Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22
1 Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto.
2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto.
3 Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.
4 Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.
5 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake.
6 Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.
7 Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata.
8 Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia.
9 Adonia akachinja kondoo, na ng'ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme;
10 ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao.
11 Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari?
12 Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani.
13 Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia?
14 Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako.
15 Basi Bath-sheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme.
16 Bath-sheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini?
17 Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa Bwana, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi.
18 Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari.
19 Tena amechinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita.
20 Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu.
21 Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu.
22 Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia.
23 Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi.
24 Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi?
25 Maana leo ameshuka, na kuchinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia!
26 Walakini mimi, mimi mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi.
27 Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?
28 Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bath-sheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme.
29 Naye mfalme akaapa, akasema, Bwana aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote,
30 hakika yake nitafanya leo kama vile nilivyokuapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu.
31 Ndipo Bath-sheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele.
32 Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme.
33 Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamtelemshe mpaka Gihoni;
34 kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi!
35 Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda.
36 Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; Bwana, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo.
37 Kama vile Bwana alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.
38 Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni.
39 Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi!
40 Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao.
41 Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki?
42 Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema.
43 Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani.
44 Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme.
45 Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia.
46 Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme.
47 Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake.
48 Na tena, mfalme akasema hivi, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo.
49 Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake.
50 Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu.
51 Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga.
52 Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.
53 Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.
1 Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema,
2 Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;
3 uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;
4 ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.
5 Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake.
6 Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani.
7 Lakini uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako; kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako.
8 Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu, ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa Bwana, nikamwambia, Mimi sitakuua kwa upanga.
9 Basi kwa hiyo usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu.
10 Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi.
11 Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.
12 Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.
13 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani?
14 Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema.
15 Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa Bwana.
16 Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema.
17 Akasema, Nena, nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami.
18 Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako.
19 Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kuume.
20 Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikataze. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukataza neno.
21 Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami.
22 Akajibu mfalme Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya.
23 Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa Bwana, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe.
24 Basi kwa hiyo, Bwana aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia.
25 Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.
26 Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu.
27 Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa Bwana; ili alitimize neno la Bwana, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo.
28 Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa Bwana, akazishika pembe za madhabahu.
29 Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa Bwana, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige.
30 Basi Benaya akaja Hemani kwa Bwana, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu.
31 Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure.
32 Naye Bwana atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda.
33 Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa Bwana.
34 Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani.
35 Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari.
36 Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote.
37 Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.
38 Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi.
39 Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi.
40 Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi.
41 Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena.
42 Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa Bwana, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema?
43 Mbona basi hukukishika kiapo cha Bwana, na amri niliyokuagiza?
44 Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo Bwana atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe.
45 Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za Bwana hata milele.
46 Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.
1 Huyo Sulemani akafanya ujamaa na Farao, mfalme wa Misri, akamwoa binti yake Farao, akamleta mjini mwa Daudi, hata alipokwisha kuijenga nyumba yake, na nyumba ya Bwana, na ukuta wa kuuzunguka Yerusalemu.
2 Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika mahali pa juu, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la Bwana, hata siku zile.
3 Sulemani naye akampenda Bwana, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
4 Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu ya madhabahu ile.
5 Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.
6 Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo.
7 Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.
8 Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi.
9 Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?
10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.
11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;
12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.
13 Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.
14 Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi.
15 Naye Sulemani akaamka, na kumbe! Ni ndoto. Akaenda Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Bwana, akatoa sadaka za kuteketezwa, akatoa na sadaka za amani; akawafanyia karamu watumishi wake wote.
16 Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.
17 Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.
18 Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.
19 Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia.
20 Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.
21 Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa.
22 Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.
23 Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.
24 Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.
25 Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.
26 Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.
27 Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.
28 Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.
