawe milele.
6 Na akija Mlawi atokaye katika malango yako mojawapo, katika Israeli yote alipokuwa akikaa, akaja kwa mapenzi yote ya nafsi yake mahali atakapochagua Bwana;
7 na atumike kwa jina la Bwana, Mungu wake, kama wafanyavyo ndugu zake wote, Walawi wasimamao huko mbele za Bwana.
8 Wawe na fungu sawasawa la kula, pamoja na haya yaliyomfikilia kwa kuuzwa urithi wa baba zake.
9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.
10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.
12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.
13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.
14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.
15 Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.
16 Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa.
17 Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema.
18 Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
19 Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.
20 Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.
21 Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena Bwana?
22 Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope

Kumbukumbu 19


1 Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao;
2 itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki.
3 Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo Bwana, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko.
4 Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo;
5 kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai;
6 asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.
7 Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu.
8 Na kama Bwana, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako;
9 nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda Bwana, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile;
10 isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako.
11 Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo;
12 ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumuua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa.
13 Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa.
14 Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki.
15 Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.
16 Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe;
17 ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za Bwana, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo;
18 nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye;
19 ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
20 Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.
21 Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.

Kumbukumbu 20


1 Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.
2 Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu,
3 awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;
4 kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi.
5 Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine.
6 Ni mtu gani aliye hapa aliyepanda shamba la mizabibu, wala hajatumia matunda yake? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, yakatumiwa na mtu mwingine matunda yake.
7 Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine.
8 Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake.
9 Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu.
10 Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani.
11 Itakuwa utakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa, na kukutumikia.
12 Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru;
13 na Bwana, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga;
14 lakini wanawake na watoto, na wanyama wa miji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa Bwana, Mungu wako.
15 Utaifanyia vivyo miji yote iliyo mbali sana nawe, isiyokuwa miji ya mataifa haya.
16 Lakini katika miji ya mataifa haya akupayo Bwana, Mungu wako, kuwa urithi, usihifadhi kuwa hai kitu cho chote kipumzikacho;
17 lakini uwaangamize kabisa, Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, kama alivyokuamuru Bwana, Mungu wako;
18 wasije wakawafunza kufanya mfano wa machukizo yao yote, waliyoifanyia miungu yao; hivyo itakuwa ni makosa juu ya Bwana, Mungu wenu.
19 Wewe utakapohusuru mji siku nyingi kwa kufanya vita juu yake, upate kuutwaa, usiangamize miti yake kwa kupeleka shoka juu yake, kwani utaweza kula matunda yake; wala usiiteme, kwa maana huo mti wa kondeni, je! Ni mtu, hata ukauzuie?
20 Ila miti uijuayo si miti ya kuliwa iangamize, na kuitema; ukajenge maburuji juu ya mji ufanyao vita juu yako, hata uanguke.

