Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31
1 Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu
2 naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto.
3 Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko.
4 Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao;
5 lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo.
6 Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.
7 Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula.
8 Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?
9 Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana.
10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana.
11 Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.
12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake.
13 Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa.
14 Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako.
15 Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana.
16 Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa.
17 Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.
18 Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena.
19 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka.
20 Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.
21 Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea Bwana dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake.
22 Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za Bwana, akae huko daima.
23 Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hata utakapomwachisha maziwa; Bwana na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hata akamwachisha maziwa.
24 Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga,na chupa ya divai,akamleta nyumbani kwa BWANA,huko Shilo ;na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo.
25 Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli.
26 Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana.
27 Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba;
28 kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.
1 Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;
2 Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.
3 Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.
4 Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
5 Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.
6 Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu.
8 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake.
9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda;
10 Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake.
11 Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia Bwana mbele yake Eli, kuhani.
12 Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali Bwana,
13 wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu ye yote alipotoa dhabihu wakati wo wote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake;
14 naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko.
15 Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi.
16 Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu.
17 Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya Bwana.
18 Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za Bwana, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani.
19 Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka.
20 Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, Bwana na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa Bwana. Kisha wakaenda nyumbani kwao.
21 Naye Bwana akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za Bwana.
22 Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.
23 Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote.
24 Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana.
25 Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana amekusudia kuwaua.
26 Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa Bwana, na kwa watu pia.
27 Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, Bwana asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao?
28 Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa mbari ya baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto?
29 Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema?
30 Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.
31 Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa mbari ya baba yako, hata nyumbani mwako hatakuwako mzee.
32 Nawe utalitazama teso la maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hatakuwako mzee milele.
33 Tena mtu wa kwako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa wapatapo kuwa watu wazima.
34 Na hii ndiyo ishara itakayokuwa kwako, itakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; watakufa wote wawili katika siku moja.
35 Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele.
36 Kisha itakuwa, ya kwamba kila mtu atakayesalia katika nyumba yako atakwenda kumsujudia, apate kipande kidogo cha fedha, na mkate mmoja; na kumwambia, Tafadhali unitie katika kazi mojawapo ya ukuhani, nipate kula kipande kidogo cha mkate.
1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.
2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),
3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;
4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.
5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.
6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.
7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.
9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.
10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.
11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.
12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.
13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.
14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.
15 Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya Bwana. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo.
16 Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa.
17 Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote Bwana aliyosema nawe.
18 Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema.
19 Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.
20 Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana.
21 Naye Bwana akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa Bwana akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la Bwana. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.
1 [Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani;wakatua karibu na Ebenezeri ,nao Wafilisti wakatua huko Afeki.
2 Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne.
3 Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu.
4 Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu.
5 Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma.
6 Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini.
7 Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo.
8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani.
9 Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao.
10 Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu.
11 Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.
12 Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake.
13 Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia.
14 Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli.
15 Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona.
16 Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu?
17 Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa.
18 Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini.
19 Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia.
20 Hata alipokuwa katika kufa, wale wanawake waliohudhuria karibu naye wakamwambia, Usiogope; kwa maana umezaa mtoto mwanamume. Walakini hakujibu, wala hakumtazama.
21 Akamwita mtoto, Ikabodi, akisema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; kwa sababu sanduku la Mungu lilikuwa limetwaliwa, na kwa sababu ya mkwewe na mumewe.
22 Naam, akasema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; maana sanduku la Mungu limetwaliwa.
1 Basi Wafilisti walikuwa wamelichukua sanduku la Mungu, wakaenda nalo kutoka Eben-ezeri hata Ashdodi.
2 Wafilisti wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka karibu na Dagoni.
3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili, kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena.
4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu.
5 Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo.
6 Lakini mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake.
7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu.
8 Basi wakatuma watu waende kuwakusanya kwao mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Mungu wa Israeli? Nao wakajibu, Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishwe liende Gathi. Wakalihamisha sanduku la Mungu wa Israeli.
9 Ikawa, walipokwisha lihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa juu ya mji huo, kwa kuwafadhaisha sana; akawapiga watu wa mjini, wadogo kwa wakubwa, wakapatwa na majipu.
10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu mpaka Ekroni. Ikawa, sanduku la Mungu lilipofika Ekroni, watu wa Ekroni walifanya kelele, wakasema, Wamelileta hilo sanduku la Mungu wa Israeli kwetu, hata kutuua sisi na watu wetu.
11 Kwa hiyo wakatuma watu waende kuwakusanya mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Liondoeni hilo sanduku la Mungu wa Israeli, liende tena mahali pake, ili lisituue sisi, wala watu wetu; kwa sababu kulikuwa na fadhaa kubwa sana mjini mwote; mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko.