1 Basi mfalme Sulemani akawa mfalme juu ya Israeli wote.
2 Na hawa ndio wakuu aliokuwa nao; Azaria mwana wa Sadoki, kuhani,
3 Elihorefu na Ahiya, wana wa Shausha, waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe;
4 na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya jeshi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
5 na Azaria mwana wa Nathani alikuwa juu ya maakida; na Zabudi mwana wa Nathani alikuwa kuhani, rafiki wake mfalme.
6 Na Ahishari alikuwa juu ya nyumba; na Adoramu mwana wa Abda alikuwa juu ya shokoa.
7 Sulemani alikuwa na maakida kumi na wawili juu ya Israeli wote, walioleta chakula cha mfalme na nyumba yake; kila mtu alikuwa na mwezi mmoja katika mwaka kuleta chakula.
8 Na haya ndiyo majina yao. Mwana wa Huri, mlimani mwa Efraimu.
9 Mwana wa Dekari, kutoka Makasi, na Shaalbimu na Bethshemeshi na Elon-beth-hanani.
10 Mwana wa Hesedi, katika Arubothi; na Soko ilikuwa kwake na nchi yote ya Heferi.
11 Mwana wa Abinadabu katika Nafath-dori yote; ndiye aliyekuwa naye Tafathi binti Sulemani kuwa mke wake.
12 Baana mwana wa Ahiludi, katika Taanaki na Megido, na Beth-sheani yote, iliyo kando ya Sarethani, chini ya Yezreeli, tangu Beth-sheani mpaka Abel-mehola, hata kupita Yokmeamu.
13 Mwana wa Geberi katika Ramoth-gileadi; na kwake ilikuwa miji ya Yairi mwana wa Manase iliyomo Gileadi; na kwake ilikuwa wilaya ya Argobu, iliyomo Bashani, miji mikubwa sitini yenye kuta na makomeo ya shaba.
14 Ahinadabu mwana wa Ido, katika Mahanaimu.
15 Ahimaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani.
16 Baana mwana wa Hushai, katika Asheri na Bealothi.
17 Yehoshafati mwana wa Parua, katika Isakari.
18 Shimei mwana wa Ela, katika Benyamini.
19 Geberi mwana wa Uri, katika nchi ya Gileadi, nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani; naye alikuwa akida wa pekee katika nchi hiyo.
20 Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi.
21 Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake.
22 Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori therathini za unga wa mzuri, na kori sitini za ngano.
23 na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona.
24 Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote.
25 Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani.
26 Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi arobaini elfu kwa magari yake, na wapandao farasi kumi na mbili elfu.
27 Na maakida wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu.
28 Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake.
29 Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.
30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.
31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.
32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.
33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.
34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.
1 Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote.
2 Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema,
3 Umemjua Daudi baba yangu jinsi asivyoweza kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata Bwana alipowatia watu chini ya nyayo zake.
4 Ila leo Bwana, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya.
5 Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, kama Bwana alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
6 Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni.
7 Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe Bwana leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi.
8 Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi.
9 Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu.
10 Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka.
11 Sulemani akampa Hiramu kori ishirini elfu za ngano, chakula cha watu wake, na kori ishirini za mafuta safi. Ndizo Sulemani alizompa Hiramu mwaka kwa mwaka.
12 Bwana akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidia. Ikawa amani kati yao Hiramu na Sulemani; wakafanyana maagano pamoja hao wawili.
13 Mfalme Sulemani akafanya shokoa ya Israeli wote; nayo shokoa hiyo ilikuwa ya watu thelathini elfu.
14 Akawatuma Lebanoni kwa mwezi, elfu kumi kwa zamu. Mwezi mmoja walikuwako huko Lebanoni, na miezi miwili wakawako kwao. Na Adoramu alikuwa juu ya shokoa.
15 Sulemani alikuwa na wachukua mizigo sabini elfu, na wakatao miti themanini elfu milimani;
16 mbali na maakida yake Sulemani waliokuwa juu ya kazi, elfu tatu na mia tatu, wasimamizi wa watu waliotenda kazi.