Kumbukumbu 21


1 Aonekanapo mtu ameuawa katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki, amelala kondeni, wala haijulikani ni nani aliyempiga;
2 na watoke nje wazee wako na waamuzi wako, nao wapime hapo mpaka miji iliyomzunguka huyo aliyeuawa;
3 na iwe, mji ulio karibu na yule aliyeuawa, wale wazee wake mji huo watwae mtamba katika kundi la ng'ombe, ambaye hajafanya kazi, wala hajakokota jembe la nira;
4 wazee wa mji huo na wamshushe yule mtamba mpaka bonde lenye maji ya mtoni, lisilolimwa wala kupandwa, wakamvunje yule mtamba shingo yake humo bondeni;
5 nao makuhani wana wa Lawi wasongee karibu, kwa kuwa ndio aliowachagua Bwana, Mungu wako, wamtumikie, na kubariki katika jina la Bwana na kila neno lishindaniwalo, na kila pigo, litakuwa kwa kufuata maneno yao;
6 na wazee wote wa mji ule, ulio karibu sana na yule aliyeuawa, na waoshe mikono yao juu ya huyo mtamba aliyevunjwa shingo yake humo bondeni;
7 na wajibizane kwamba, Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuiona.
8 Ee Bwana, samehe watu wako Israeli, uliowakomboa, wala usiache damu ya asiye makosa ikakaa katikati ya watu wako Israeli. Na ile damu utasamehewa kwao.
9 Ndivyo utakavyoondoa damu ya asiye makosa katikati yako, utakapofanya yaliyo sawa machoni pa Bwana.
10 Utakapokwenda vitani kupigana juu ya adui zako, na Bwana, Mungu wako, awatiapo mikononi mwako, nawe uwachukuapo mateka,
11 ukaona kati ya mateka mwanamke mzuri, ukafanya tamaa kwake, ukawaza kumtwaa kuwa mkeo;
12 ndipo umchukue kwenu nyumbani kwako, naye atanyoa kichwa, akate na kucha;
13 avue na mavazi ya uteka wake akae nyumbani mwako, awakalie matanga babaye na mamaye mwezi mzima, kisha uingie kwake uwe mumewe, naye awe mkeo.
14 Tena utakapokuwa huna furaha naye, mpe ruhusa aende atakako; lakini usimwuze kabisa kwa fedha, usimfanye kama mtumwa, kwa kuwa ulimtweza.
15 Akiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa;
16 ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu;
17 lakini amkubali mzaliwa wa kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.
18 Mtu akiwa na mwana mkaidi, mshupavu, asiyetii sauti ya baba yake, wala sauti ya mama yake, nao wajapomwadhibu hawasikizi,
19 ndipo babaye na mamaye na wamkamate, na kumpeleka kwa wazee wa mji wake, katika lango la mahali pake;
20 wawaambie wazee wa mji wake, Huyu mwana wetu ni mkaidi, mshupavu, hasikizi sauti yetu; ni mwasherati, tena ni mlevi.
21 Waume wote wa mji wake na wamtupie mawe, afe; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako; na Israeli wote watasikia na kuogopa.
22 Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti;
23 mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi wako.

Kumbukumbu 22


1 Umwonapo ng'ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo.
2 Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie.
3 Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona.
4 Umwonapo punda wa nduguyo, au ng'ombe wake, ameanguka kando ya njia, usijifiche kama usiyemwona; sharti umsaidie kumwinua tena.
5 Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.
6 Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;
7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi.
8 Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko.
9 Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako.
10 Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja.
11 Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja.
12 Ujifanyizie vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika.
13 Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia,
14 kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira;
15 ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni;
16 na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia;
17 angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji.
18 Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi,
19 wamtoze shekeli mia za fedha, wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli; naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.
20 Lakini likiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira;
21 na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
22 Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli.
23 Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye;
24 watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
25 Lakini yule mtu mume kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee;
26 lakini yule kijana usimfanye neno; hana dhambi yule kijana ipasayo kuuawa, kwa kuwa ni mfano wa mtu kumwondokea mwenzake akamwua, ni vivyo lilivyo jambo hili;
27 kwani alimkuta kondeni; yule kijana aliyeposwa akalia, pasiwe na mtu wa kumwokoa.
28 Mtu mume akimwona kijana aliye mwanamwali ambaye hajaposwa, akamshika na kulala naye, wakaonekana;
29 yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote.
30 Mtu mume asimtwae mke wa baba yake, wala asifunue ncha ya mavazi ya baba yake.

Kumbukumbu 23


1 Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa Bwana.
2 Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa Bwana; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa Bwana.
3Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele;
4kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize.
5Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda Bwana, Mungu wako.
6Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele.
7Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake.
8Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa Bwana.
9Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya.
10Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;
11lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.
12Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;
13nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;
14kwa kuwa Bwana. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.
15Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;
16na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.
17Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.
18Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.
19Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;
20mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.
21Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.
22Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.
23Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.
24Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.
25Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.