12 Na wale wasiokufa walipigwa kwa yale majipu; na kilio cha mji kikafika mbinguni.
1 Basi, hilo sanduku la Bwana lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba.
2 Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Bwana? Tuonyesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake.
3 Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu.
4 Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa yatakuwa ya namna gani, hayo tutakayompelekea? Nao wakajibu, Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya mashehe wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya mashehe wenu.
5 Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu.
6 Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao?
7 Basi sasa jifanyizieni gari jipya, mtwae na ng'ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng'ombe garini, na kuwaondoa ndama zao na kuwatia zizini;
8 kisha, litwaeni hilo sanduku la Bwana, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda.
9 Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni ajali iliyotupata.
10 Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng'ombe wawili wakamwao, wakawafunga garini, na ndama zao wakawafunga zizini;
11 kisha wakaliweka sanduku la Bwana juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao.
12 Na hao ng'ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi.
13 Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona.
14 Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng'ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
15 Nao Walawi walilishusha sanduku la Bwana, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa Bwana.
16 Na hao mashehe watano wa Wafilisti, hapo walipokwisha kuyaona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo.
17 Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa Bwana; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja;
18 na panya wa dhahabu, kwa idadi ya miji yote ya Wafilisti, milki zao wale mashehe watano, miji yenye maboma na vijiji vya mashamba pia. Nalo lile jiwe kubwa, ambalo juu yake waliliweka sanduku la Bwana, liko hata hivi leo hapo kondeni pa Yoshua wa Beth-shemeshi.
19 Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu.
20 Nao watu wa Beth-shemeshi wakasema, Ni nani awezaye kusimama mbele za Bwana, huyu Mungu mtakatifu? Naye atapanda kwenda kwa nani kutoka kwetu?
21 Nao wakatuma wajumbe waende kwa wenyeji wa Kiriath-yearimu, kusema, Wafilisti wamelirudisha sanduku la Bwana; basi shukeni, mkalichukue kwenu.
1 Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la Bwana, wakalileta ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la Bwana.
2 Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea Bwana.
3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti.
4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake.
5 Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.
6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.
7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.
8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.
9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia.
10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.
11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari.
12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia.
13 Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli.
14 Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori.
15 Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake.
16 Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua Israeli mahali hapo pote.
17 Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea Bwana madhabahu.
1 Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli.
2 Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba.
3 Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.
4 Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;
5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.
6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.
7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.
8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.
9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.
10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.
11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.
12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.
13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.
14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.
15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.
16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe.
17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.
18 Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; Bwana asiwajibu siku ile.
19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;
20 ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu.
21 Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana.
22 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.
1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.
2 Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.
3 Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao.
4 Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata.
5 Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi.
6 Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea.
7 Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi?
8 Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu.
9 (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.)
10 Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu.
11 Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?
12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu;
13 mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona.
14 Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu.
15 Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,
16 Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.
17 Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.
18 Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?
19 Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.
20 Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?
21 Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?
22 Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini.
23 Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke akiba.
24 Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa akiba ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hata wakati uliokusudiwa, maana nalisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo.
25 Hata waliposhuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, akaongea na Sauli darini.
26 Nao wakaamka alfajiri; kisha ikawa, kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli darini, akisema, Inuka, nikupeleke kwenu. Basi Sauli akainuka, nao wakatoka wote wawili, yeye na Samweli.
27 Hata walipokuwa wakishuka mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, Mwambie mtumishi atangulie, (naye akatangulia), bali wewe simama hapa sasa, ili nikuambie neno la Mungu.
1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake.
2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu?
3 Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai;
4 nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao.
5 Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri;
6 na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine.
7 Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
8 Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya.
9 Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile.
10 Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao.
11 Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?
12 Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n'nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?
13 Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu.
14 Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli.
15 Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje?
16 Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo.
17 Basi Samweli akawakusanya watu mbele za Bwana huko Mispa
18 akawaambia wana wa Israeli, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea;
19 lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za Bwana, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu.
20 Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.
21 Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana.
22 Basi wakazidi kumwuliza Bwana, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye Bwana akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo.
23 Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu.
24 Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na Bwana, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi!
25 Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za Bwana. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake.
26 Sauli naye akaenda nyumbani kwake huko Gibea; na pamoja naye wakaenda kikosi cha watu, ambao Mungu alikuwa ameigusa mioyo yao.
27 Walakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je! Atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi.
1 Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni ,akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi;na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi,na sisi tutakutumikia.
2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia.
3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea.
4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia.
5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6 Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana.
7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue.
13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika Israeli.
14 Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuimarishe ufalme huko mara ya pili.
15 Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za Bwana huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za Bwana; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.