17 Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa.
18 Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba.
1 Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya Bwana.
2 Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea Bwana, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini.
3 Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba.
4 Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia.
5 Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kote kote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote.
6 Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba.
7 Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.
8 Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kuume wa nyumba; mtu hupanda madaraja ya kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu.
9 Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi.
10 Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi.
11 Neno la Bwana likamjia Sulemani, kusema,
12 Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako.
13 Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli.
14 Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza.
15 Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi.
16 Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu.
17 Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arobaini.
18 Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana.
19 Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la Bwana.
20 Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi.
21 Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu.
22 Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu.
23 Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi.
24 Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili.
25 Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja.
26 Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo.
27 Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba.
28 Akayafunika makerubi kwa dhahabu.
29 Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje.
30 Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje.
31 Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano.
32 Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende.
33 Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne;
34 na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana.
35 Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro.
36 Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi.
37 Katika mwaka wa nne nyumba ya Bwana ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu.
38 Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.
1 Naye Sulemani alikuwa katika kuijenga nyumba yake mwenyewe miaka kumi na mitatu, akaimaliza nyumba yake yote.
2 Kwa kuwa aliijenga nyumba ya mwitu wa Lebanoni; mikono mia urefu wake, na mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake, juu ya safu nne za nguzo za mwerezi, na mihimili ya mwerezi juu ya nguzo.
3 Ikafunikwa juu kwa mwerezi juu ya mihimili arobaini na mitano, iliyokuwa juu ya nguzo; kumi na mitano kwa safu.
4 Na madirisha yalikuwako safu tatu, mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.
5 Na milango yote na miimo ilikuwa ya mraba, ilivyoangaziwa; na mwangaza kuelekea mwangaza katika madaraja matatu.
6 Akaifanya baraza ya nguzo; mikono hamsini urefu wake, na mikono thelathini upana wake; na ukumbi mbele yake; na nguzo na mihimili minene mbele yake.
7 Akaifanya baraza ya kiti cha enzi, ili ahukumu ndani yake, ndiyo baraza ya hukumu; nayo ikafunikwa mwerezi tangu sakafu mpaka dari.
8 Nayo nyumba yake atakayokalia, katika behewa nyingine iliyokuwa ndani kupita baraza, ilikuwa ya kazi kama hiyo. Tena akamjengea nyumba binti Farao, (ambaye Sulemani alikuwa amemwoa), mfano wa ile baraza.
9 Hizi zote zilikuwa za mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, yaliyokatwa kwa misumeno, ndani na nje, tangu msingi hata mawe ya juu, na nje vile vile hata behewa kuu.
10 Nao msingi ulikuwa wa mawe ya thamani, mawe makubwa, mawe mikono kumi, na mawe ya mikono minane.
11 Na juu kulikuwa na mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, na mierezi.
12 Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya Bwana, na ukumbi wa nyumba.
13 Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Huramu kutoka Tiro.
14 Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila ya Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, mstadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikilia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote.
15 Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii.
16 Akafanya taji mbili za shaba iliyoyeyushwa za kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji ya pili.
17 Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili
18 Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili.
19 Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne.
20 Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili.
21 Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto ,akaiita jina lake Boazi.
22 Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.
23 Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.
24 Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa.
25 Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.
26 Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili.
27 Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.
28 Na kazi ya matako ndiyo hii; yalikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio;
29 na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng'ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na tako; na chini ya simba na ng'ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza.
30 Kila tako lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni.
31 Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya tako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana.
32 Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya tako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu.
33 Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu.
34 Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za tako moja; mataruma hayo ni kitu kimoja na tako lenyewe.
35 Na juu ya tako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya tako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo.
36 Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote.
37 Hivyo akayafanya yale matako kumi; yote yalikuwa ya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja.
38 Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arobaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya tako moja, katika yale matako kumi.