Kumbukumbu 24


1 Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake, kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake.
2Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine.
3Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe;
4yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za Bwana; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi.
5Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa.
6Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani.
7Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
8Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao.
9Kumbukeni na Bwana, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri.
10Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake.
11Simama nje, yule umkopeshaye akuletee nje ile rehani.
12Naye akiwa ni mtu maskini, usilale na rehani yake.
13Sharti umrudishie rehani lichwapo jua, apate kulala na mavazi yake, na kukubarikia; nayo itakuwa ni haki kwako mbele za Bwana, Mungu wako.
14Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji, kama ni wa nduguzo, au kama ni wageni wako mmojawapo walio katika nchi yako, ndani ya malango yako;
15mpe ujira wake kwa siku yake, wala jua lisichwe juu yake; kwa maana ni maskini, moyo wake umeutumainia huo; asije akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako.
16Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
17Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani;
18bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.
19Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako.
20Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.
21Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.
22Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.

Kumbukumbu 25


1 Pakiwa na mashindano kati ya watu, wakaenda maamuzini, na hao waamuzi wakawaamua; na wampe haki mwenye haki, na wamhukumie makosa yule mwovu;
2na iwe, ikimpasa kupigwa yule mwovu, alazwe chini na mwamuzi, na kupigwa mbele ya uso wake, kwa kadiri ya uovu wake, kwa kuhesabu.
3Aweza kumpiga fimbo arobaini asizidishe asije akaonekana nduguyo kuwa amedharauliwa kwako, azidishapo kwa kumpiga fimbo nyingi juu ya hizi.
4Ng'ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa.
5Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe.
6Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli.
7Na yule mtu kwamba hapendi kumtwaa mke wa nduguye, aende huyo mke wa nduguye langoni kwa wazee, akawaambie, Nduguye mume wangu yuakataa kumsimamishia nduguye jina katika Israeli, hataki kunitimizia yampasayo nduguye mume wangu.
8Ndipo wamwite wazee wa mji wake waseme naye; naye akisimama na kusema, Sitaki mimi kumtwaa mwanamke huyu,
9ndipo mke wa nduguye amkaribie mbele ya hao wazee, amvue kiatu chake mguuni mwake, na kumtemea mate ya uso; kisha atajibu yule mwanamke, aseme, Mume akataaye kumjengea nduguye nyumba yake na afanywe hivi.
10Na jina lake katika Israeli liitwe, Nyumba ya mvuliwa kiatu.
11Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake;
12umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako.
13Usiwe na mawe ya kupimia mbalimbali, kubwa na dogo, katika mfuko wako.
14Usiwe na vipimo mbalimbali, kikubwa na kidogo, katika nyumba yako.
15Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.
16Kwa kuwa wote wayatendao mambo kama haya, wote watendao yasiyo haki, ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako.
17Kumbuka aliyokufanya Amaleki katika njia mlipokuwa mkitoka Misri;
18jinsi alivyokukuta katika njia, akapiga katika watu wako walioachwa nyuma, wote waliokuwa wanyonge nyuma yako, ulipokuwa umechoka na kuzimia; wala asimche Mungu.
19Basi itakuwa, hapo atakapokwisha kukupumzisha Bwana, Mungu wako, katika adui zako wote walio kando-kando, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi uimiliki, ndipo uufute ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu; usisahau.

Kumbukumbu 26


1 Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake;
2 twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko.
3 Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa Bwana, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi Bwana aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.
4 Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako.
5 Nawe ujibu, ukaseme mbele za Bwana, Mungu wako, Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri, akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi.
6 Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito.
7 Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu.
8 Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu;
9 naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.
10 Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako;
11 ukayafurahie mema yote ambayo Bwana, Mungu wako, amekupa, na nyumba yako, wewe, na Mlawi, na mgeni aliye kati yako.
12 Utakapokwisha kutoa zaka, katika zaka zote za maongeo yako mwaka wa tatu, ambao ndio mwaka wa kutolea zaka, umpe zile zaka Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, wapate kula ndani ya malango yako na kushiba;
13 nawe sema mbele ya Bwana, Mungu wako, Vitu vilivyo vitakatifu nimeviondoa katika nyumba yangu, nami mimewapa Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, kwa mfano wa maagizo yako uliyoniusia yote; sikukosa maagizo yako yo yote, wala sikuyasahau;
14 katika vitu hivyo sikula wakati wa kukaa matanga mimi, wala sikuviondoa nikiwa na unajisi, wala sikutoa kwa ajili ya wafu katika vitu hivyo; sauti ya Bwana, Mungu wangu, nimeisikiza, nimefanya yote, kama ulivyoniamuru.
15 Uangalie kutoka makazi yako matakatifu mbinguni, uwabarikie watu wako Israeli, na nchi uliyotupa kama ulivyowaapia baba zetu, nchi imiminikayo maziwa na asali.
16 Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote.
17 Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake;
18 naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote;
19 na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.

Kumbukumbu 27


1 Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo.
2 Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo Bwana, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo,
3 uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi Bwana, Mungu wa baba zako.
4 Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo.
5 Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake.
6 Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake;
7 ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako.
8 Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana.
9 Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa Bwana, Mungu wako.
10 Basi isikize sauti ya Bwana, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo.
11 Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema,
12 Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini;
13 na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali.
14 Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu,
15 Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina.
16 Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina.
17 Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina.
18 Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina.
19 Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina.
20 Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina.
21 Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina.
22 Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina.
23 Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina.
24 Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina.
25 Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina.
26 Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.

Kumbukumbu 28


1 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.
7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8 Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.
9 Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.
10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako.
11 Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.
12 Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.
13 Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;
14 msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.
15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.
17 Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.
18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
19 Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,
20 Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.
21 Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.
22 Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.
23 Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.
24 Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.
25 Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.
26 Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.
27 Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.
28 Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;
29 utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.
30 Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.
31 Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.
32 Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.
33 Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;
34 hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.
35 Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.
36 Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.
37 Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana.
38 Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.
39 Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.
40 Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.
41 Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.
42 Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.
43 Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.
44 Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.
45 Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;
46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;
47 kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;
48 kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
49 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake;
50 taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;
51 naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.
52 Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako.
53 Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako.
54 Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye;
55 hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote.
56 Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,
57 na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.
58 Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, Bwana, MUNGU WAKO;
59 ndipo atakapofanya Bwana mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana.
60 Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe.
61 Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo Bwana juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa.
62 Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako.
63 Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi Bwana juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi Bwana juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.
64 Bwana atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe.
65 Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini Bwana atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;
66 na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako;
67 asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona.
68 Bwana atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena po pote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.

Kumbukumbu 29


1 Haya ndiyo maneno ya agano Bwana alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu.
2 Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote Bwana aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote;
3 yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu;
4 lakini Bwana hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi.
5 Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako.
6 Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
7 Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga;
8 tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi.
9 Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo.
10 Leo mmesimama nyote mbele za Bwana, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli,
11 vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako;
12 ili uingie katika agano la Bwana, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe Bwana, Mungu wako, hivi leo;
13 apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
14 Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki;
15 ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya Bwana, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo;
16 (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao;
17 nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;)
18 asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache Bwana, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;
19 ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu;
20 Bwana hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya Bwana na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu.
21 Bwana atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati.
22 Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia Bwana;
23 ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua Bwana kwa ghadhabu yake na hasira zake;
24 mataifa yote watasema, Mbona Bwana ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa?
25 Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la Bwana, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri;
26 wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye;
27 ndipo ikawashwa hasira ya Bwana juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki;
28 Bwana akawang'oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo.
29 Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.

Kumbukumbu 30


1 Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako,
2 nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;
3 ndipo Bwana, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako.
4 Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa;
5 atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako.
6 Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.
7 Na laana hizi zote Bwana, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa.
8 Nawe utarudi, uitii sauti ya Bwana, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo.
9 Na Bwana, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng'ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa Bwana atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako;
10 ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.
11 Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13 Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;
16 kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.
17 Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia;
18 nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki.
19 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;
20 kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.

Kumbukumbu 31


1 Musa akaenda akawaambia Waisraeli maneno haya yote.
2 Akawaambia, Mimi leo ni mwenye miaka mia na ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani.
3 Bwana Mungu wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena.
4 Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu.
5 Naye Bwana atawatia mikononi mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru.
6 Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.
7 Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi Bwana aliyowaapia baba zao, ya kwamba atawapa; nawe utawarithisha.
8 Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.
9 Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa Lawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, na wazee wote wa Israeli.
10 Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda,
11 Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao.
12 Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii;
13 na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki.
14 Bwana akamwambia Musa, Tazama, siku zako za kufa zinakaribia, umwite Yoshua, nanyi mkajihudhurishe katika hema ya kukutania, ili nipate kumwagiza kazi. Musa na Yoshua wakaenda, wakajihudhurisha ndani ya hema ya kukutania.
15 Bwana akaonekana katika Hema katika nguzo ya wingu; na ile nguzo ya wingu ikasimama juu ya mlango wa Hema.
16 Bwana akamwambia Musa, Angalia, wewe utalala na baba zako; na watu hawa wataondoka, wataifuata kwa ukahaba miungu ya kigeni ya nchi waiendeayo kuwa kati yao, nao wataniacha mimi na kulivunja agano langu, nililofanya nao.
17 Ndipo hasira yangu itakapowaka juu yao siku hiyo, nami nitawaacha, nitawaficha uso wangu, nao wataliwa, tena watajiliwa na mambo maovu mengi na mashaka; hata waseme siku hiyo, Je! Kujiliwa kwetu na maovu haya si kwa sababu Mungu wetu hayumo kati yetu?
18 Nami nitawaficha uso wangu kwa kweli siku hiyo, kwa maovu yote waliyoyafanya, kwa kuigeukia hiyo miungu mingine.
19 Basi sasa jiandikieni wimbo huu, uwafundishe wana wa Israeli; kawatie vinywani mwao, ili uwe shahidi kwangu wimbo huu, juu ya wana wa Israeli.
20 Kwa kuwa nitakapokwisha kuwatia katika nchi niliyowaapia baba zao, imiminikayo maziwa na asali; nao watakapokwisha kula na kushiba, na kuwanda; ndipo watakapoigeukia hiyo miungu mingine, na kuitumikia, na kunidharau mimi, na kulivunja agano langu.
21 Tena itakuwa, wakiisha kujiliwa na mambo maovu mengi na mashaka, utashuhudia wimbo huu mbele yao kama shahidi, kwa maana hautasahauliwa katika vinywa vya uzao wao; kwani nayajua mawazo yao wayawazayo, hata sasa kabla sijawatia katika nchi niliyoapa.
22 Basi Musa akauandika wimbo huu siku iyo hiyo, akawafundisha wana wa Israeli.
23 Akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, Uwe hodari na moyo mkuu, kwa kuwa utawapeleka wana wa Israeli katika nchi niliyowaapia; nami nitakuwa pamoja nawe.
24 Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha,
25 ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la agano la Bwana akawaambia,
26 Twaeni chuo hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako.
27 Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi nikali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya Bwana; siuze nitakapokwisha kufa!
28 Nikutanishieni wazee wote wa kabila zenu, na maakida yenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao.
29 Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa Bwana kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu.
30 Musa akasema maneno ya wimbo huu masikioni mwa kusanyiko la wana wa Israeli hata yakaisha.

Kumbukumbu 32


1 Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.
2 Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua, Maneno yangu yatatona-tona kama umande; Kama manyunyu juu ya majani mabichi; Kama matone ya mvua juu ya mimea.
3 Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu.
4 Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili.
5 Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.
6 Je! Mnamlipa Bwana hivi, Enyi watu wapumbavu na ujinga? Je! Yeye siye baba yako aliyekununua? Amekufanya, na kukuweka imara.
7 Kumbuka siku za kale, Tafakari miaka ya vizazi vingi; Mwulize baba yako, naye atakuonyesha; Wazee wako, nao watakuambia.
8 Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao, Alipowabagua wanadamu, Aliweka mipaka ya watu Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.
9 Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake.
10 Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho;
11 Mfano wa tai ataharikishaye kioto chake; Na kupapatika juu ya makinda yake, Alikunjua mbawa zake, akawatwaa, Akawachukua juu ya mbawa zake;
12 Bwana peke yake alimwongoza, Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.
13 Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka, Naye akala mazao ya mashamba; Akamnyonyesha asali iliyotoka jabalini, Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume;
14 Siagi ya ng'ombe, na maziwa ya kondoo, Pamoja na mafuta ya wana-kondoo, Kondoo waume wa Kibashani, na mbuzi, Na unono wa ngano iliyo nzuri; Ukanywa divai, damu ya mizabibu.
15 Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake.
16 Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo.
17 Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau.
19 Bwana akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.
20 Akasema, Nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio imani ndani yao.
21 Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; Wamenikasirisha kwa ubatili wao; Nami nitawatia wivu kwa wasio watu, Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo.
22 Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, Unateketea hata chini ya kuzimu, Unakula dunia pamoja na mazao yake, Unaunguza misingi ya milima.
23 Nitaweka madhara juu yao chunguchungu; Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe;
24 Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto, Na uharibifu mkali; Nitawapelekea meno ya wanyama wakali, Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini.
25 Nje upanga utawafifiliza Na ndani ya vyumba, utisho; Utaangamiza mvulana na msichana, Anyonyaye pamoja na mwenye mvi,
26 Nalisema, Ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu;
27 Isipokuwa naliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo, Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka, Wala Bwana hakuyafanya haya yote.
28 Maana hawa ni taifa wasio shauri, Wala fahamu hamna ndani yao.
29 Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao.
30 Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa?
31 Maana, Mwamba wao si kama Mwamba wetu, Hata adui zetu wenyewe ndivyo wahukumuvyo.
32 Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Sodoma, Nao ni wa mashamba ya Gomora; Zabibu zao ni zabibu za uchungu, Vichala vyao ni vichungu.
33 Mvinyo yao ni sumu ya majoka, Uchungu mkali wa nyoka.
34 Je! Haya hayakuwekwa akiba kwangu? Na kutiwa muhuri kati ya hazina yangu?
35 Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao; Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
36 Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumwa wake, Aonapo ya kuwa nguvu zao zimeondoka, Na ya kuwa habaki mtu, aliyefungwa wala asiyefungwa,
37 Naye atasema, Iko wapi miungu yao, Mwamba ule walioutumaini;
38 Uliokula shahamu za sadaka zao, Na kunywa divai ya sadaka zao za kinywaji? Na waondoke na kuwasaidia ninyi; Na wawe hao himaya yenu.
39 Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,
40 Maana, nainua mkono wangu mbinguni, Na kusema, Kama Mimi niishivyo milele,
41 Nikiunoa upanga wangu wa umeme, Mkono wangu ukishika hukumu, Nitawatoza kisasi adui zangu, Nitawalipa wanaonichukia.
42 Nitailevya mishale yangu kwa damu, Na upanga wangu utakula nyama; Pamoja na damu ya waliouawa na waliotekwa nyara, Katika vichwa vya wakuu wa adui.
43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake; Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake, Atawatoza kisasi adui zake, Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake.
44 Musa akaja akasema maneno haya yote ya wimbo huu masikioni mwa watu, yeye na Yoshua, mwana wa Nuni.
45 Musa akamaliza kuwaambia Israeli wote maneno haya yote;
46 akawaambia, Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo nashuhudia kwenu hivi leo; nayo waamuruni watoto wenu, wayatunze na kuyafanya maneno yote ya torati hii.
47 Kwa maana si jambo lisilofaa kwenu; maana, ni maisha yenu, na kwa jambo hili mtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki.
48 Bwana akasema na Musa siku iyo hiyo, akamwambia,
49 Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki;
50 ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe pamoja na watu wake;
51 kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli.
52 Kwani utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli.

Kumbukumbu 33


1 Hii ndiyo baraka ya Musa, huyo mtu wa Mungu, aliyowabarikia wana wa Israeli kabla ya kufa kwake.
2 Akasema,Bwana alitoka Sinai,Akawaondokea kutoka Seiri;Aliangaza katika kilima cha Parani,Akaja Meribath-Kadeshi.Upande wake wa kuume Palikuwa na sheria ya moto-moto kwao.
3 Hakika awapenda hayo makabila ya watu; Watakatifu wake wote wamo mkononi mwako; Nao waliketi miguuni pako; Watapokea kila mmoja katika maneno yako.
4 Musa alituagiza torati, Ni urithi kwa mkutano wa Yakobo.
5 Akawa mfalme katika Yeshuruni, Walipokutanika wakuu wa watu, Makabila yote ya Israeli pamoja.
6 Reubeni na aishi, asife; Lakini watu wake na wawe wachache.
7 Na baraka ya Yuda ni hii; akasema, Isikize, Ee Bwana, sauti ya Yuda, Umlete ndani kwa watu wake; Alijitetea kwa mikono yake; Nawe utakuwa msaada juu ya adui zake.
8 Akamnena Lawi, Thumimu yako na Urimu yako vina mtakatifu wako, Uliyemjaribu huko Masa; Ukateta naye kwenye maji ya Meriba.
9 Aliyemtaja baba yake na mama yake, Mimi sikumwona; Wala nduguze hakuwakubali; Wala hakuwajua watoto wake mwenyewe; Maana wameliangalia neno lako, Wamelishika agano lako.
10 Watamfundisha Yakobo hukumu zako, Na Israeli torati yako, Wataweka uvumba mbele zako, Na sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni mwako.
11 Ee Bwana, ubariki mali zake, Utakabali kazi ya mikono yake; Uwapige viuno vyao waondokao juu yake, Na wenye kumchukia, wasiinuke tena.
12 Akamnena Benyamini, Mpenzi wa Bwana atakaa salama kwake; Yuamfunika mchana kutwa, Naye hukaa kati ya mabega yake.
13 Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na Bwana; Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande, Na kwa kilindi kilalacho chini,
14 Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, Na kwa vitu vilivyo bora vya maongeo ya miezi,
15 Na kwa vitu viteule vya milima ya kale, Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele,
16 Na kwa vitu vilivyo bora vya nchi, na kujaa kwake, Na uradhi wake aliyekaa ndani ya kile kijiti; Na ije baraka juu ya kichwa chake Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliyetengwa na nduguze.
17 Mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wake mume, enzi ni yake; Na pembe zake ni pembe za nyati; Kwa hizo atayasukuma mataifa yote, hata ncha za nchi; Nao ni makumi ya maelfu ya Efraimu, Nao ni maelfu ya Manase.
18 Na Zabuloni akamnena, Furahi Zabuloni, katika kutoka kwako;
19 Watayaita mataifa waje mlimani; Wakasongeze huko sadaka za haki; Kwa kuwa watanyonya wingi wa bahari, Na akiba zilizofichamana za mchangani.
20 Na Gadi akamnena, Na abarikiwe amwongezaye Gadi; Yeye hukaa kama simba mke, Hurarua mkono, naam, na utosi wa kichwa.
21 Akajichagulia sehemu ya kwanza, Kwani ndiko lilikowekwa fungu la mtoa-sheria; Akaja pamoja na wakuu wa watu, Akaitekeleza haki ya Bwana, Na hukumu zake kwa Israeli.
22 Na Dani akamnena, Dani ni mwana-simba, Arukaye kutoka Bashani.
23 Na Naftali akamnena, Ee Naftali, uliyeshiba fadhili, Uliyejawa na baraka ya Bwana; Umiliki magharibi na kusini.
24 Na Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta.
25 Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.
26 Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni, Ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie. Na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27 Mungu wa milele ndiye makazi yako, Na mikono ya milele i chini yako. Na mbele yako amemsukumia mbali adui; Akasema, Angamiza.
28 Na Israeli anakaa salama, Chemchemi ya Yakobo peke yake, Katika nchi ya ngano na divai; Naam, mbingu zake zadondoza umande.
29 U heri, Israeli. Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na Bwana! Ndiye ngao ya msaada wako, Na upanga wa utukufu wako; Na adui zako watajitiisha chini yako, Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.

Kumbukumbu 34


1 Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. Bwana akamwonyesha nchi yote ya Gileadi hata Dani;
2 na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi;
3 na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari.
4 Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko.
5 Basi Musa, mtumishi wa Bwana, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la Bwana.
6 Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo.
7 Musa alikuwa mtu wa miaka mia na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.
8 Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha.
9 Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.
10 Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;
11 katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote;
12 na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.