1 Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu.
2 Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo.
3 Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za Bwana, na mbele ya masihi wake,nalitwaa ng`ombe wa nani? au nalitwaa punda wa nani? au ni nani niliye mdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi.
4 Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote.
5 Akawaambia, Bwana ni shahidi juu yenu, na masihi
6 Samweli akawaambia watu, Ni yeye Bwana aliyewaweka Musa na Haruni, ndiye yeye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.
7 Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za Bwana, kwa kutaja matendo yote ya haki ya Bwana, aliyowatendea ninyi na baba zenu.
8 Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia Bwana, ndipo Bwana akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa.
9 Lakini wakamsahau Bwana, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao.
10 Nao wakamlilia Bwana, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha Bwana, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa utuokoe na mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe.
11 Bwana akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama.
12 Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa Bwana, Mungu wenu, ni mfalme wenu.
13 Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, Bwana ameweka mfalme juu yenu.
14 Kama mkimcha Bwana, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya Bwana, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata Bwana, Mungu wenu, vema!
15 Bali msipoisikia sauti ya Bwana, mkiiasi amri ya Bwana, ndipo mkono wa Bwana utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.
16 Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, Bwana atakalolitenda mbele ya macho yenu.
17 Leo je! Si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana, kwamba apeleke ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu ni mwingi sana, mlioufanya machoni pa Bwana, kwa kujitakia mfalme.
18 Basi Samweli akamwomba Bwana, naye Bwana akapeleka ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa Bwana sana, na Samweli pia.
19 Watu wote wakamwambia Samweli, Utuombee sisi watumwa wako kwa Bwana, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme.
20 Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote.
21 Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili,
22 visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza Bwana kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe.
23 Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka
24 Mcheni Bwana tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu.
25 Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.
1 Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala;naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli.
2 Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake.
3 Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania.
4 Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali.
5 Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni.
6 Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika.
7 Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka.
8 Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye.
9 Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa.
10 Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu.
11 Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi;
12 basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za Bwana; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa.
13 Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele.
14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile Bwana alilokuamuru.
15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita.
16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi.
17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali;
18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika.
19 Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki;
20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake;
21 ila walikuwa na tupa za kunolea sululu, na miundu, na mauma, na mashoka; na kwa kuinoa michokoo.
22 Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu ye yote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo.
23 Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mwanya wa Mikmashi.
1 Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye.
2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita;
3 na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka.
4 Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene.
5 Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba.
6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.
7 Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako.
8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao.
9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie.
10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana Bwana amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu.
11 Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania watoka katika mashimo walimojificha!
12 Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mchukua silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonyesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa Bwana amewatia mikononi mwa Israeli.
13 Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake.
14 Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulipata kama watu ishirini, katika nafasi kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima.
15 Kukawa na tetemeko katika marago, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji wa nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno.
16 Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huko na huko.
17 Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yeye aliyechukua silaha zake hawapo.
18 Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli
19 Ikawa Sauli alipokuwa katika kusema na kuhani, hayo makelele katika marago ya Wafilisti yakaendelea na kuzidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudisha mkono wako.
20 Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa.
21 Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka maragoni toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
22 Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani.
23 Hivyo Bwana akawaokoa Israeli siku ile; na vita vikapita mbele karibu na Beth-aveni. Wakati huo mbele ya wana wa Israeli.
24 Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula.
25 Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi.
26 Na hapo watu walipokwisha kuingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; walakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo.
27 Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru.
28 Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu.
29 Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nalionja asali hii kidogo.
30 Je! Si zaidi sana, kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti.
31 Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu.
32 Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng'ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.
33 Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya Bwana, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.
34 Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng'ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya Bwana, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng'ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo.
35 Naye Sauli akamjengea Bwana madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea Bwana.
36 Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya yo yote uyaonayo kuwa ni mema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa.
37 Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lo lote siku ile.
38 Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani.
39 Kwa maana, aishivyo Bwana, awaokoaye Israeli, ijapokuwa i katika Yonathani, mwanangu, kufa atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu ye yote aliyemjibu.
40 Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.
41 Kwa hiyo Sauli akamwambia Bwana, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu ,Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa,lakini watu wakapona.
42 Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye Bwana atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,]
43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.
44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.
45 Walakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Aishivyo Bwana, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife.
46 Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao.
47 Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake zote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na po pote alipogeukia, akawashinda.
48 Naye akatenda kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli katika mikono yao waliowateka nyara.
49 Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali;
50 na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli.
51 Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli.
52 Tena, kulikuwa na vita vikali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu ye yote aliyekuwa hodari, au mtu ye yote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.
1 Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya Bwana.