39 Akayaweka yale matako, matano upande wa kuume wa nyumba, na matano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kuume wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini.
40 Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya Bwana;
41 zile nguzo mbili, na vimbe mbili za taji zilikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;
42 na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;
43 na yale matako kumi, na birika kumi juu ya matako;
44 na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari;
45 na masufuria, na majembe, na mabakuli; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya Bwana, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa.
46 Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani.
47 Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana.
48 Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa Bwana; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu;
49 na vinara vya taa, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu;
50 na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu.
51 Hivyo ikamalizika kazi yote Sulemani mfalme aliyoifanya katika nyumba ya Bwana. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya Bwana.
1 Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.
2 Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
3 Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku.
4 Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha.
5 Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi.
6 Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi.
7 Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.
8 Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.
9 Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri.
10 Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu;
11 hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana.
12 Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.
13 Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.
14 Mfalme akageuza uso wake, akawabariki mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
15 Akasema, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena na Daudi baba yangu kwa kinywa chake akalitimiza kwa mkono wake, akasema,
16 Tokea siku ile nilipowatoa watu wangu Israeli katika Misri, sikuchagua mji wo wote katika kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe hapo; lakini nalimchagua Daudi awe juu ya watu wangu Israeli.
17 Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
18 Lakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.
19 Lakini wewe hutanijengea nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
20 Basi Bwana amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama Bwana alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
21 Na humo sanduku hili nimelifanyizia mahali, ambalo ndani yake mna maagano ya Bwana, aliyoyafanya na baba zetu, hapo alipowatoa katika nchi ya Misri.
22 Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni.
23 Akasema Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.
24 Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
25 Na sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.
26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.
27 Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!
28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.
29 Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa.
30 Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.
31 Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii;
32 basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
33 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii;
34 basi, usikie huko mbinguni, ukawaachilie watu wako Israeli dhambi yao, ukawarejeze tena katika nchi uliyowapa baba zao.
35 Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa;
36 basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao.
37 Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao; au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
38 maombi yo yote au dua yo yote ikifanywa na mtu awaye yote, au na watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu maradhi ya moyo wake, na kuikunjua mikono yake kuielekea nyumba hii;
39 basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote);
40 ili wakuche wewe siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
41 Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako;
42 (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii;
43 basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako.
44 Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yo yote utakayowapeleka, wakikuomba, Bwana, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
45 basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao.
46 Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu;
47 basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu;
48 watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
49 basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao;
50 ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia.
51 Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuu ya chuma.
52 Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia.
53 Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.
54 Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba Bwana maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya Bwana, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni.
55 Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema,
56 Na ahimidiwe Bwana, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake.
57 Bwana, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe;
58 aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu.
59 Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za Bwana, na yawe karibu na Bwana, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku.
60 Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine.
61 Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.
62 Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za Bwana.
63 Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea Bwana, ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Bwana.
64 Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Bwana ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani.
65 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za Bwana, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne.
66 Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.
1 Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya,
2 basi, Bwana akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni.
3 Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote;
4 na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu,
5 ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.
6 Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
7 basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote.
8 Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?
9 Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao.
10 Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya Bwana na nyumba yake mfalme,
11 (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya.
12 Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala haikumpendeza.
13 Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo.
14 Hiramu akamletea mfalme talanta sitini za dhahabu.
15 Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hazori, na Megido, na Gezeri.
16 Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani.
17 Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini,
18 na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi;
19 na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.
20 Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli;
21 watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.
22 Lakini wa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu shokoa; ila ndio watu wa vita, na wangoje wake, na wakuu wake, na akida zake, na wakuu, wa magari yake, na wa wapanda farasi wake.