2 Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
3 Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.
4 Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
5 Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
6 Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
7 Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
8 Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.
9 Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.
10 Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema,
11 Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.
12 Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
13 Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana, nimeitimiza amri ya Bwana.
14 Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia?
15 Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.
16 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.
17 Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
18 Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
19 Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?
20 Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
22 Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.
25 Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.
26 Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.
27 Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.
28 Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.
29 Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.
30 Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu Bwana, Mungu wako.
31 Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu Bwana.
32 Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka.
33 Lakini Samweli akamjibu, Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, vivyo hivyo mama yako atafiwa miongoni mwa wanawake. Basi Samweli akamkata Agagi vipande mbele za Bwana huko Gilgali.
34 Na baada ya hayo Samweli akaenda zake kule Rama; naye Sauli akakwea kwenda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.
35 Wala Samweli hakuenda tena kuonana na Sauli hata siku ya kufa kwake; lakini Samweli alikuwa akimlilia Sauli; naye Bwana akaghairi ya kuwa amemtawaza Sauli awe mfalme juu ya Israeli.
1 Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.
2 Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu.
3 Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.
4 Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani?
5 Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu.
6 Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake.
7 Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.
8 Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu.
9 Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu.
10 Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa.
11 Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.
12 Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.
13 Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.
14 Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.
15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.
17 Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.
18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye.
19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.
20 Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe.
21 Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake.
22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu.
23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.
1 Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu.
2 Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti.
3 Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati.
4 Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja.
5 Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba.
6 Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake.
7 Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia.
8 Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi.
9 Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.
10 Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.
11 Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.
12 Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu.
13 Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama.
14 Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli.
15 Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu.
16 Naye yule Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini.
17 Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa uwachukulie ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako;
18 ukampelekee akida wa elfu yao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wa hali gani, kisha uniletee jawabu yao.
19 Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.
20 Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita.
21 Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili.
22 Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake.
23 Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia.
24 Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.
25 Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli.
26 Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?
27 Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua.
28 Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita.
29 Naye Daudi akamjibu, Je! Mimi nimekosa nini sasa? Je! Si neno kubwa hilo?
30 Naye akamgeukia ili kumwelekea mtu mwingine, akasema naye jinsi ile ile; na watu wakamjibu tena jinsi ile ile kama ya kwanza.
31 Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita.
32 Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.
33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.
34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,
35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.
36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
37 Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.
38 Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii.
39 Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua.
40 Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
41 Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia.
42 Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri.
43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.
45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.
46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.
48 Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti.
49 Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi.
50 Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake.
51 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia.
52 Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka ufikapo Gathi, na mpaka malango ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu, mpaka Gathi, na mpaka Ekroni.
53 Kisha wana wa Israeli wakarudi kutoka katika kuwafukuza Wafilisti, wakateka nyara marago yao.
54 Naye Daudi akakitwaa kichwa chake yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu; lakini silaha zake akaziweka hemani mwake.
55 Basi Sauli, hapo alipomwona Daudi akitoka ili kumwendea yule Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, Je! Abneri, kijana huyu ni mwana wa nani? Abneri akamjibu, Ee mfalme, kama iishivyo roho yako, mimi siwezi kusema.
56 Basi mfalme akasema, Uliza wewe, kijana huyu ni mwana wa nani.
57 Hata na Daudi alipokuwa yuarudi kutoka katika kumwua yule Mfilisti, Abneri alimtwaa, akamleta mbele ya Sauli, naye anacho kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake.
58 Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.
1 Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe.
2 Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake.
3 Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe.
4 Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake.
5 Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.
6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.
7 Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.
8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?
9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.
10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.
11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.
13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu.
14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa.
16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.
17 Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya Bwana. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake.
18 Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme?
19 Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi.
20 Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza.
21 Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu.
22 Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme.
23 Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo?
24 Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi.
25 Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti.
26 Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado;
27 basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake.
28 Sauli akaona na kutambua ya kwamba Bwana alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda.
29 Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote.
30 Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatoka; kisha ikawa, kila mara walipotoka, Daudi akatenda kwa busara zaidi ya watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.
1 Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi.
2 Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;
3 na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lo lote nitakuambia.
4 Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana.
5 Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?
6 Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.
7 Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.
8 Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake.
9 Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa Bwana ilimjilia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake.
10 Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule.
11 Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa.
12 Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.
13 Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo.
14 Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Hawezi.
15 Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua.
16 Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake!
17 Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue?
18 Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi.
19 Naye Sauli akaambiwa, kusema, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama.
20 Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.
21 Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri.
22 Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama.
23 Basi akaenda Nayothi huko Rama, na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama.
24 Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu husema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?