23 Hao maakida wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowaamuru watu watendao kazi.
24 Lakini binti Farao akapanda toka mji wa Daudi, mpaka hiyo nyumba yake Sulemani, aliyomjengea; kisha, aliijenga Milo.
25 Na mara tatu kila mwaka Sulemani alikuwa akitoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu aliyomjengea Bwana akafukiza uvumba pamoja nazo juu ya madhabahu iliyokuwako mbele za Bwana. Hivyo akaimaliza nyumba.
26 Tena, mfalme Sulemani akaunda merikebu huko Ezion-geberi, ulioko karibu na Elothi, pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu.
27 Naye Hiramu akatuma merikebuni watumishi wake, wanamaji wenye kuijua bahari, pamoja na watumishi wake Sulemani.
28 Wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu, talanta mia nne na ishirini, wakamletea mfalme Sulemani.
1 Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.
2 Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni.
3 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie.
4 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga,
5 na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia.
6 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
7 Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.
8 Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.
9 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.
10 Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.
11 Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani.
12 Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya Bwana, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo.
13 Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
14 Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita,
15 zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya maliwali wa nchi.
16 Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu.
17 Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.
18 Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.
19 Kiti kile kilikuwa na daraja sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
20 Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita huko na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wo wote.
21 Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.
22 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.
23 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.
24 Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.
25 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.
26 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
27 Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
28 Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake.
29 Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia hamsini; vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.
1 Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti,
2 na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.
3 Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.
4 Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.
5 Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.
6 Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.
7 Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni.
8 Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.
9 Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili,
10 akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru Bwana.
11 Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.
12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.
13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.
14 Ndipo Bwana akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu.
15 Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu,
16 (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hata alipompoteza kila mwanamume wa Edomu);
17 yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi akali ni mtoto mdogo.
18 Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akamwamria vyakula, akampa mashamba.
19 Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza umbu la mkewe, umbu la Tapenesi aliyekuwa malkia.
20 Naye huyo umbu la Tapenesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapenesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao.
21 Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu.
22 Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu.
23 Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,
24 naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.
25 Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
26 Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme.
27 Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwinulia mfalme mkono. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi.
28 Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu.
29 Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani.
30 Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili.
31 Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi,
32 (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli);
33 kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake.
34 Walakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; lakini nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu,
35 lakini nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe kabila kumi.
36 Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko.
37 Nami nitakutwaa wewe, nawe utatawala kama roho yako inavyotamani, nawe utakuwa mfalme juu ya Israeli.
38 Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli.
39 Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima.
40 Basi Sulemani akataka kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akaondoka, akakimbilia Misri, kwa Shishaki, mfalme wa Misri, akakaa katika Misri hata wakati wa kufa kwake Sulemani.
41 Nayo yaliyosalia ya Sulemani, mambo yake na yote aliyoyafanya, na hekima yake, je! Hayo siyo yaliyoandikwa kitabuni mwa mambo yake Sulemani?
42 Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arobaini.
43 Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.
1 Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme.
2 Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri,
3 wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,
4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.
5 Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao.
6 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa?
7 Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima.
8 Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake.
9 Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako?
10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge.
12 Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.
13 Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa;
14 akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge.
15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni.
16 Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hakuwasikia, hao watu walimjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya! Nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Ee Daudi. Hivyo Israeli wakaenda zao hemani kwao.
17 Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu aliwatawala wao.
18 Ndipo mfalme Rehoboamu akampeleka Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, nao Israeli wote wakampiga kwa mawe hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda katika gari, ili akimbilie Yerusalemu.
19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.
20 Ikawa, Israeli wote waliposikia ya kwamba Yeroboamu amerudi, wakapeleka watu wakamwita aje mkutanoni, wakamfanya mfalme juu ya Israeli wote; wala hapakuwa na mtu aliyeshikamana na nyumba ya Daudi, ila kabila ya Yuda peke yake.
21 Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda, pamoja na kabila ya Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu, waliokuwa watu wa vita, ili wapigane na nyumba ya Israeli, waurudishe ufalme tena kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
22 Lakini likaja neno la Mungu kwa Shemaya mtu wa Mungu, kusema,
23 Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na jamaa yote ya Yuda na Benyamini, na watu waliosalia, ukisema,
24 Bwana asema hivi, Msiende, wala msipigane na ndugu zenu wana wa Israeli; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakalisikiliza neno la Bwana, wakarudi, wakaenda zao, sawasawa na neno la Bwana.
25 Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli.
26 Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi.
27 Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda.
28 Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng'ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri.
29 Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani.
30 Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani.
31 Tena akafanya nyumba za mahali pa juu, akafanya na watu wo wote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani.
32 Yeroboamu akaamuru kushika sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo katika Betheli akiwatolea dhabihu wale ng'ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya.
33 Akatoa dhabihu juu ya ile madhabahu aliyoifanya katika Betheli, siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouwaza moyoni mwake mwenyewe; akawaamuru wana wa Israeli waishike sikukuu hiyo, akapanda kuiendea madhabahu, ili kufukiza uvumba.
1 Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.
2 Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.
3 Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.
4 Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.
5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.
6 Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.
7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.
8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.
11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.
12 Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.
13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.
14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.
15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.
20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;
21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,
22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.
23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.
24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.
25 Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.
26 Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya Bwana; kwa hiyo Bwana amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia.
27 Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.
28 Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.
29 Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.
30 Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu!
31 Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
32 Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la Bwana, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.
33 Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wo wote.
34 Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.
1 Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu.
2 Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.
3 Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje.
4 Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake.
5 Bwana akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine.
6 Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito.
7 Nenda, umwambie Yeroboamu, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli,
8 nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu;
9 lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako;
10 tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia.
11 Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa Bwana amelinena hilo.
12 Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa.
13 Na Israeli wote watamlilia, na kumzika, kwa maana ndiye peke yake wa Yeroboamu atakayeingia kaburini; kwa sababu limeonekana ndani yake jambo lililo jema kwa Bwana, Mungu wa Israeli, nyumbani mwa Yeroboamu.
14 Tena Bwana atajiinulia mfalme wa Israeli atakayeiharibu nyumba ya Yeroboamu siku ile; na nini tena hata sasa?
15 Kwa kuwa Bwana atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang'oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng'ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha Bwana.
16 Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli.
17 Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa.
18 Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la Bwana, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii.
19 Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
20 Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake.
21 Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni.
22 Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa Bwana; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao.
23 Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
24 Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.
25 Ikawa, mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu;
26 akazichukua hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao zote za dhahabu alizozifanya Sulemani.
27 Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.
28 Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa Bwana, hao walinzi walizichukua; wakazirudisha tena katika chumba cha walinzi.
29 Na mambo yake Rehoboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
30 Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote.
31 Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni. Na mwanawe, Abiya, alitawala mahali pake.
1 Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda.
2 Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.
3 Akaziendea dhambi zote za babaye, alizozifanya kabla yake; wala moyo wake haukuwa mkamilifu na Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye.
4 Walakini kwa ajili ya Daudi, Bwana, Mungu wake, akampa taa humo Yerusalemu, amwinue mwanawe baada yake, na kuufanya imara Yerusalemu;
5 kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti.
6 Basi kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote za maisha yake.
7 Na mambo yote ya Abiya yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.
8 Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi. Akatawala Asa mwanawe mahali pake.
9 Mwaka wa ishirini wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala juu ya Yuda.
10 Akatawala miaka arobaini na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.
11 Basi, Asa akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu, kama alivyofanya babaye Daudi.
12 Akawafukuza mahanithi katika nchi, akaziondoa sanamu zote walizozifanya baba zake.
13 Hata na Maaka, mamaye, akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.
14 Lakini mahali pa juu hapakuondoshwa; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu kwa Bwana siku zake zote.
15 Akavileta vile vitu alivyovitakasa baba yake, na vile alivyovitakasa yeye mwenyewe, katika nyumba ya Bwana, fedha; na dhahabu, na vyombo.