1 Kisha Daudi akatoka Nayothi huko Rama, akakimbia, akaenda kwa Yonathani, akasema mbele yake, Nimefanya nini? Uovu wangu ni nini? Dhambi yangu mbele ya baba yako ni nini, hata akaitaka roho yangu?
2 Naye akamwambia, Hasha! Hutakufa; angalia, baba yangu hatendi neno kubwa wala dogo bila kuifunulia mimi, na baba yangu ana sababu gani ya kunificha jambo hili? Sivyo usemavyo.
3 Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo Bwana, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti.
4 Ndipo Yonathani akamwambia Daudi, Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea.
5 Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.
6 Baba yako akiona ya kuwa sipo basi sema, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa, aende upesi Bethlehemu, mji wake, kwa maana iko huko dhabihu ya mwaka kwa ajili ya jamaa yake yote.
7 Basi, akisema, Ni vema, mimi mtumishi wako nitakuwa na amani; bali akikasirika, ujue ya kuwa amekusudia kutenda jambo baya.
8 Basi, unitendee mema mimi mtumishi wako; kwa sababu umenitia mimi mtumishi wako katika agano la Bwana pamoja nawe, lakini ikiwa mna uovu moyoni mwangu, uniue wewe mwenyewe; kwa nini kunileta kwa baba yako?
9 Naye Yonathani akasema, Haya na yawe mbali nawe, kwa maana kama ningejua ya kuwa baba yangu amekusudia kukutenda neno baya, je! Singekuambia?
10 Basi Daudi akamwambia Yonathani, Ni nani atakayeniambia, ikiwa baba yako amekujibu maneno makali?
11 Yonathani akamwambia Daudi, Twende zetu nje mashambani. Wakatoka wote wawili, wakaenda mashambani.
12 Naye Yonathani akamwambia Daudi, Bwana, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili?
13 Bwana anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na Bwana awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14 Nawe utanionyesha fadhili za Bwana, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai;
15 lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule Bwana atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.
16 Basi Yonathani akafanya agano na jamaa yake Daudi, akisema, Bwana naye atayataka mkononi mwa adui zake Daudi.
17 Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe.
18 Kisha Yonathani akamwambia, Kesho ni mwandamo wa mwezi, nawe utakosekana, kwa sababu kiti chako kitakuwa hakina mtu.
19 Nawe ukiisha kungoja siku tatu, shuka upesi ufike kuko huko ulikojificha, siku ya shughuli ile; nawe kaa karibu na kile kichuguu kule.
20 Nami nitapiga mishale mitatu kando-kando yake, kana kwamba ninapiga shabaha.
21 Kisha, angalia, nitamtuma mtoto na kumwambia, Nenda ukaitafute mishale. Hapo nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko upande wako huu, itwae; basi uje, maana iko amani kwako, wala hapana hatari, Bwana aishivyo.
22 Bali nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko huko mbele yako; basi enenda zako, kwa maana Bwana amekuamuru uende zako.
23 Na kwa habari ya neno lile tulilonena, wewe na mimi, angalia Bwana yu kati ya wewe na mimi milele.
24 Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula.
25 Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu.
26 Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata.
27 Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo?
28 Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu;
29 akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.
30 Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako.
31 Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu, maana hakika yake atakufa huyu.
32 Yonathani akamjibu Sauli, baba yake, akamwambia, Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini?
33 Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi.
34 Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha.
35 Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye.
36 Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake.
37 Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako?
38 Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake.
39 Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe.
40 Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini.
41 Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi.
42 Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la Bwana ya kwamba, Bwana atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.
1 Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwani wewe kuwa peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe?
2 Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani.
3 Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa.
4 Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake.
5 Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi?
6 Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za Bwana, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa.
7 Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za Bwana jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli.
8 Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka.
9 Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe.
10 Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi.
11 Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake.
12 Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi.
13 Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake.
14 Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu?
15 Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?
1 Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
2 Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.
3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.
4 Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.
5 Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi.
6 Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka.
7 Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa maakida wa watu elfu, na maakida wa watu mia;
8 hata ninyi nyote mkafanya fitina juu yangu, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemwondokesha mtumishi wangu juu yangu, anivizie kama hivi leo?
9 Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nalimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu.
10 Naye akamwuliza Bwana kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti.
11 Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia.
12 Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu.
13 Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo?
14 Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako?
15 Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi.
16 Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.
17 Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa Bwana, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa Bwana.
18 Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani.
19 Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo.
20 Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi.
21 Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa Bwana.
22 Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nalijua yakini ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo.
23 Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.
1 Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria.
2 Basi Daudi akamwuliza Bwana, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye Bwana akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila.
3 Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti?
4 Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye Bwana akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako.
5 Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila.
6 Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake.
7 Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo.
8 Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake.
9 Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera.
10 Ndipo Daudi akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu.
11 Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye Bwana akamjibu, Atashuka.
12 Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? Bwana akasema, Watakutia.
13 Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje.
14 Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake.
15 Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi.
16 Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu.
17 Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu.
18 Na hao wawili wakafanya agano mbele za Bwana; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.
19 Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni?
20 Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme.
21 Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na Bwana; kwa sababu mmenihurumia.
22 Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba atenda kwa hila nyingi.
23 Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafuta-tafuta katika elfu zote za Yuda.
24 Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini wa jangwa.
25 Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni.
26 Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana kwenda zake kwa hofu ya Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake wakamzunguka Daudi na watu wake ili kuwakamata.
27 Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi.
28 Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kinyume cha Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi.
29 Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.
1 Ikawa, Sauli aliporudi baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya Engedi.
2 Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.
3 Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana.
4 Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri.
5 Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli.
6 Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA,neon hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.
7 Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake.
8 Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia.
9 Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru?
10 Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.
11 Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.
12 Bwana atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako.
13 Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako.
14 Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto.
15 Basi Bwana atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako.
16 Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia.
17 Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya.
18 Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani Bwana aliponitia mikononi mwako, hukuniua.
19 Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama? Basi Bwana na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo.
20 Na sasa, angalia, najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako.
21 Basi sasa, uniapie kwa Bwana, ya kwamba hutawakatilia mbali wazao wangu baada yangu, wala hutaliharibu jina langu katika mbari ya baba yangu.
22 Naye Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akaenda zake kwao; lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.
1 Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama.
2 Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli.
3 Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.
4 Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake.
5 Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie;
6 na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao.
7 Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.
8 Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi.
9 Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza.
10 Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake!
11 Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?
12 Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote.
13 Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao.
14 Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana.
15 Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni;
16 watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.
17 Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.
18 Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.
19 Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.
20 Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.
21 Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema.
22 Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.
23 Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi.
24 Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.
25 Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.
26 Basi sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.
27 Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu.
28 Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika Bwana atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya Bwana; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote.
29 Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na Bwana, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo.
30 Tena itakuwa, hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli;
31 hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako.
32 Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;
33 na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.
34 Kwa kuwa ni kweli, aishivyo Bwana, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.
35 Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.
36 Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka.
37 Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe.
38 Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa.
39 Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe Bwana ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali Bwana amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.
40 Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe.
41 Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.
42 Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe.
43 Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wakawa wote wawili wakeze.
44 Walakini Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi, aliyekuwa mtu wa Galimu, Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi.
1 Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kuelekea Yeshimoni?
2 Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu.
3 Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani.
4 Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika.
5 Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka.
6 Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe.
7 Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka.
8 Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili.
9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi
10 Daudi akasema, Aishivyo Bwana, Bwana atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea.
11 Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi
12 Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia.
13 Kisha Daudi akaenda ng'ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao;
14 naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme?
15 Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako?
16 Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo Bwana, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi*fq* wa Bwana. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake?
17 Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme.
18 Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu?
19 Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni Bwana aliyekuondokesha juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za Bwana; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa Bwana, wakisema, Enenda, katumikie miungu mingine.
20 Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa Bwana; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani.
21 Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.
22 Daudi akajibu, akasema, Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae.
23 Naye Bwana atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake; maana Bwana amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyosha mkono wangu juu ya masihi wa BWANA.
24 Tena, angalia, kama vile maisha yako yalivyokuwa na thamani machoni pangu, kadhalika na maisha yangu na yawe na thamani machoni pa Bwana, akaniokoe katika shida zote.
25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, Ubarikiwe, Daudi, mwanangu; utatenda mambo makuu, tena hakika yako utashinda. Basi, Daudi akaenda zake; Sauli naye akarudi kwao.
1 Ndipo Daudi aliposema moyoni mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka katika mikono yake.
2 Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
3 Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.
4 Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe?
6 Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo.
7 Na hesabu ya siku alizokaa Daudi katika nchi ya Wafilisti ilikuwa mwaka mzima na miezi minne.
8 Naye Daudi na watu wake walikuwa wakikwea na kuwashambulia Wageshuri, na Wagirizi, na Waamaleki waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo, tangu Telemu, hapo uendapo Shuri, hata mpaka nchi ya Misri.
9 Tena Daudi akaipiga nchi hiyo, asimhifadhi hai mume wala mke, akateka nyara kondoo, na ng'ombe, na punda, na ngamia na mavazi; kisha akarejea na kufika kwa Akishi.
10 Naye Akishi humwuliza, Je! Mmeshambulia upande gani leo? Na Daudi husema, Juu ya Negebu ya Yuda, au, juu ya Negebu ya Wayerameeli, au, juu ya Negebu ya Wakeni.
11 Tena Daudi hakumhifadhi hai mume wala mke, ili kuwaleta Gathi maana alisema, Wasituchongee kusema, Ndivyo alivyofanya Daudi, tena ndivyo ilivyokuwa desturi yake wakati wote alipokaa katika nchi ya Wafilisti.
12 Hivyo Akishi akamsadiki Daudi, akasema, Amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu hata milele.
1 Ikawa siku zile hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao waende vitani, ili kupigana na Israeli. Naye Akishi akamwambia Daudi, Jua hakika ya kuwa wewe utatoka pamoja nami jeshini, wewe na watu wako.
2 Naye Daudi akamwambia Akishi, Vema, sasa utajua atakayoyatenda mtumishi wako. Naye Akishi akamwambia Daudi, Haya basi! Mimi nitakufanya wewe kuwa mlinda kichwa changu daima.
3 Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Israeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi.
4 Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa.
5 Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana.
6 Lakini Sauli alipouliza kwa Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii.
7 Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.
8 Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.
9 Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?
10 Naye Sauli akamwapia kwa Bwana, akasema, Aishivyo Bwana, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili.
11 Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli.
12 Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.
13 Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi.
14 Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia.
15 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje.
16 Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa Bwana amekuacha, naye amekuwa adui yako?
17 Yeye Bwana amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; Bwana amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.
18 Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya Bwana, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii Bwana amekutendea hili leo.
19 Tena pamoja na wewe Bwana atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena Bwana atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti.
20 Mara Sauli akaanguka chini kifulifuli, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yo yote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.
21 Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli, akamwona ya kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimeutia uhai wangu mkononi mwangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia.
22 Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie ngaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako.
23 Lakini yeye alikataa, akasema, Mimi sitaki kula. Ila watumishi wake, pamoja na yule mwanamke, wakamlazimisha; naye akaisikiliza sauti yao. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.
24 Naye yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona nyumbani; akafanya haraka kumchinja; akatwaa na unga, akaukanda, akafanya mkate wa mofa kwa unga huo;
25 kisha akamwandalia Sauli na watumishi wake; wakala. Ndipo wakaondoka, wakaenda zao usiku ule.
1 Basi hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki; nao Waisraeli wakafanya kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.
2 Nao mashehe wa Wafilisti wakapita mbele, mia kwa mia, na elfu kwa elfu; naye Daudi na watu wake wakapita wa mwisho pamoja na Akishi.
3 Ndipo wakuu wa Wafilisti wakasema, Waebrania hawa wafanyani hapa? Naye Akishi akawaambia wakuu wa Wafilisti, Je! Siye huyu Daudi, yule mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amefuatana na mimi siku hizi, naam, miaka hii, wala mimi nisione hatia kwake, tangu hapo aliponiangukia mimi hata leo?
4 Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia; nao wakuu wa Wafilisti wakamwambia, Mrudishe huyu, apate kurejea mahali pake ulipomwagiza, wala asiende pamoja nasi vitani, asije akawa adui wetu vitani; kwani mtu huyu angejipatanisha na bwana wake kwa njia gani? Je! Si kwa vichwa vya watu hawa?
5 Je! Siye huyo Daudi, ambaye waliimbiana habari zake katika michezo, wakisema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake?
6 Ndipo Akishi akamwita Daudi, akamwambia, Aishivyo Bwana, wewe umekuwa mwenye adili, tena kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema machoni pangu; kwa sababu mimi sikuona uovu ndani yako tangu siku ile uliponijia hata leo; walakini hao wakuu hawakuridhii.
7 Basi sasa urudi, uende zako kwa amani, ili usiwachukize hao mashehe wa Wafilisti.
8 Naye Daudi akamwambia Akishi, Lakini mimi nimefanyaje? Nawe umeona nini kwangu mimi mtumwa wako, muda wote niliokaa mbele yako hata leo, nisipate ruhusa niende na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?
9 Akishi akajibu, akamwambia Daudi, Mimi najua ya kuwa u mwema machoni pangu, kama malaika wa Mungu; ila hao wakuu wa Wafilisti wamesema, Huyu hatakwea pamoja nasi kwenda vitani.
10 Kwa hiyo sasa amka asubuhi na mapema, wewe na watumwa wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; nanyi mtakapoamka asubuhi na mapema, na kupata mwanga, nendeni zenu.
11 Basi Daudi akaamka asubuhi na mapema, yeye na watu wake, kwenda zao asubuhi, kuirudia nchi ya Wafilisti. Nao Wafilisti wakakwea kwenda Yezreeli.
1 Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto;
2 nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao.
3 Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena.
5 Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.
6 Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika Bwana, Mungu wake.
7 Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.
8 Daudi akauliza kwa Bwana, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.
9 Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye, nao wakakifikilia kijito Besori, ambapo wale walioachwa nyuma walikaa.
10 Lakini Daudi akakaza kufuata, yeye na watu mia nne; kwa maana watu mia mbili walikaa nyuma, ambao walitaka kuzimia hata hawakuweza kukivuka hicho kijito Besori.
11 Nao wakamkuta Mmisri mavueni, wakamleta kwa Daudi, na kumpa chakula, naye akala; nao wakampa maji ya kunywa;
12 kisha wakampa kipande cha mkate wa tini, na vishada viwili vya zabibu; naye akiisha kula roho yake ikamrudia; kwa maana alikuwa hakula chakula wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.
13 Ndipo Daudi akamwuliza, Wewe u mtu wa nani; nawe umetoka wapi? Naye akasema, Mimi ni kijana wa Misri, mtumwa wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu tangu siku hizi tatu nalishikwa na ugonjwa.
14 Sisi tulishambulia Negebu ya Wakerethi, na ya milki ya Yuda, na Negebu ya Kalebu; na huo mji wa Siklagi tukauchoma moto.
15 Daudi akamwambia, Je! Wewe utaniongoza chini hata nilifikilie jeshi hilo? Naye akasema, Uniapie kwa Mungu, ya kwamba hutaniua, wala kunitia mikononi mwa huyo bwana wangu, nami nitakuongoza chini hata kulifikilia jeshi hilo.
16 Na hapo alipokuwa amewaongoza chini, tazama, hao walikuwa wametawanyika juu ya nchi yote, wakila na kunywa, na kufanya karamu, kwa sababu ya hizo nyara kubwa walizochukua katika nchi ya Wafilisti, na katika nchi ya Yuda.
17 Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hata jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia.
18 Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili.
19 Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala cho chote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote.
20 Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng'ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.
21 Kisha Daudi aliwafikilia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.
22 Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu cho chote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.
23 Ndipo Daudi akasema, La, ndugu zangu, msitende hivyo katika hizo nyara alizotupa Bwana, ambaye ndiye aliyetuhifadhi, akalitia mikononi mwetu lile jeshi lililokuja kinyume chetu.
24 Tena ni nani atakayewasikiliza ninyi katika jambo hili? Kwa kuwa kama lilivyo fungu lake yeye ashukaye vitani, ndivyo litakavyokuwa na fungu lake huyo akaaye karibu na vyombo; watagawiwa sawasawa.
25 Basi ikawa hivyo tangu siku ile na baadaye; akaiweka iwe amri na agizo la Israeli hata leo.
26 Basi Daudi alipofika Siklagi, aliwapelekea wazee wa Yuda, rafiki zake, sehemu ya nyara, akasema, Angalieni, zawadi yenu katika nyara za adui za Bwana;
27 yaani, kwa hao wa Betheli, na kwa hao wa Ramoth-Negebu, na kwa hao wa Yatiri;
28 na kwa hao wa Aroeri, na kwa hao wa Sifmothi, na kwa hao wa Eshtemoa;
29 na kwa hao wa Rakali, na kwa hao wa miji ya Wayerameeli, na kwa hao wa miji ya Wakeni;
30 na kwa hao wa Horma, na kwa hao wa Korashani, na kwa hao wa Athaki;
31 na kwa hao wa Hebroni, na kwa hao wa kila mahali alipozoelea Daudi mwenyewe na watu wake.
1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima wa Gilboa.
2 Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.
3 Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.
4 Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.
5 Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa pamoja naye.
6 Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu, na mchukua silaha zake, na watu wake wote pamoja siku iyo hiyo.
7 Kisha watu wa Israeli waliokuwa upande wa pili wa bonde lile, na ng'ambo ya Yordani, walipoona ya kuwa watu wa Israeli wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo.
8 Hata ikawa, siku ya pili yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara waliouawa, walimwona Sauli na wanawe watatu wameanguka juu ya mlima wa Gilboa.
9 Wakamkata kichwa, wakamvua silaha zake, wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari nyumbani mwa sanamu zao, na kwa watu.
10 Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa Maashtorethi; wakakitundika kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-shani.
11 Na wenyeji wa Yabesh-Gileadi waliposikia habari zake, jinsi hao Wafilisti walivyomtenda Sauli,
12 wakainuka mashujaa wote, wakaenda usiku kucha, wakautwaa mwili wake Sauli, na miili ya wanawe, na kuiondoa ukutani kwa Beth-shani nao wakaja Yabeshi, na kuiteketeza huko.
13 Kisha wakaitwaa mifupa yao, na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.