16 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.
17 Kisha, Baasha mfalme wa Israeli akaondoka juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.
18 Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,
19 Tumepatana mimi nawe, na baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea zawadi, fedha na dhahabu; basi nenda, uyavunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.
20 Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma wakuu wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli, akapiga Iyoni, na Dani, na Abel-beth-maaka na Kinerothi yote, na nchi yote ya Naftali.
21 Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo akaacha kuujenga Rama, akaenda akakaa Tirza.
22 Ndipo mfalme Asa akatangaza kwa Yuda pia; asiachiliwe mtu; nao wakayachukua mawe ya Rama na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye mfalme Asa akajenga kwa vitu hivyo Geba wa Benyamini na Mispa.
23 Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu.
24 Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.
25 Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.
26 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.
27 Basi Baasha wa Ahiya, wa mbari ya Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.
28 Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.
29 Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi ye yote, hata alipomharibu sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;
30 kwa sababu ya makosa yake Yeroboamu aliyoyakosa, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; kwa sababu ya chukizo lake alilomchukiza Bwana, Mungu wa Israeli, hata kumghadhibisha.
31 Basi mambo yote ya Nadabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
32 Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.
33 Katika mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya alianza kutawala juu ya Israeli wote huko Tirza, akatawala miaka ishirini na minne.
34 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana akaiendea njia ya Yeroboamu, na kosa lake ambalo kwa hilo aliwakosesha Israeli.
1 Ndipo neno la Bwana likamjia Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, kusema,
2 Kwa kuwa mimi nilikuinua kutoka katika mavumbi, na kukufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nawe umeiendea njia ya Yeroboamu, na kuwakosesha watu wangu Israeli, hata wanighadhibishe kwa makosa yao;
3 angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati.
4 Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla.
5 Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
6 Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake.
7 Tena neno la Bwana likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa Bwana, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu.
8 Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili.
9 Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamfanyia fitina; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza;
10 Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake.
11 Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake.
12 Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la Bwana, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii,
13 kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
14 Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
15 Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti.
16 Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni.
17 Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza.
18 Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa;
19 kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa Bwana, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli.
20 Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
21 Ndipo watu wa Israeli wakatengwa sehemu mbili; nusu ya watu wakamfuata Tibni mwana wa Ginathi, ili wamfanye mfalme; nusu wakamfuata Omri.
22 Lakini hao watu waliomfuata Omri wakawashinda watu waliomfuata Tibni mwana wa Ginathi; basi akafa Tibni, akatawala Omri.
23 Katika mwaka wa thelathini na moja wa Asa, mfalme wa Yuda, Omri alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi na miwili. Akatawala huko Tirza miaka sita.
24 Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kuliandama jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima.
25 Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia;
26 kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
27 Nayo mambo yote ya Omri yaliyosalia aliyoyatenda, na uthabiti alioufanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
28 Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake.
29 Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili.
30 Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana kuliko wote waliomtangulia.
31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia.
32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria.
33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.
34 Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.
1 Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.
2 Neno la Bwana likamjia, kusema,
3 Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.
4 Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.
5 Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani.
6 Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.
7 Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.
8 Neno la Bwana likamjia, kusema,
9 Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.
10 Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.
11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.
12 Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.
13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.
14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.
15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.
16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.
17 Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena.
18 Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu?
19 Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake.
20 Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe.
21 Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena.
22 Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.
23 Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai.
24 Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.
1 Ikawa baada ya siku nyingi, neno la Bwana likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi.
2 Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria.
3 Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha Bwana sana;
4 kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji).
5 Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote.
6 Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake.
7 Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?
8 Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.
9 Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?
10 Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona.
11 Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.
12 Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya Bwana atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha Bwana tangu ujana wangu.
13 Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana? Jinsi nilivyowaficha manabii wa Bwana, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?
14 Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua.
15 Eliya akasema, Kama Bwana wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo.
16 Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya.
17 Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli?
18 Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za Bwana; nawe umewafuata mabaali.
19 Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli.
20 Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli.
21 Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.
22 Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini.
23 Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini.
24 Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.
25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini.
26 Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya.
27 Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.
28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.
29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika.
31 Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli.
32 Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.
33 Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.
34 Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu.
35 Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji.
36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.
40 Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.
41 Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.
42 Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.
43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.
44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.
45 Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.
46 Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.
1 Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
2 Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.
3 Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko.
4 Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.
5 Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule.
6 Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena.
7 Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.
8 Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.
9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya?
10 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.
11 Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;
12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.
13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?
14 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe.
15 Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu.
16 Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.
17 Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.
18 Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.
19 Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake.
20 Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea?
21 Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.
1 Basi, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita.
2 Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi.
3 Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu.
4 Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo.
5 Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi;
6 lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao,na kukichukua.
7 Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.
8 Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali.
9 Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo.
10 Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.
11 Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.
12 Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.
13 Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi Bwana.
14 Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, Bwana asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.
15 Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16 Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.
17 Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.
18 Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.
19 Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.
20 Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.
21 Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.
22 Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
23 Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.
24 Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.
25 Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.
26 Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.
27 Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.
28 Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, Bwana ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi Bwana.
29 Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.
30 Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.
31 Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, tuvae magunia viunoni, na kamba vichwani, tumtokee mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.
32 Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.
33 Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.
34 Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang'anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.
35 Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la Bwana, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.
36 Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya Bwana, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.
37 Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.
38 Basi yule nabii akaenda akamngoja mfalme njiani, amejibadilisha kwa kilemba juu ya macho yake.
39 Ikawa mfalme alipopita, alimwita mfalme; akasema, Mtumwa wako aliingia katikati ya pigano; na tazama, mtu mmoja akanigeukia akaniletea mtu, akaniambia, Umlinde mtu huyu; akipotea kwa njia yo yote, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, au utatoa talanta ya fedha.
40 Ikawa mtumishi wako alipokuwa akitenda haya na haya, yule akaenda zake. Mfalme wa Israeli akamwambia, Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.
41 Akafanya haraka akakiondoa kilemba machoni mwake, mfalme wa Israeli akamtambua kuwa ni mmoja wao manabii.
42 Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa sababu umemwachilia atoke mkononi mwako mtu niliyemweka ili aangamizwe kabisa, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, na watu wako mahali pa watu wake.
43 Mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake na moyo mzito, mwenye hasira, akaja Samaria.
1 Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria.
2 Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake.
3 Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu.
4 Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.
5 Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula?
6 Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu.
7 Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.
8 Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi.
9 Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu,
10 mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.
11 Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea.
12 Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu.
13 Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.
14 Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.
15 Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa.
16 Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.
17 Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema,
18 Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki.
19 Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.
20 Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
21 Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli.
22 Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli.
23 Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.
24 Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla.
25 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea.
26 Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)
27 Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.
28 Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,
29 Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.
1 Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli.
2 Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli.
3 Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu?
4 Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako.
5 Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.
6 Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
7 Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye?
8 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.
9 Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla.
10 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao.
11 Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike.
12 Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
13 Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema.
14 Mikaya akasema, Kama Bwana aishivyo, neno lile Bwana aniambialo, ndilo nitakalolinena.
15 Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
16 Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?
17 Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.
18 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
19 Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.
20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.
22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.
23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.
24 Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya Bwana alitokaje kwangu ili aseme na wewe?
25 Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.
26 Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme;
27 mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.
28 Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.
29 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi.
30 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani.
31 Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.
32 Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele.
33 Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
34 Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
35 Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.
36 Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.
37 Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.
38 Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la Bwana alilolinena.
39 Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
40 Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.
41 Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.
42 Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.
43 Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu.
44 Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.
45 Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
46 Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi.
47 Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme.
48 Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; walakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi.
49 Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali.
50 Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.
51 Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli.
52 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli.
53 Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake.