Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36
1 Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alithibitishwa katika ufalme wake, naye Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno.
2 Sulemani akasema na Israeli wote, na maakida wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila shehe wa Israeli wote, wakuu wa nyumba za mababa.
3 Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo ilipokuwako hema ya kukutania ya Mungu, aliyoifanya Musa mtumishi wa Bwana jangwani.
4 Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu.
5 Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanyiza Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya Bwana; Sulemani na kusanyiko wakaiendea.
6 Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za Bwana, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu yake.
7 Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe.
8 Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake.
9 Basi sasa, Ee Bwana Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi.
10 Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?
11 Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;
12 basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.
13 Akaja Sulemani kutoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya hema ya kukutania, mpaka Yerusalemu; akatawala juu ya Israeli.
14 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
16 Nao farasi, aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi; kila kundi na thamani yake.
17 Nao hupandisha, na kuleta kutoka Misri gari kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi kwa mia na hamsini, vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.
1 Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, na kuujengea ufalme wake nyumba.
2 Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
3 Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro,akisema ,kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi , ajijengee nyumba ya kukaa ,unitendee na mimi.
4 Angalia, najenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za Bwana, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli.
5 Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote.
6 Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake?
7 Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu Daudi.
8 Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako,
9 ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.
10 Na tazama, nitawapa watumishi wako, wachongaji wakatao miti, kori ishirini elfu za ngano iliyopondwa , na kori ishirini elfu za shayiri , na bathi ishirini elfu za mvinyo,na bathi ishirini elfu za mafuta.
11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akajibu kwa waraka, aliompelekea Sulemani, Ni kwa sababu Bwana awapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme juu yao.
12 Hiramu akasema tena, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, aliyezifanya mbingu na nchi, ambaye amempa mfalme Daudi mwana wa hekima, mwenye busara na akili, ili amjengee Bwana nyumba, na nyumba kwa ufalme wake.
13 Na sasa nimemtuma mtu mstadi, mwenye akili, yaani, Hiramu baba yangu.
14 mwana wa mwanamke wa binti za Dani, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, ajuaye sana kazi ya dhahabu, na ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya mawe, na ya mti, ya urujuani, ya samawi, na ya kitani safi, na ya nyekundu; tena mstadi wa kuchora machoro yo yote, na wa kufikiri fikira yo yote; apate kuagiziwa kazi pamoja na watu wako wastadi, tena na wastadi wa bwana wangu Daudi baba yako.
15 Basi sasa hiyo ngano na shayiri, mafuta na mvinyo, aliyonena bwana wangu, na wapelekewe watumishi wake;
16 nasi tutakata miti katika Lebanoni, kadiri utakavyohitaji; na kukuletea tukiieleza baharini mpaka Yafa; nawe utaichukua Yerusalemu.
17 Ndipo Sulemani akawahesabu wageni wote waliokuwamo katika nchi ya Israeli, sawasawa na hesabu aliyowahesabu Daudi baba yake; wakatokea mia hamsini na tatu elfu, na mia sita.
18 Akaweka katika hao sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na themanini elfu wawe wachongaji milimani, na wasimamizi elfu tatu na mia sita, ili wawatie watu kazini.
1 Ndipo Sulemani akaanza kuijenga nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, juu ya mlima Moria, pale Bwana alipomtokea Daudi babaye alipotengeza mahali pale alipoagiza Daudi, katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.
2 Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.
3 Basi hii ndiyo misingi ya majengo ya nyumba ya Mungu aliyoiweka Sulemani. Urefu wake kwa mikono ya cheo cha kwanza ulikuwa mikono sitini, na upana wake mikono ishirini.
4 Na ukumbi uliokuwa mbele yake, urefu wake kadiri ya upana wa nyumba ulikuwa mikono ishirini, na kwenda juu kwake mia na ishirini; akaufunikiza ndani kwa dhahabu safi.
5 Nayo nyumba kubwa akaifunika miti ya miberoshi, aliyoifunikiza kwa dhahabu safi, akaifanyizia mitende na minyororo.
6 Akaipamba nyumba kwa vito iwe na uzuri; nayo dhahabu ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.
7 Tena, akaifunikiza kwa dhahabu nyumba, na boriti, na vizingiti, na kuta zake, na milango yake; akachora makerubi kutani.
8 Akaifanya nyumba ya patakatifu pa patakatifu; urefu wake kadiri ya upana wa nyumba, ulikuwa mikono ishirini, na upana wake mikono ishirini; akaifunikiza kwa dhahabu safi, ya talanta mia sita.
9 Na uzani wa misumari ulikuwa shekeli hamsini za dhahabu. Akazifunikiza orofa zake za juu kwa dhahabu.
10 Na ndani ya nyumba ya patakatifu pa patakatifu akafanyiza makerubi mawili ya kuchonga; wakayafunikiza kwa dhahabu.
11 Na mabawa ya makerubi hayo urefu wake ulikuwa mikono ishirini; bawa moja mikono mitano, likiufikilia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la pili.
12 Na bawa la kerubi la pili lilikuwa mikono mitano, likiufikilia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la kwanza.
13 Yakaenea mabawa ya makerubi hayo mikono ishirini; yakasimama juu ya miguu yao, na nyuso zao ziliielekea nyumba.
14 Akalifanya pazia la samawi na urujuani na nyekundu, na kitani safi, akaifanyizia makerubi.
15 Tena akafanya mbele ya nyumba nguzo mbili za mikono thelathini na tano kwenda juu kwake, na taji iliyokuwa juu yake moja moja ilikuwa mikono mitano.
16 Akafanya minyororo ndani ya chumba cha ndani, akaiweka juu ya vichwa vya nguzo; akafanya makomamanga mia, akayaweka juu ya hiyo minyororo.
17 Akazisimamisha nguzo hizo mbele ya hekalu, moja upande wa kuume, na ya pili upande wa kushoto; akaliita jina la ile ya kuume Yakini, na jina la ile ya kushoto Boazi.
1 Tena akafanya madhabahu ya shaba, mikono ishirini urefu wake, na mikono ishirini upana wake, na mikono kumi kwenda juu kwake.
2 Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ya mviringo, na kwenda juu kwake ilikuwa mikono mitano; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.
3 Na chini yake palikuwa na mifano ya ng'ombe, walioizunguka pande zote ,kwa mikono kumi,wakiizunguka pande zote ile bahari. Ng`ombe walikuwa safu mbili ,wakayeyushwa hapo ilipoyeyushwa hiyo bahari.
4 Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.
5 Na unene wake ulikuwa nyanda nne, na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu tatu, kukaa ndani yake.
6 Akafanya na birika kumi, akaziweka tano upande wa kuume, na tano upande wa kushoto, za kuoshea; ndizo walizooshea mambo ya kafara; lakini hiyo bahari ilikuwa ya makuhani ya kuogea.
7 Akavifanya vinara vya taa kumi vya dhahabu, kadiri ya vilivyoagiziwa; akavitia hekaluni, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto.
8 Akafanya na meza kumi, akazitia hekaluni, tano upande wa kuume, na tano upande wa kushoto. Kisha akafanya mabakuli mia ya dhahabu.
9 Tena akaufanya ua wa makuhani, na ua mkubwa, nayo milango yake, akaifunikiza kwa shaba milango yake.
10 Nayo bahari akaiweka upande wa kuume kwa mashariki, kuelekea kusini.
11 Na Huramu akayafanya masufuria, na majembe, na mabakuli. Basi Huramu akamaliza kufanya hiyo kazi, aliyomfanyia mfalme Sulemani ya nyumba ya Mungu;
12 zile nguzo mbili, na vimbe, na taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo; nazo nyavu mbili za kuzifunika vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo;
13 na makomamanga mia nne ya nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo.
14 Akayafanya na matako, na mabirika akafanya juu ya matako;
15 bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini yake.
16 Masufuria pia, na majembe, na nyuma, na vyombo vyake vyote, Huramu akamfanyia mfalme Sulemani kwa nyumba ya BWANA ,vya shaba iliyokatuka.
17 Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sereda.
18 Ndivyo alivyovifanya Sulemani vyombo hivyo vyote, vingi sana; kwa kuwa uzani wa shaba ulikuwa hautafutikani.
19 Basi Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu, madhabahu ya dhahabu pia, nazo meza, ambazo juu yake iliwekwa mikate ya wonyesho;
20 na vinara na taa zake, ziwake kama ilivyoagizwa mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu iliyosafika;
21 na maua, na taa, na makoleo, ya dhahabu, ndiyo dhahabu bora;
22 na mikasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu iliyosafika; na kwa habari za mahali pa kuingia nyumbani, milango yake ya ndani ya patakatifu pa patakatifu, na milango ya nyumba, yaani ya hekalu, ilikuwa ya dhahabu.
1 Hivyo ikaisha kazi yote Sulemani aliyoifanyia nyumba ya Bwana. Sulemani akaviingiza vitu alivyovitakasa baba yake Daudi; fedha, na dhahabu, na vyombo vyote, akavitia ndani ya hazina za nyumba ya Mungu.
2 Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.
3 Wakakutana watu wote wa Israeli mbele ya mfalme wakati wa sikukuu, katika mwezi wa saba.
4 Wakaja wazee wote wa Israeli, nao Walawi wakajitwika sanduku.
5 Wakalipandisha sanduku, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwamo Hemani, vitu hivyo makuhani Walawi wakavipandisha.
6 Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli, waliokutanika kwake, walikuwako mbele ya sanduku, wakichinja dhabihu za kondoo na ng'ombe, wasiohesabika wala kujumlishwa kwa kuwa wengi.
7 Makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Bwana mahali pake katika chumba cha ndani cha nyumba, patakatifu pa patakatifu, yaani, chini ya mabawa ya makerubi.
8 Kwa maana makerubi yalinyosha mabawa yao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.
9 Na ile miti ilikuwa mirefu, hata ncha za miti zilionekana sandukuni mbele ya chumba cha ndani, lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.
10 Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili alizozitia Musa huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka Misri.
11 Ikawa makuhani walipokwisha kutoka katika patakatifu; (kwani makuhani wote waliokuwapo, walikuwa wamejitakasa, wala hawakuzishika zamu zao;
12 tena Walawi waimbaji, wote pia, yaani Asafu, na Hemani, na Yeduthuni, na wana wao, na ndugu zao, hali wamevaa kitani safi, wenye matoazi na vinanda na vinubi, wamesimama upande wa mashariki wa madhabahu, na pamoja nao makuhani mia na ishirini wakipiga panda;)
13 hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru Bwana nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya Bwana,
14 hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa Bwana.
1 Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.
2 Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.
3 Mfalme akageuza uso wake, akawabarikia mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
4 Akasema, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema,
5 Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wo wote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu ye yote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli;
6 lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli.
7 Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
8 Lakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako;
9 lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu.
10 Basi Bwana amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama Bwana alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
11 Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la Bwana, alilolifanya na wana wa Israeli.
12 Akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono;
13 (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni);
14 akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote;
15 uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
16 Sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu.
17 Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi.
18 Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga!
19 Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee Bwana, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako;
20 ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa.
21 Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
22 Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu;
23 basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
24 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu;
25 basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao.
26 Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo;
27 basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi.
28 Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
29 yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii;
30 basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu);
31 ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
32 Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii;
33 basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako.
34 Ikiwa watu wako wametoka kupigana na adui zao, utakakowatuma ko kote, wakikuomba kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
35 basi uyasikie huko mbinguni wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao.
36 Wakikukosa, (maana hakuna mtu asiyekosa), hata uwakasirikie, na kuwatia mikononi mwa adui zao, wawahamishe, na kuwachukua mateka mpaka nchi iliyo mbali au iliyo karibu;
37 basi wakikumbuka katika nchi walikohamishwa, na kutubu, na kukusihi katika nchi ya uhamisho wao, wakisema, Tumekosa, tumetenda kwa ukaidi, tumefanya maovu;
38 wakurudiapo kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya uhamisho wao, adui walikowahamisha, wakiomba na kuielekea nchi uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
39 basi uyasikie toka mbinguni, toka makaoni mwako, wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako, waliokosa juu yako.
40 Na sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa.
41 Sasa, Ee Bwana, Mungu, uondoke, uende kwenye raha yako, wewe na sanduku la nguvu zako; makuhani wako, Ee Bwana, Mungu, wavikwe wokovu, watakatifu wako na washangilie mema.
42 Ee Bwana, Mungu, usiurudishe nyuma uso wa masihi wako,uzikumbuke fadhili za Daudi mtumishi wako.
1 Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba.
2 Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.
3 Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.
4 Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana.
5 Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu.
6 Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya Bwana, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama.
7 Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta.
8 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.
9 Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.
10 Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.
11 Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.
12 Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.
13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;
14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.
15 Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.
16 Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.
17 Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;
18 ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.
19 Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;
20 ndipo nitawang'oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.
21 Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona Bwana ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?
22 Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao.
1 Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani aliijenga nyumba ya Bwana, na nyumba yake mwenyewe;
2 ndipo Sulemani akaijenga miji ile Hiramu aliyompa Sulemani, akawakalisha humo wana wa Israeli.
3 Naye Sulemani akaenda Hamath-zoba, akaushinda.
4 Akaujenga Tadmori wa nyikani, na miji yote ya hazina, aliyoijenga katika Hamathi.
5 Tena akaujenga Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye boma, yenye kuta, na malango, na makomeo;
6 na Baalathi, na miji yote ya hazina Sulemani aliyokuwa nayo, na miji yote ya magari yake, na miji ya wapanda farasi wake, na ya anasa yote aliyopenda Sulemani kujenga humo Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.
7 Basi kwa habari ya watu wote waliosalia wa Wahiti, na wa Waamori, na wa Waperizi, na wa Wahivi, na wa Wayebusi, wasiokuwa wa Israeli;
8 wa watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuwakomesha, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.
9 Wala katika wana wa Israeli Sulemani hakuwafanya watumwa kazini mwake; lakini hao walikuwa watu wa vita, na wakuu wa majemadari wake, na maakida wa magari yake na wa wapanda farasi wake.
10 Na hao walikuwa maakida wakuu wa Sulemani, watu mia mbili na hamsini, waliotawala juu ya watu.
11 Sulemani akamleta binti Farao kutoka mji wa Daudi mpaka nyumba aliyomjengea; kwa kuwa alisema, Mke wangu hatakaa nyumbani mwa Daudi mfalme wa Israeli, kwa kuwa ni patakatifu, mahali palipofika sanduku la Bwana.
12 Ndipo Sulemani akamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana, aliyoijenga mbele ya ukumbi,
13 kadiri ilivyohitajiwa huduma ya kila siku, akitoa sawasawa na amri ya Musa, siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoamriwa, mara tatu kila mwaka, yaani, sikukuu ya mikate isiyochachwa, na sikukuu ya majuma, na sikukuu ya vibanda.
14 Akaziamuru, sawasawa na agizo la Daudi babaye, zamu za makuhani za kutumika, nao Walawi kwa kadiri ya malinzi yao, ili kusifu, na kuhudumu mbele ya makuhani, kama ilivyohitajiwa kila siku; tena mabawabu kwa zamu zao za kila mlango; maana ndivyo alivyoamuru Daudi mtu wa Mungu.
15 Wala hawakuyaacha maagizo ya mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi kwa neno lo lote, wala kwa habari ya hazina.
16 Basi ikatengenezwa kazi yote ya Sulemani hata siku ya kutiwa msingi wa nyumba ya Bwana, na hata ilipokwisha. Hivyo ikamalizika nyumba ya Bwana.
17 Ndipo Sulemani akaenda Esion-geberi, na Elothi, pwani ya nchi ya Edomu.
18 Naye Hiramu akamletea merikebu kwa mikono ya watumishi wake, na watumishi waliokuwa wana-maji; nao wakafika Ofiri pamoja na watumishi wa Sulemani, wakachukua kutoka huko talanta mia nne na hamsini za dhahabu, wakamletea mfalme Sulemani.
1 Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
2 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.
3 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,
4 na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana; roho yake ilizimia.
5 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6 Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.
7 Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
8 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.
9 Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.
10 Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.
11 Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.
12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13 Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
14 mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15 Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; ngao moja hupata shekeli mia sita za dhahabu iliyofuliwa.
16 Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kigao kimoja hupata shekeli mia tatu za dhahabu; mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.
17 Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.
18 Kiti kile kilikuwa na daraja sita, tena na kikao cha miguu cha dhahabu, navyo vilikuwa vimeshikamana na kiti; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
19 Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita, huko na huko; wala hakikufanyika kwa mfano wake katika ufalme wo wote.
20 Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.
21 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu zilizokwenda Tarshishi pamoja na watumishi wa Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.
22 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.
23 Wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.
24 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.
25 Sulemani akawa na mazizi ya farasi na magari elfu nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
26 Akatawala juu ya wafalme wote toka Mto hata nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri.
27 Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
28 Wakamletea Sulemani farasi kutoka Misri, na kutoka nchi zote.
29 Basi mambo yake Sulemani yaliyosalia, ya kwanza, na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe ya Nathani nabii, katika unabii wa Ahiya, Mshiloni, na katika maono ya Ido mwonaji juu ya Yeroboamu mwana wa Nebati?
30 Akatawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote miaka arobaini.
31 Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa mjini mwa Daudi babaye; akatawala Rehoboamu mwanawe badala yake.
1 Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme.
2 Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.
3 Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,
4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.
5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao.
6 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa?
7 Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote.
8 Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake.
9 Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako.
10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu akiwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.
12 Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.
13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,
14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.
15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.
16 Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao.
17 Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao.
18 Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu.
19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.
1 Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu waliokuwa hodari, watu wa vita, ili wapigane juu ya Israeli, ili wamrudishie Rehoboamu huo ufalme.
2Lakini neno la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema,
3Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, uwaambie na Israeli wote waliomo Yuda na Benyamini, ukisema,
4Bwana asema hivi, Hamtapanda wala kupigana na ndugu zenu; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakayasikiliza maneno ya Bwana, wakarudi katika kumwendea Yeroboamu.
5Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.
6Akajenga na Bethlehemu, na Etamu, na Tekoa,
7na Bethsuri, na Soko, na Adulamu,
8na Gathi, na Maresha, na Zifu,
9na Adoraimu, na Lakishi, na Azeka,
10na Sora, na Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.
11Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.
12Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.
13Wakamwendea makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote, kutoka mpaka wao wote.
14Kwani Walawi wakaacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwatupa, ili wasimfanyie Bwana ukuhani;
15naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozifanya.
16Na kutoka katika kabila zote za Israeli, wakaandamwa na hao waliojikaza nia kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakaja Yerusalemu, ili wamtolee dhabihu Bwana, Mungu wa baba zao.
17Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.
18Rehoboamu akaoa mke, Mahalathi binti Yerimothi mwana wa Daudi, na wa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese;
19akamzalia wana, Yeushi, na Shemaria, na Zahamu.
20Kisha baada yake akamwoa Maaka, binti Absalomu; na yeye akamzalia Abiya, na Atai, na Ziza, na Shelomithi.
21Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa wana ishirini na wanane na binti sitini).
22Rehoboamu akamsimamisha Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme.
23Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi.
1 Ikawa ulipothibitika ufalme wa Rehoboamu, naye amepata nguvu, aliiacha torati ya Bwana, na Israeli wote pamoja naye.
2Ikawa katika mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; kwa kuwa walikuwa wamemwasi Bwana;
3mwenye magari elfu moja na mia mbili, na wapanda farasi sitini elfu; na watu wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye; Walubi, na Wasukii, na Wakushi.
4Akaitwaa miji yenye maboma iliyokuwa ya Yuda, akaja Yerusalemu.
5Ndipo akaja Shemaya nabii kwa Rehoboamu, na kwa wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu kwa sababu ya Shishaki, akawaambia, Bwana asema hivi, Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo nami nimewaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.
6Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, Bwana ndiye mwenye haki.
7Naye Bwana alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la Bwana likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki.
8Walakini watamtumikia; ili wapate kujua utumwa wangu, na huo utumwa wa falme za nchi.
9Basi Shishaki, mfalme wa Misri, akapanda juu ya Yerusalemu, akazichukua hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao za dhahabu alizozifanya Sulemani.
10Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.
11Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa Bwana, wakaja walinzi wakazichukua, wakazirudisha tena chumbani mwa walinzi.
12Naye alipojinyenyekeza, ghadhabu ya Bwana ikamgeukia mbali, asimharibu kabisa; tena yalionekana katika Yuda mambo mema.
13Basi mfalme Rehoboamu akajitia nguvu katika Yerusalemu, akatawala; maana Rehoboamu alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke huko jina lake. Na jina la mamaye aliitwa Naama Mwamoni.
14Naye akatenda yaliyo maovu, kwa kuwa hakuukaza moyo wake amtafute Bwana.
15Basi mambo yake Rehoboamu, ya kwanza na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe za Shemaya nabii na Ido mwonaji, kwa jinsi ya kuandika nasaba? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote.
16Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa katika mji wa Daudi. Na Abiya mwanawe alitawala mahali pake.
1 Katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu, akaanza Abiya kutawala juu ya Yuda.
2 Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka binti Urieli wa Gibea. Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.
3 Abiya akapanga vita mwenye jeshi la watu hodari wa vita, watu wateule mia nne elfu; naye Yeroboamu akapanga vita juu yake mwenye watu wateule mia nane elfu, waliokuwa waume mashujaa.
4 Basi Abiya akasimama juu ya kilima cha Semaraimu, kilichoko milimani mwa Efraimu, akasema, Nisikieni, enyi Yeroboamu na Israeli wote;
5 je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?
6 Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati, mtumwa wa Sulemani mwana wa Daudi, akainuka, akamfanyia fitina bwana wake.
7 Wakamkusanyikia watu mabaradhuli, wasiofaa kitu, waliojitia nguvu juu ya Rehoboamu mwana wa Sulemani, Rehoboamu alipokuwa kijana na wa moyo mwororo, asiweze kuwazuia.
8 Hata sasa mwajidhania kuwa mtauzuia ufalme wa Bwana mikononi mwa wana wa Daudi; nanyi mmekuwa jamii kubwa, na kwenu mna ndama za dhahabu alizowafanyia Yeroboamu kuwa miungu.
9 Je! Hamkuwafukuza makuhani wa Bwana, wana wa Haruni, na Walawi; mkajifanyia makuhani kama wafanyavyo watu wa nchi nyingine? Hata ye yote ajaye kujifanya wakfu na ndama, na kondoo waume saba, aweza kuwa kuhani wa hiyo isiyo miungu.
10 Lakini sisi, Bwana ndiye Mungu wetu, wala sisi hatukumwacha; tena tunao makuhani wanaomtumikia Bwana, wana wa Haruni, na Walawi, kwa kazi yao;
11 nao humtolea Bwana kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi twayalinda malinzi ya Bwana, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha.
12 Na tazama, Mungu yu pamoja nasi atutangulie, na makuhani wake wenye mapanda, ili wapige sauti ya kugutusha juu yenu. Enyi wana wa Israeli, msipigane na Bwana, Mungu wa baba zenu; kwani hamtafanikiwa.
13 Lakini Yeroboamu aliwazungushia waviziao kwa nyuma; basi wao wakawa mbele ya Yuda, na wale waviziao nyuma yao.
14 Na Yuda walipotazama nyuma, angalia, vita vikawa mbele na nyuma; wakamlilia Bwana, na makuhani wakapiga mapanda.
15 Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda.
16 Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao.
17 Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli mia tano elfu, watu wateule.
18 Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea Bwana, Mungu wa baba zao.
19 Abiya akamfuata Yeroboamu, akamnyang'anya miji, Betheli na miji yake, na Yeshana na miji yake, na Efroni na miji yake.
20 Wala Yeroboamu hakupata nguvu tena siku za Abiya; kisha Bwana akampiga, akafa.
21 Ila Abiya akapata nguvu, akaoa wake kumi na wanne, akazaa wana ishirini na wawili, na binti kumi na sita.
22 Na mambo ya Abiya yaliyosalia, na njia zake, na maneno yake, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.
1 Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi.
2 Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa Bwana, Mungu wake;
3 maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera;
4 akawaamuru Yuda wamtafute Bwana, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri.
5 Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake.
6 Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu Bwana amemstarehesha.
7 Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta Bwana, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.
8 Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa.
9 Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha.
10 Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha.
11 Naye Asa akamlilia Bwana, Mungu wake, akasema, Bwana, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee Bwana, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu.
12 Basi, Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia.
13 Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; nao wengi wakaanguka wa Wakushi hata wasiweze kupona; kwa sababu waliangamizwa mbele za Bwana, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka mengi sana.
14 Wakaipiga miji yote kando-kando ya Gerari; maana hofu ya Bwana ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno.
15 Wakazipiga pia hema za ng'ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu.
1 Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;
2 naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; Bwana yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.
3 Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;
4 lakini walipomgeukia Bwana, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.
5 Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.
6 Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.
7 Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.
8 Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya Bwana, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa Bwana.
9 Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.
10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.
11 Wakamchinjia Bwana siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng'ombe mia saba, na kondoo elfu saba.
12 Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta Bwana, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;
13 na ya kwamba ye yote asiyemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke.
14 Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa mapanda, na kwa baragumu.
15 Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye Bwana akawastarehesha pande zote.
16 Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.
17 Lakini mahali pa juu hapakuondolewa katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.
18 Akavileta nyumbani mwa Mungu vitu alivyovitakasa babaye, na vile alivyovitakasa mwenyewe, fedha, na dhahabu, na vyombo.
19 Wala hapakuwa na vita tena hata mwaka wa thelathini na tano wa kutawala kwake Asa.
1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwake Asa, Baasha mfalme wa Israeli akapanda juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.
2 Ndipo Asa akatoa fedha na dhahabu katika hazina za nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, akampelekea Ben-hadadi mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,
3 Kwangu na kwako na liwe agano kama lilivyokuwa kwa baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea fedha na dhahabu; basi, uvunje agano lako na Baasha, mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.
4 Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawapeleka maakida wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli; wakapiga Iyoni, na Dani, na Abel-maimu, na miji ya hazina yote ya Naftali.
5 Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuujenga Rama, akaikomesha kazi yake.
6 Ndipo mfalme Asa akawatwaa Yuda wote; nao wakayachukua mawe ya Rama, na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye akajenga kwa vitu hivyo Geba na Mispa.
7 Wakati ule Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea Bwana, Mungu wako, kwa hiyo limeokoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.
8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? Lakini, kwa kuwa ulimtegemea Bwana, aliwatia mkononi mwako.
9 Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita.
10 Ndipo Asa akamkasirikia mwonaji, akamtia nyumbani mwa mkatale; maana amemghadhibikia kwa sababu ya neno hilo. Na Asa akawaonea baadhi ya watu wakati ule ule.
11 Na tazama, mambo yake Asa, ya kwanza na ya mwisho, angalia, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
12 Akashikwa Asa na ugonjwa wa miguu katika mwaka wa thelathini na kenda wa kumiliki kwake; ugonjwa wake ukazidi sana; lakini hakumtafuta Bwana katika ugonjwa wake, bali waganga.
13 Asa akalala na babaze, akafa katika mwaka wa arobaini na mmoja wa kumiliki kwake.
14 Wakamzika katika makaburi yake mwenyewe, aliyojichimbia katika mji wa Daudi, wakamlaza juu ya kitanda kilichojazwa manukato, na kila namna ya machanganyiko ya hao mafundi wa dawa; wakamfukizia mafukizo makuu sana.
1 Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake, akajitia nguvu juu ya Israeli.
2 Akaweka jeshi katika miji yote yenye maboma ya Yuda, akatia na askari walinzi katika nchi ya Yuda, na katika miji ya Efraimu, aliyoitwaa Asa babaye.
3 Naye Bwana alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali;
4 lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri zake, wala si katika matendo ya Israeli.
5 Kwa hiyo Bwana akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote; basi akawa na mali na heshima tele.
6 Ukainuliwa moyo wake katika njia za Bwana; na zaidi ya hayo akapaondoa mahali pa juu, na maashera, katika Yuda.
7 Tena, katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake, akawatuma wakuu wake, yaani, Ben-haili, na Obadia, na Zekaria, na Nethaneli, na Mikaya, ili kufundisha mijini mwa Yuda;
8 na pamoja nao Walawi, yaani, Shemaya, na Nethania, na Zebadia, na Asaheli, na Shemiramothi, na Yehonathani, na Adonia, na Tobia, na Tob-adonia, Walawi; na pamoja nao Elishama na Yehoramu, makuhani.
9 Wakafundisha katika Yuda, wenye kitabu cha torati ya Bwana; wakazunguka katika miji yote ya Yuda, wakafundisha kati ya watu.
10 Hofu ya Bwana ikaziangukia falme za nchi zote zilizozunguka Yuda, wasipigane vita na Yehoshafati.
11 Na baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi, na fedha ya kodi; Waarabu nao wakamletea makundi, kondoo waume saba elfu na mia saba, na mabeberu saba elfu na mia saba.
12 Ukuu wake Yehoshafati ukazidi sana; akajenga katika Yuda ngome na miji ya hazina.
13 Naye alikuwa na kazi nyingi katika miji ya Yuda; na watu wa vita, watu mashujaa humo Yerusalemu.
14 Na hivi ndivyo walivyohesabiwa kwa mbari za baba zao; wa Yuda, maakida wa maelfu; Adna jemadari, na pamoja naye watu mashujaa mia tatu elfu;
15 na wa pili wake Yehohanani akida, na pamoja naye mia mbili na themanini elfu;
16 na baada yake Amasia mwana wa Zikri, aliyejitoa kwa Bwana kwa moyo, na pamoja naye mia mbili elfu, watu mashujaa;
17 na wa Benyamini; Eliada mtu shujaa, na pamoja naye mia mbili elfu wenye nyuta na ngao;
18 na wa pili wake Yehozabadi, na pamoja naye mia na themanini elfu waliojiweka tayari kwa vita.
19 Hao ndio waliomngojea mfalme, zaidi ya hao mfalme aliowaweka katika miji yenye maboma katika Yuda yote.
1 Basi, Yehoshafati alikuwa na mali na heshima tele, tena akafanya ujamaa na Ahabu.
2 Hata baada ya miaka kadha wa kadha akamshukia Ahabu huko Samaria. Ahabu akamchinjia kondoo na ng'ombe tele, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, akamshawishi ili apande pamoja naye waende Ramoth-gileadi.
3 Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani.
4 Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.
5 Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, Kwea; kwa kuwa Mungu atautia mkononi mwa mfalme.
6 Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye?
7 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.
8 Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla.
9 Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye sakafu pa kuingilia lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao.
10 Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia.
11 Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.
12 Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.
13 Mikaya akasema, Kama aishivyo Bwana, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.
14 Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu.
15 Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?
16 Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.
17 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
18 Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.
19 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
20 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani?
21 Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo.
22 Basi sasa, angalia, Bwana ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye Bwana amenena mabaya juu yako.
23 Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya Bwana ili aseme na wewe?
24 Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.
25 Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme;
26 mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.
27 Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.
28 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi.
29 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani.
30 Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru maakida wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.
31 Ikawa maakida wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na Bwana akamsaidia; Mungu akawafarakisha kwake.
32 Ikawa, maakida wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.
33 Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.
34 Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua.
1 Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.
2 Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao Bwana? Kwa ajili ya hayo ghadhabu i juu yako itokayo kwa Bwana.
3 Walakini yameonekana mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.
4 Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao.
5 Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;
6 akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.
7 Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.
8 Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu.
9 Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili.
10 Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.
11 Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema
1 Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani.
2 Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi).
3 Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.
4 Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana.
5 Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa Bwana, mbele ya ua mpya;
6 akasema, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako.
7 Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele?
8 Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema,
9 Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa.
10 Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu;
11 tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha.
12 Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako.
13 Wakasimama Yuda wote mbele za Bwana, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao.
14 Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko;
15 akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.
16 Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli.
17 Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa Bwana ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa Bwana yu pamoja nanyi.
18 Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana.
19 Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.
20 Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.
21 Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele.
22 Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa.
23 Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe.
24 Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka.
25 Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana.
26 Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia Bwana; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo.
27 Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa Bwana amewafurahisha juu ya adui zao.
28 Wakafika Yerusalemu wenye vinanda vinubi na mapanda kwenda nyumbani kwa Bwana.
29 Ikawa hofu ya Mungu juu ya falme zote za nchi, waliposikia ya kuwa Bwana amepigana juu ya adui za Israeli.
30 Basi ukatulia ufalme wake Yehoshafati; kwa sababu Mungu wake alimstarehesha pande zote.
31 Yehoshafati akatawala juu ya Yuda; alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.
32 Akaiendea njia ya Asa babaye, wala hakuiacha, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana.
33 Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; wala mioyo ya watu bado haijakazwa kwa Mungu wa baba zao.
34 Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, angalia, yameandikwa katika tarehe ya Yehu mwana wa Hanani, iliyotiwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli.
35 Baada ya hayo Yehoshafati mfalme wa Yuda akapatana na Ahazia mfalme wa Israeli; naye huyo ndiye aliyefanya mabaya mno;
36 akapatana naye kufanya merikebu za kuendea Tarshishi; wakazifanya merikebu zile huko Esion-geberi.
37 Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii juu ya Yehoshafati, akasema, Kwa sababu umepatana na Ahazia, Bwana amezivunja-vunja kazi zako. Zikavunjika merikebu, zisiweze kufika Tarshishi.
1 Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; akatawala Yehoramu mwanawe mahali pake.
2 Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, na Yehieli, na Zekaria, na Azaria, na Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli.
3 Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, na za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza.
4 Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujitia nguvu, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia.
5 Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.
6 Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya maovu machoni pa Bwana.
7 Walakini Bwana hakupenda kuiharibu nyumba ya Daudi, kwa sababu ya agano alilolifanya na Daudi, na kama alivyomwahidi kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.
8 Zamani zake Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, wakajifanyia mfalme.
9 Ndipo akavuka Yehoramu na maakida wake, na magari yake yote pamoja naye; akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na hao maakida wa magari.
10 Hivyo Edomu wakaasi chini ya mkono wa Yuda, hata leo; wakaasi na Libna zamani zizo hizo chini ya mkono wake: kwa sababu alikuwa amemwacha Bwana, Mungu wa baba zake.
11 Tena ndiye aliyefanya mahali pa juu milimani pa Yuda, na kuwaendesha katika uasherati wenyeji wa Yerusalemu, na kuwakosesha Yuda.
12 Likamjia andiko kutoka kwa Eliya nabii, kusema, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa sababu hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;
13 lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaendesha katika uasherati Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;
14 tazama, Bwana atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;
15 nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku.
16 Bwana akawaamsha roho Wafilisti, na Waarabu waliowaelekea Wakushi juu ya Yehoramu,
17 nao wakakwea juu ya nchi ya Yuda, wakaipenya, wakaichukua mali yote iliyoonekama nyumbani mwa mfalme, na wanawe pia, na wakeze; asisaziwe mwana hata mmoja, ila Ahazia, aliyekuwa mdogo miongoni mwa wanawe.
18 Na baada ya hayo yote Bwana akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka.
19 Ikawa baada ya siku, ikiisha miaka miwili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiugua vibaya. Wala watu wake hawakumfukizia mafukizo kama ya baba zake.
20 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.
1 Nao wenyeji wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja matuoni pamoja na Waarabu. Hivyo akatawala Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda.
2 Ahazia alikuwa na umri wa miaka arobaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri.
3 Yeye naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu.
4 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, alipokwisha kufa babaye, hata aangamie.
5 Naye akaenda kwa mashauri yao, akafuatana na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-Gileadi;nao Washami wakamjeruhi Yoramu.
6 Akarudi Yezreeli ili aponye jeraha walizomjeruhi huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda ,akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu,katika Yezreeli,kwa sababu alikuwa hawezi.
7 Basi kuangamia kwake Ahazia kulitokana na Mungu, kwa vile alivyomwendea Yoramu; kwa kuwa alipofika, akatoka pamoja na Yoramu juu ya Yehu mwana wa Nimshi, ambaye Bwana alimtia mafuta ili awakatilie mbali nyumba ya Ahabu.
8 Ikawa, Yehu alipokuwa akiwafanyia hukumu nyumba ya Ahabu, aliwakuta wakuu wa Yuda, na wana wa nduguze Ahazia, wakimtumikia Ahazia, akawaua.
9 Akamtafuta Ahazia, wakamkamata, (naye alikuwa amejificha Samaria,) wakamleta kwa Yehu, wakamwua; wakamzika, kwa maana wakasema, Huyu ni mwana wa Yehoshafati, huyo aliyemtafuta Bwana kwa moyo wake wote. Wala nyumba ya Ahazia hawakuwa na uwezo wa kuushika ufalme.
10 Basi Athalia, mama wa Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaangamiza wazao wote wa kifalme wa nyumba ya Yuda.
11 Ila Yehosheba, binti mfalme, akamtwaa Yoashi, mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliouawa, akamweka yeye na yaya wake katika chumba cha kulala. Basi Yehosheba, binti mfalme Yehoramu, mkewe Yehoyada kuhani, (naye alikuwa umbu lake Ahazia,) akaficha usoni pa Athalia, asimwue.
12 Akawako pamoja nao, amefichwa nyumbani mwa Mungu, miaka sita. Na Athalia akaitawala nchi.
1 Hata mwaka wa saba Yehoyada akajitia nguvu, akawatwaa maakida wa mamia, Azaria mwana wa Yerohamu, na Ishmaeli mwana wa Yehohanani, na Azaria mwana wa Obedi, na Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri, akapatana nao.
2 Wakazunguka katikati ya Yuda, wakawakusanya Walawi kutoka katika miji yote ya Yuda, na wakuu wa nyumba za mababa wa Israeli, wakaja Yerusalemu.
3 Na kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme nyumbani mwa Mungu. Akawaambia, Angalieni, mwana wa mfalme atatawala, kama Bwana alivyonena juu ya wana wa Daudi.
4 Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, ninyi mwingiao siku ya sabato, wa makuhani, na wa Walawi, mtalinda milangoni;
5 na theluthi nyumbani pa mfalme; na theluthi mlangoni pa msingi; na watu wote watakuwapo nyuani mwa nyumba ya Bwana.
6 Wala asiingie mtu nyumbani mwa Bwana, ila makuhani, na hao watumikao wa Walawi; hao wataingia, kwa kuwa hao ni watakatifu; ila watu wote watalinda malinzi ya Bwana.
7 Nao Walawi watamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye nyumbani na auawe; nanyi mfuatane na mfalme, aingiapo na atokapo.
8 Basi Walawi na Yuda wote wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia siku ya sabato, na wale watakaotoka siku ya sabato; kwa maana Yehoyada kuhani hakuzifumua zamu.
9 Naye Yehoyada kuhani akawapa maakida wa mamia mikuki, na ngao, na vigao, vilivyokuwa vya mfalme Daudi, vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu.
10 Akawasimamisha watu wote, kila mtu mwenye silaha yake mkononi, toka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto, upande wa madhabahu na nyumba, kumzunguka mfalme pande zote.
11 Ndipo wakamleta nje mwana wa mfalme, wakamvika taji, na kumpa ule ushuhuda, wakamtawaza awe mfalme; Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, wakasema, Mfalme na aishi.
12 Na Athalia alipoisikia sauti ya watu, na ya walinzi, na ya hao waliomsifu mfalme, akaingia kwa watu nyumbani mwa Bwana;
13 akatazama, na angalia, mfalme amesimama karibu na nguzo yake mlangoni, nao maakida na wenye mapanda karibu na mfalme; wakafurahi watu wote wa nchi, wakapiga mapanda; waimbaji pia wakipiga vinanda, wakaongoza nyimbo za kusifu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akasema, Fitina! Fitina!
14 Yehoyada kuhani akawaleta nje maakida wa mamia, waliowekwa juu ya jeshi, akawaambia, Mtoeni nje kati ya safu; naye ye yote amfuataye, na auawe kwa upanga; kwani kuhani amesema, Msimwue katika nyumba ya Bwana.
15 Basi wakampisha njia; akaenda kwa kuingia pa mlango wa farasi nyumbani mwa mfalme; nao wakamwua huko.
16 Kisha, Yehoyada akafanya agano, yeye na watu wote, na mfalme, kwamba watakuwa watu wa Bwana.
17 Na watu wote wakaiendea nyumba ya Baali, wakaibomoa; wakavunja-vunja madhabahu zake na sanamu zake, wakamwua Matani kuhani wa Baali mbele ya madhabahu.
18 Yehoyada akauamuru usimamizi wa nyumba ya Bwana chini ya mkono wa makuhani Walawi, aliowagawa Daudi nyumbani mwa Bwana, ili wazisongeze sadaka za kuteketezwa za Bwana, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, kwa kufurahi na kuimba, kama alivyoamuru Daudi.
19 Akawasimamisha walinzi malangoni pa nyumba ya Bwana, asiingie aliye mchafu kwa vyo vyote.
20 Akawatwaa maakida wa mamia, na watu wakubwa, na hao watawalao watu, na watu wote wa nchi, akamtelemsha mfalme kutoka nyumba ya Bwana; wakalipitia lango la juu waende nyumbani kwa mfalme, wakamketisha mfalme katika kiti cha ufalme.
21 Basi wakafurahi watu wote wa nchi, na mji ukatulia; naye Athalia wakamwua kwa upanga.
1 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana siku zote za Yehoyada kuhani.
3 Yehoyada akamwoza wake wawili, naye akazaa wana na binti.
4 Ikawa baada ya haya, Yoashi alikuwa na nia ya kuitengeneza nyumba ya Mungu.
5 Akawakusanya makuhani na Walawi, akawaambia, Nendeni mijini mwa Yuda, mkakusanye katika Israeli wote fedha, ili kuitengeneza nyumba ya Mungu wenu mwaka kwa mwaka, mkafanye bidii kuliharakisha neno hili. Walakini Walawi hawakuliharakisha.
6 Mfalme akamwita Yehoyada mkuu wao, akamwambia, Mbona hukuwataka Walawi waitoze Yuda na Yerusalemu kodi ya Musa mtumishi wa Bwana, na ya kusanyiko la Israeli, kwa ajili ya hema ya ushuhuda?
7 Kwa kuwa wana wa Athalia, yule mwanamke mwovu, walikuwa wameibomoa nyumba ya Mungu; na vitakatifu vyote vya nyumba ya Bwana wamewapatia mabaali.
8 Basi mfalme akaamuru, nao wakafanyiza kasha, wakaliweka nje langoni pa nyumba ya Bwana.
9 Wakapiga mbiu katika Yuda na Yerusalemu, kumletea Bwana kodi aliyoiweka Musa mtumishi wa Mungu, juu ya Israeli jangwani.
10 Wakafurahi maakida wote na watu wote, wakaleta na kutia ndani ya kasha, hata wakaisha.
11 Ikawa wakati walipoletewa kasha wasimamizi wa mfalme kwa mkono wa Walawi, nao wakaona ya kwamba kuna fedha nyingi, huja karani wa mfalme, na msimamizi wake kuhani mkuu, wakatoa yaliyomo kashani, kisha hulichukua kasha, na kulirudisha mahali pake. Ndivyo walivyofanya siku kwa siku, wakakusanya fedha tele.
12 Na mfalme na Yehoyada waliwapa hao waliofanya kazi ya utumishi wa nyumba ya Bwana; nao wakawaajiri waashi na maseremala ili kuitengeza nyumba ya Bwana, na hao pia wafuao chuma na shaba ili kuitengeza nyumba ya Bwana.
13 Hivyo mafundi wakafanya kazi yao, nao wakaimaliza, wakaisimamisha nyumba ya Mungu kama ilivyopasa, wakaifanya imara.
14 Nao walipokwisha, wakaleta mbele ya mfalme na Yehoyada fedha iliyobaki, vikafanyizwa kwayo vyombo vya nyumba ya Bwana, vyombo vya utumishi, navyo vya kutolea, na miiko, na vyombo vya dhahabu na fedha. Wakatoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya Bwana, daima, siku zote za Yehoyada.
15 Lakini Yehoyada akawa mzee, mwenye umri mwingi, akafa; alipokufa alikuwa na umri wa miaka mia na thelathini.
16 Wakamzika katika mji wa Daudi kati ya wafalme, kwa sababu ametenda mema katika Israeli, na kwa Mungu, na katika nyumba yake.
17 Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.
18 Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
19 Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.
20 Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.
21 Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana.
22 Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.
23 Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote.
24 Maana wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno, kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao. Hivyo wakamfanyia Yoashi hukumu.
25 Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi,) watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi, lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.
26 Na hawa ndio waliomfanyia fitina, Zabadi mwana wa Shimeathi mwanamke Mwamoni, na Yehozabadi mwana wa Shimrithi mwanamke Mmoabi.
27 Basi kwa habari ya wanawe, na ukubwa wa mizigo aliolemewa, na majengo ya nyumba ya Mungu, tazama, hayo yameandikwa katika maelezo ya kitabu cha wafalme. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.
1 Amazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, lakini si kwa moyo mkamilifu.
3 Basi ikawa, alipopata nguvu katika ufalme wake, akawaua watumishi wale waliomwua mfalme babaye.
4 Lakini watoto wao hakuwaua, ila alifanya sawasawa na hayo yaliyoandikwa katika torati, katika kitabu cha Musa, kama Bwana alivyoamuru, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa dhambi yake mwenyewe.
5 Tena Amazia akawakusanya Yuda, akawaweka sawasawa na nyumba za baba zao chini ya maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, naam, Yuda pia, na Benyamini; tangu wenye miaka ishirini na zaidi akawahesabu, akawaona kuwa watu wateule mia tatu elfu, wawezao kwenda vitani, waliozoea mkuki na ngao.
6 Akaajiri pia watu mashujaa mia elfu wa Israeli kwa talanta mia za fedha.
7 Lakini mtu wa Mungu akamjia, akasema, Ee mfalme, usiwaache jeshi la Israeli waende nawe; kwa kuwa Bwana hayupo pamoja na Israeli, yaani, wana wote wa Efraimu.
8 Lakini ukitaka kwenda, haya, jitie nguvu upigane; Mungu atakuangusha mbele ya adui; maana Mungu anazo nguvu za kusaidia, na kuangusha.
9 Amazia akamwambia mtu wa Mungu, Lakini tuzifanyieje zile talanta mia nilizowapa jeshi la Israeli? Mtu wa Mungu akajibu, Bwana aweza kukupa zaidi sana kuliko hizo.
10 Ndipo Amazia akawafarakisha jeshi lililomjia kutoka Efraimu, ili warudi kwao; kwa hiyo ikawaka sana hasira yao juu ya Yuda, nao wakarudi kwao wenye hasira kali.
11 Amazia akapiga moyo konde, akawaongoza watu wake, akaenda mpaka Bonde la Chumvi, akawapiga katika wana wa Seiri watu elfu kumi.
12 Na elfu kumi wengine, ambao wana wa Yuda waliwachukua wali hai, wakawaleta juu ya jabali, wakawaangusha toka juu ya jabali, hata wakavunjika-vunjika wote.
13 Lakini wale watu wa jeshi, aliowarudisha Amazia, wasiende naye vitani, hao wakaiteka miji ya Yuda, tangu Samaria mpaka Beth-horoni, wakawapiga watu elfu tatu, wakachukua nyara nyingi.
14 Basi ikawa, Amazia alipokwisha rudi kutoka kuwaua Waedomi, alileta miungu ya wana wa Seiri, akaisimamisha kuwa miungu yake, akajiinama mbele yao, akaifukizia uvumba.
15 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?
16 Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.
17 Ndipo mfalme Amazia akafanya shauri, akatuma wajumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu,mfalme wa Israeli,kusema,njoo,tutazamane uso kwa uso.
18 Na Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma wajumbe kwa Amazia mfalme wa Yuda, kusema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ukatuma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.
19 Wasema, Tazama, umewapiga Edomu; na moyo wako wakutukuza ujisifu; kaa nyumbani mwako basi; mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?
20 Lakini Amazia hakutaka kusikia, kwa maana hayo yalitoka kwa Mungu, ili awatie mikononi mwao, kwa kuwa wameitafuta miungu ya Edomu.
21 Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda huko Beth-shemeshi, ulio wa Yuda.
22 Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.
23 Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi,akamchukua mpaka Yerusalemu ,akauvunja ukuta wa Yerusalemu , toka lango la Efraimu mpaka lango la pembeni ,mikono mia nne.
24 Akaitwaa dhahabu yote, na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana nyumbani mwa Mungu kwa Obed-edomu, na hazina za nyumba ya mfalme, tena watu kuwa amana, akarudi Samaria.
25 Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mfalme wa Israeli, miaka kumi na mitano.
26 Na mambo yote ya Amazia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, tazama, je! Hayakuandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli?
27 Basi, toka wakati alipogeuka Amazia katika kumfuata Bwana, wakamfanyia fitina katika Yerusalemu; naye akakimbia mpaka Lakishi; lakini wakatuma kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.
28 Wakamleta juu ya farasi; wakamzika pamoja na babaze katika mji wa Yuda.
1 Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, naye alikuwa mwenye miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa Amazia babaye.
2 Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.
3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.
4 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye.
5 Akajitia nia amtafute Mungu katika siku za Zekaria, aliyekuwa na fahamu katika maono ya Mungu; na muda alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.
6 Akatoka akapigana na Wafilisti, akauvunja ukuta wa Gathi, na ukuta wa Yabne, na ukuta wa Ashdodi; akajenga miji katika Ashdodi na katikati ya Wafilisti.
7 Mungu akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni.
8 Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka pa kuingilia Misri; kwa kuwa akaongezeka nguvu mno.
9 Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye lango la pembeni, na penye lango la bonde, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu.
10 Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabirika mengi, maana alikuwa na ng'ombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima.
11 Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, sawasawa na hesabu walivyohesabiwa na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa maakida wa mfalme.
12 Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita.
13 Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, mia tatu na saba elfu, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui.
14 Uzia akawafanyizia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo.
15 Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya minara na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.
16 Lakini alipokuwa na nguvu, moyo wake ulitukuka, hata akafanya maovu, akamwasi Bwana, Mungu wake; kwani aliingia hekaluni mwa Bwana, ili afukize uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia.
17 Azaria kuhani akaingia nyuma yake, na pamoja naye makuhani themanini wa Bwana, mashujaa;
18 wakamzuia Uzia mfalme, wakamwambia, Si haki yako, Uzia, kumfukizia Bwana uvumba, ila ni haki ya makuhani wana wa Haruni, waliofanywa wakfu, ili wafukize uvumba; toka katika patakatifu; kwa kuwa umekosa; wala haitakuwa kwa heshima yako kutoka kwa Bwana, Mungu.
19 Akaghadhibika Uzia; naye alikuwa na chetezo mkononi cha kufukizia uvumba; naye hapo alipowaghadhibikia makuhani, ukamtokea ukoma katika paji la uso wake mbele ya makuhani nyumbani mwa Bwana karibu na madhabahu ya kufukizia.
20 Azaria kuhani mkuu na makuhani wote wakamtazama, na angalia, alikuwa na ukoma pajini mwa uso, wakamtoa humo upesi; hata na yeye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu Bwana amempiga.
21 Uzia mfalme akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee, kwa kuwa ni mwenye ukoma; maana alitengwa na nyumba ya Bwana; na Yothamu mwanawe alikuwa juu ya nyumba ya mfalme, akiwahukumu watu wa nchi.
22 Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, aliyaandika Isaya nabii, mwana wa Amozi.
23 Basi Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze katika konde la kuzikia la wafalme; kwa kuwa walisema, Huyu ni mwenye ukoma. Na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake
1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Uzia babaye; isipokuwa hakuingia hekaluni mwa Bwana. Lakini watu walikuwa wakali kufanya maovu.
3 Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya Bwana, na juu ya ukuta wa Ofeli akajenga sana.
4 Tena akajenga miji katika milima ya Yuda, na mwituni akajenga ngome na minara.
5 Kisha akapigana na mfalme wa wana wa Amoni, akawashinda. Na wana wa Amoni wakampa mwaka ule ule talanta mia za fedha, na kori elfu kumi za ngano, na elfu kumi za shayiri. Hayo ndiyo waliyomtolea wana wa Amoni, mwaka wa pili pia, na mwaka wa tatu.
6 Basi Yothamu akawa na nguvu, kwa kuwa alizitengeneza njia zake mbele za Bwana, Mungu wake.
7 Na mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na vita vyake vyote, na njia zake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita huko Yerusalemu.
9 Yothamu akalala na babaze, wakamzika katika mji wa Daudi; na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.
1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, kama Daudi babaye;
2 bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, akawafanyizia mabaali sanamu za kusubu.
3 Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.
4 Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
5 Kwa hiyo Bwana, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu.
6 Kwa kuwa Peka mwana wa Remalia akawaua katika Yuda siku moja watu mia na ishirini elfu, mashujaa wote; kwa sababu walikuwa wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao.
7 Naye Zikri, mtu hodari wa Efraimu, akawaua Maaseya mwana wa mfalme, na Azrikamu mkuu wa nyumba, na Elkana, aliyekuwa wa pili wake mfalme.
8 Wana wa Israeli wakachukua wa ndugu zao wafungwa mia mbili elfu, wanawake, na wana, na binti, pia wakachukua kwao nyara nyingi, wakazileta nyara Samaria.
9 Lakini kulikuwako huko nabii wa Bwana, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa Bwana, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni.
10 Na sasa mwanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu, wawe kwenu watumwa na wajakazi; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya Bwana, Mungu wenu?
11 Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya Bwana iliyo kali i juu yenu.
12 Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai,
13 wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za Bwana, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli.
14 Basi watu wenye silaha wakawaacha wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote.
15 Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wote wao waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria.
16 Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie.
17 Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa.
18 Wafilisti pia walikuwa wameingia miji ya Shefela, na ya Negebu ya Yuda, nao wameutwaa Beth-shemeshi, na Ayaloni, na Gederothi, na Soko pamoja na miji yake, na Timna pamoja na miji yake, na Gimzo pia na miji yake; wakakaa humo.
19 Kwa maana Bwana aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi Bwana mno.
20 Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lo lote.
21 Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya Bwana, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo.
22 Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi Bwana, huyo mfalme Ahazi.
23 Kwani akaitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote.
24 Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya Bwana; akajifanyizia madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu.
25 Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha Bwana, Mungu wa babaze.
26 Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
27 Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.
1 Hezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Abiya binti Zekaria.
2 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.
3 Yeye, katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake, katika mwezi wa kwanza, aliifungua milango ya nyumba ya Bwana, akaitengeneza.
4 Akawaingiza makuhani na Walawi, akawakusanya uwandani upande wa mashariki,
5 akawaambia, Nisikieni, enyi Walawi; jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zenu, mkautoe uchafu katika patakatifu.
6 Kwa maana baba zetu wameasi, na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, Mungu wetu, wamemwacha, na kugeuzia mbali nyuso zao na makao ya Bwana, na kumpa maungo.
7 Tena wameifunga milango ya ukumbi, na kuzizima taa, wala hawakufukiza uvumba, wala hawakumtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa katika patakatifu.
8 Kwa hiyo hasira ya Bwana imekuwa juu ya Yuda na Yerusalemu, naye amewatoa kuwa matetemeko, wawe ushangao, na mazomeo, kama mwonavyo kwa macho yenu.
9 Kwa kuwa, tazama, baba zetu wameangamia kwa upanga, na wana wetu, na binti zetu, na wake zetu wametekwa kwa ajili ya hayo.
10 Basi nia yangu ni kufanya agano na Bwana, Mungu wa Israeli, ili kwamba hasira yake kali itugeukie mbali.
11 Basi wanangu, msijipurukushe sasa, kwa kuwa Bwana amewachagua ninyi msimame mbele yake, kumhudumia, nanyi mpate kuwa watumishi wake, mkafukize uvumba.
12 Ndipo wakaondoka Walawi, Mahathi mwana wa Amasai, na Yoeli mwana wa Azaria, wa wana wa Wakohathi; na wa wana wa Merari, Kishi mwana wa Abdi, na Azaria mwana wa Yehaleleli; na wa Wagershoni, Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13 na wa wana wa Elisafani, Shimri na Yeueli; na wa wana wa Asafu, Zekaria na Matania;
14 na wa wana wa Hemani, Yehueli na Shimei; na wa wana wa Yeduthuni, Shemaya na Uzieli.
15 Wakawakusanya ndugu zao, wakajitakasa, wakaingia, kama alivyoamuru mfalme kwa maneno ya Bwana, ili waisafishe nyumba ya Bwana.
16 Nao makuhani wakaingia nyumbani mwa Bwana, katika mahali pa ndani, ili waisafishe, wakatoa uchafu wote waliouona hekaluni mwa Bwana, wakautupa nje uani mwa nyumba ya Bwana. Walawi wakautwaa, ili wauchukue nje mpaka kijito cha Kidroni.
17 Basi wakaanza kutakasa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, hata siku ya nane ya mwezi wakafika katika ukumbi wa Bwana; wakaitakasa nyumba ya Bwana katika muda wa siku nane; wakamaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza.
18 Wakaingia ndani kwa Hezekia mfalme, wakasema, Tumeisafisha nyumba yote ya Bwana, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na vyombo vyake vyote, na meza ya mikate ya wonyesho, pamoja na vyombo vyake vyote.
19 Tena vyombo vyote alivyovitupa mfalme Ahazi alipotawala, hapo alipoasi, tumevitengeza na kuvitakasa; navyo, tazama, vipo mbele ya madhabahu ya Bwana.
20 Ndipo Hezekia mfalme akaamka mapema, akakusanya wakuu wa mji, akapanda nyumbani kwa Bwana.
21 Wakaleta ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, na wana-kondoo saba, na mabeberu saba, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, na kwa ajili ya patakatifu, na kwa ajili ya Yuda. Akaamuru makuhani, wana wa Haruni, wawatoe madhabahuni pa Bwana.
22 Basi wakawachinja ng'ombe, na makuhani wakaipokea damu, wakainyunyiza madhabahuni; wakawachinja kondoo waume, na kuinyunyiza damu madhabahuni; wakawachinja na wana-kondoo, na kuinyunyiza damu madhabahuni.
23 Wakawaleta karibu mabeberu wa sadaka ya dhambi mbele ya mfalme na kusanyiko; wakawawekea mikono yao;
24 na makuhani wakawachinja, wakaitoa damu yao kuwa sadaka ya dhambi madhabahuni, ili kuwafanyia Israeli wote upatanisho; maana mfalme aliamuru Israeli wote wafanyiwe sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya dhambi.
25 Akawasimamisha Walawi nyumbani mwa Bwana wenye matoazi, wenye vinanda, na wenye vinubi, kama alivyoamuru Daudi, na Gadi mwonaji wa mfalme, na Nathani nabii; kwani Bwana aliamuru hivi kwa manabii wake.
26 Wakasimama Walawi wenye vinanda vya Daudi, na makuhani wenye mapanda.
27 Hezekia akaamuru kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Na wakati ilipoanza sadaka hiyo ya kuteketezwa, ukaanza na huo wimbo wa Bwana, na mapanda, pamoja na vinanda vya Daudi mfalme wa Israeli.
28 Na kusanyiko lote wakaabudu, waimbaji wakaimba, wenye mapanda wakapiga; haya yote yakaendelea hata ilipomalizika sadaka ya kuteketezwa.
29 Hata walipokwisha kutoa sadaka, mfalme, na hao wote waliokuwapo naye, wakasujudia, wakaabudu.
30 Tena Hezekia mfalme na wakuu wakawaamuru Walawi, wamwimbie Bwana sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwa furaha, wakainama vichwa, wakaabudu.
31 Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa Bwana, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukrani nyumbani mwa Bwana. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo ya shukrani; na wote wenye moyo wa ukarimu, wakaleta sadaka za kuteketezwa.
32 Na hesabu ya sadaka hizo za kuteketezwa walizozileta kusanyiko ikawa ng'ombe waume sabini, kondoo waume mia, na wana-kondoo mia mbili; hao wote walikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
33 Na vitu vitakatifu vilikuwa ng'ombe mia sita, na kondoo elfu tatu.
34 Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.
35 Na tena sadaka za kuteketezwa nazo zilikuwa nyingi, pamoja na mafuta ya sadaka za amani, na sadaka za kinywaji kwa kila sadaka ya kuteketezwa. Hivyo ikatengezeka huduma ya nyumba ya Bwana.
36 Akafurahi Hezekia, na watu wote, kwa sababu ya hayo Mungu aliyowatengenezea watu; maana jambo hilo likawa kwa ghafula.
1 Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa Bwana Yerusalemu, ili wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli.
2 Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walifanya shauri kufanya pasaka mwezi wa pili.
3 Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani walikuwa hawajajitakasa wa kutosha, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.
4 Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.
5 Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.
6 Wakaenda matarishi wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7 Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi Bwana, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ushangao, kama mwonavyo.
8 Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa Bwana, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali.
9 Kwa kuwa mkimrudia Bwana, ndugu zenu na watoto wenu watahurumiwa machoni pa hao waliowachukua mateka, nao watairudia nchi hii; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.
10 Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka-cheka, na kuwadhihaki.
11 Ila watu wengine wa Asheri, na wa Manase, na wa Zabuloni walijinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.
12 Tena katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa ukiwapa moyo mmoja, waitimize amri ya mfalme na wakuu kwa neno la Bwana.
13 Basi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.
14 Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.
15 Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa Bwana.
16 Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.
17 Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa Bwana.
18 Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, Bwana mwema na amsamehe kila mtu,
19 aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.
20 Bwana akamsikia Hezekia, akawaponya watu.
21 Nao wana wa Israeli waliohudhuria Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu Bwana siku kwa siku, wakimwimbia Bwana kwa vinanda vyenye sauti kuu.
22 Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa wastadi wa kumtumikia Bwana. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani Bwana, Mungu wa baba zao.
23 Na kusanyiko lote wakafanya shauri kufanya sikukuu siku saba nyingine; wakafanya sikukuu siku saba nyingine kwa furaha.
24 Maana Hezekia, mfalme wa Yuda, aliwatolea kusanyiko matoleo ya ng'ombe elfu, na kondoo elfu saba; na wakuu wakawatolea kusanyiko ng'ombe elfu, na kondoo elfu kumi; tena wakajitakasa makuhani wengi sana.
25 Na kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na kusanyiko lote waliotoka Israeli, na wageni waliotoka katika nchi ya Israeli, nao waliokaa Yuda, wakafurahi.
26 Ikawa furaha kuu katika Yerusalemu; kwa sababu tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hayajakuwako mambo kama hayo huko Yerusalemu.
27 Ndipo wakasimama makuhani Walawi, wakawabariki watu; ikasikiwa sauti yao, sala yao ikafika hata makao yake matakatifu, yaani, mbinguni.
1 Basi hayo yote yalipokwisha, wakatoka Israeli wote waliokuwako waende miji ya Yuda, wakazivunja-vunja nguzo, wakayakata-kata maashera, wakabomoa mahali pa juu na madhabahu katika Yuda yote na Benyamini, katika Efraimu pia na Manase, hata walipokwisha kuviharibu vyote. Ndipo wana wa Israeli wote wakarudi, kila mtu kwa milki yake, mijini kwao.
2 Hezekia akaziweka zamu za makuhani na Walawi kwa zamu zao, kila mtu kwa kadiri ya huduma yake, makuhani na Walawi pia, kwa sadaka za kuteketezwa na kwa sadaka za amani, kutumika, na kushukuru, na kusifu, malangoni mwa matuo ya Bwana.
3 Tena akaweka sehemu ya mfalme ya mali zake kwa sadaka za kuteketezwa, yaani, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na sadaka za kuteketezwa za sabato, na za mwezi mpya, na sikukuu, kama ilivyoandikwa katika torati ya Bwana.
4 Tena akawaamuru watu waliokaa Yerusalemu, watoe sehemu ya makuhani na Walawi, ili hao wajibidiishe katika torati ya Bwana.
5 Mara ilipotangaa amri, wana wa Israeli wakatoa kwa wingi malimbuko ya nafaka, na divai, na mafuta, na asali, na mazao yote ya mashamba; na zaka za vitu vyote wakazileta nyingi.
6 Nao wana wa Israeli na Yuda, waliokaa mijini mwa Yuda, wakaleta pia zaka za ng'ombe na kondoo, na zaka za vitu vilivyowekwa wakfu, alivyowekewa Bwana, Mungu wao, wakaviweka chungu chungu.
7 Katika mwezi wa tatu wakaanza kuweka misingi ya hizo chungu, wakazimaliza katika mwezi wa saba.
8 Hata walipokuja Hezekia na wakuu, na kuziona zile chungu, wakamhimidi Bwana, na watu wake Israeli.
9 Ndipo Hezekia akaulizana na makuhani na Walawi katika habari ya hizo chungu.
10 Azaria kuhani mkuu, wa nyumba ya Sadoki, akamjibu, akasema, Tangu watu walipoanza kuleta matoleo nyumbani kwa Bwana, tumekula na kushiba, na kusaza tele; kwa kuwa Bwana amewabariki watu wake; na kilichosalia ndiyo akiba hii kubwa.
11 Ndipo Hezekia akaamuru kutengeneza vyumba nyumbani mwa Bwana; wakavitengeneza.
12 Wakayaingiza matoleo na zaka na vitu vilivyowekwa wakfu, kwa uaminifu; na juu yake Konania Mlawi alikuwa mkuu, na wa pili ni Shimei nduguye.
13 Na Yehieli, na Azaria, na Nahathi, na Asaheli, na Yerimothi, na Yozabadi, na Elieli, na Ismakia, na Mahathi, na Benaya, walikuwa wasimamizi chini ya mkono wa Konania na Shimei nduguye, kwa amri ya Hezekia mfalme, na Azaria mkuu wa nyumba ya Mungu.
14 Na Kore, mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa mlango wa mashariki, alizisimamia sadaka za hiari za Mungu; ili kugawa matoleo ya Bwana, navyo vitu vilivyokuwa vitakatifu sana.
15 Na chini yake walikuwa Edeni, na Minyamini, na Yeshua, na Shemaya, na Amaria, na Shekania, mijini mwa makuhani, kwa walivyoaminiwa, ili kuwagawia ndugu zao kwa zamu, wakuu na wadogo sawasawa;
16 zaidi ya wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wanaume, wenye miaka mitatu na zaidi, kila mmoja aliyeingia nyumbani mwa Bwana, kama ilivyopasa kazi ya kila siku, kwa huduma zao katika malinzi yao, kwa kadiri ya zamu zao;
17 na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya makuhani kufuata nyumba za baba zao, na Walawi, wenye umri wa miaka ishirini na zaidi, katika malinzi yao, kwa kadiri ya zamu zao;
18 na wale waliohesabiwa kwa nasaba ya wadogo wao wote, wake zao, na wana wao, na binti zao, katika kusanyiko lote; kwani kwa vile walivyoaminiwa, wakajitakasa katika utakatifu;
19 tena kwa ajili ya wana wa Haruni makuhani, waliokuwamo mashambani mwa malisho ya miji yao, mji kwa mji, kulikuwa na watu waliotajwa majina yao, ili kuwagawia sehemu wanaume wote miongoni mwa makuhani, na wote waliohesabiwa kwa nasaba miongoni mwa Walawi.
20 Na hivyo ndivyo alivyofanya Hezekia katika Yuda yote; akatenda yaliyo mema, na ya adili, na uaminifu, mbele za Bwana, Mungu wake.
21 Na katika kila kazi aliyoanza kwa utumishi wa nyumba ya Mungu, na kwa torati, na kwa amri, ili kumtafuta Mungu wake, aliifanya kwa moyo wake wote, akafanikiwa.
1 :Ikawa, baada ya mambo hayo, na uaminifu huo, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akaja, akaingia katika Yuda, akafanya marago juu ya miji yenye maboma, akadhania kwamba ataipata iwe yake.
2 Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,
3 akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.
4 Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?
5 Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.
6 Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,
7 Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;
8 kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo Bwana, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.
9 Na baada ya hayo Senakeribu mfalme wa Ashuru, akatuma watumishi wake waende Yerusalemu, (naye alikuwapo mbele ya Lakishi, na uwezo wake wote pamoja naye,) kwa Hezekia, mfalme wa Yuda, na kwa Yuda wote waliokuwako Yerusalemu, kusema,
10 Senakeribu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Mwatumainia nini hata mkae mkihusuriwa katika Yerusalemu?
11 Siye Hezekia anayewashawishi, mtolewe kufa kwa njaa na kwa kiu, akisema, Bwana, Mungu wetu, atatuokoa na mkono wa mfalme wa Ashuru?
12 Si yeye Hezekia huyo aliyeondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaamuru Yuda na Yerusalemu, akisema, Abuduni mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtafukiza uvumba?
13 Je! Ninyi hamjui mimi na baba zangu tuliyowafanyia watu wote wa nchi? Je! Miungu ya mataifa wa nchi iliweza kuokoa kwa lo lote nchi zao na mkono wangu?
14 Ni yupi miongoni mwa miungu ya mataifa wale walioharibiwa kabisa na baba zangu, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, hata Mungu wenu aweze kuwaokoa ninyi na mkono wangu?
15 Basi sasa asiwadanganye Hezekia, wala asiwashawishi kwa hayo, wala msimwamini; kwa kuwa hapana mungu wa taifa lo lote, wala wa ufalme wo wote, aliyeweza kuwaokoa watu wake na mkono wangu, au na mkono wa baba zangu; sembuse Mungu wenu atawaokoaje ninyi na mkono wangu?
16 Na watumishi wake wakazidi kusema juu ya Bwana Mungu, na juu ya Hezekia, mtumishi wake.
17 Tena akaandika waraka, kumtukana Bwana, Mungu wa Israeli, na kumwambia, akisema, Kama vile miungu ya mataifa wa nchi isivyowaokoa watu wao na mkono wangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hatawaokoa watu wake na mkono wangu.
18 Wakawalilia kwa sauti kuu, kwa lugha ya Kiyahudi, watu wa Yerusalemu waliokuwako ukutani ili kuwaogofisha, na kuwafadhaisha; hata wapate kuutwaa mji.
19 Wakamnenea Mungu wa Yerusalemu, kana kwamba kuitaja miungu ya mataifa wa nchi, iliyo kazi ya mikono ya watu.
20 Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni.
21 Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.
22 Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.
23 Watu wengi walimletea Bwana zawadi huko Yerusalemu, na vitu vya thamani kwa Hezekia, mfalme wa Yuda; hata yeye akatukuka tangu wakati ule machoni pa mataifa yote.
24 Katika siku hizo Hezekia akaugua akawa katika hatari ya kufa; akamwomba Bwana; naye akasema naye, akampa ishara.
25 Walakini kadiri alivyofadhiliwa Hezekia hakumrudishia vivyo; kwa kuwa moyo wake ulitukuka; kwa hiyo ikawako hasira juu yake, na juu ya Yuda na Yerusalemu.
26 Hata hivyo Hezekia akajinyenyekeza kwa ajili ya huku kutukuka kwa moyo wake, yeye na wenyeji wa Yerusalemu, hata haikuwajia hasira ya Bwana siku za Hezekia.
27 Naye Hezekia akawa na mali nyingi mno na heshima; akajifanyizia hazina za fedha, na za dhahabu, na za vito, na za manukato, na za ngao, na za namna zote za vyombo vya thamani;
28 ghala pia za mazao ya nafaka na mvinyo na mafuta; na malisho ya wanyama wa namna zote, na makundi mazizini.
29 Tena akajifanyizia miji, na mali za kondoo na ng'ombe kwa wingi; maana Mungu alimtajirisha sana sana.
30 Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote.
31 Walakini kwa habari ya wajumbe wa wakuu wa Babeli, waliotuma kwake kuuliza ajabu iliyofanywa katika nchi, Mungu akamwacha, ili amjaribu, ili kwamba ayajue yote yaliyokuwamo moyoni mwake.
32 Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na matendo yake mema, tazama, yameandikwa katika maono ya Isaya nabii, mwana wa Amozi, katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
33 Hezekia akalala na babaze, wakamzika mahali pa kupandia makaburi ya wana wa Daudi; nao Yuda wote na wenyeji wa Yerusalemu wakamfanyia heshima alipokufa. Na Manase mwanawe akatawala mahali pake.
1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka hamsini na mitano.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo yote ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopabomoa Hezekia babaye; akazisimamisha madhabahu za mabaali, akafanya na sanamu za maashera, akaabudu jeshi lote la mbinguni, na kulitumikia.
4 Akajenga madhabahu katika nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu litakuwako jina langu milele.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika nyua mbili za nyumba ya Bwana.
6 Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.
7 Akaiweka sanamu ya kuchonga aliyoifanya, katika nyumba ya Mungu ambayo Mungu alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;
8 wala sitawaondoshea miguu tena Israeli katika nchi niliyowaagizia baba zenu; wakiangalia tu kutenda yote niliyowaamuru, yaani, torati yote, na sheria, na maagizo, niliyowaamuru kwa mkono wa Musa.
9 Basi Manase akawakosesha Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, hata wakazidi kufanya mabaya kuliko mataifa, aliowaharibu Bwana mbele ya wana wa Israeli.
10 Naye Bwana akasema na Manase, na watu wake; wala wasiangalie.
11 Kwa hiyo Bwana akaleta juu yao maakida wa jeshi la mfalme wa Ashuru, waliomkamata Manase kwa minyororo, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli.
12 Hata alipokuwa katika taabu, akamsihi Bwana, Mungu wake, akajinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.
13 Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akajua ya kwamba Bwana ndiye Mungu.
14 Hata baada ya hayo akaujengea mji wa Daudi ukuta wa nje, upande wa magharibi wa Gihoni, bondeni, hata kufika maingilio ya lango la samaki; akauzungusha Ofeli, akauinua juu sana; akaweka maakida mashujaa katika miji yote ya Yuda yenye maboma.
15 Akaiondoa miungu migeni, na hiyo sanamu nyumbani mwa Bwana, na madhabahu zote alizozijenga katika mlima wa nyumba ya Bwana, na Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.
16 Akaijenga madhabahu ya Bwana, akatoa juu yake dhabihu za sadaka za amani, na za shukrani, akawaamuru Yuda wamtumikie Bwana, Mungu wa Israeli.
17 Lakini watu wakaendelea kutoa dhabihu katika mahali pa juu, ila wakamtolea Bwana, Mungu wao tu.
18 Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na maombi yake kwa Mungu wake, na maneno ya waonaji walionena naye kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, tazama, yameandikwa kati ya mambo ya wafalme wa Israeli.
19 Sala yake pia, na jinsi Mungu alivyomtakabali, na dhambi yake yote, na kosa lake, na mahali alipopajenga mahali pa juu, na kupasimamishia maashera na sanamu za kuchonga, kabla ya kujinyenyekeza; tazama, hayo yameandikwa katika tarehe ya Hozai.
20 Basi Manase akalala na babaze, wakamzika nyumbani mwake; na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
21 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka miwili.
22 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kama alivyofanya Manase babaye; Amoni akazitolea dhabihu sanamu zote alizozifanya Manase babaye, akazitumikia.
23 Wala hakujinyenyekeza mbele za Bwana, kama Manase babaye alivyojinyenyekeza; lakini huyo Amoni akaongeza makosa juu ya makosa.
24 Wakamfanyia fitina watumishi wake, wakamwua katika nyumba yake mwenyewe.
25 Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliomfanyia fitina mfalme Amoni; watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme badala yake.
1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto.
3 Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akali mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa maashera, na sanamu za kuchora, nazo za kusubu.
4 Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikata-kata; na maashera, na sanamu za kuchonga, nazo za kusubu, akazivunja-vunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu.
5 Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu.
6 Na katika miji ya Manase, na Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote.
7 Akazibomoa madhabahu, akaponda-ponda maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikata-kata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.
8 Hata katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake, alipokwisha kuisafisha nchi, na nyumba, akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, na Maaseya, akida wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, mwandishi wa tarehe, waitengeneze nyumba ya Bwana, Mungu wake.
9 Wakamjia Hilkia kuhani mkuu, wakampa fedha, iliyoletwa nyumbani mwa Mungu, waliyoikusanya Walawi, wangoje mlango, mikononi mwa Manase na Efraimu, na mabaki yote ya Israeli, na Yuda yote na Benyamini, na wenyeji wa Yerusalemu.
10 Wakaitia mikononi mwa watenda kazi walioisimamia nyumba ya Bwana; na hao mafundi waliotenda kazi nyumbani mwa Bwana wakaitoa kwa kuitengeneza na kuifanya upya nyumba;
11 wakawapa maseremala na waashi, ili wanunue mawe ya kuchonga, na miti ya kuungia, na kuifanyiza boriti kwa nyumba zile walizoziharibu wafalme wa Yuda.
12 Nao watu wakatenda kazi kwa uaminifu; na wasimamizi wao walikuwa Yahathi na Obadia, Walawi, wa wana wa Merari; na Zekaria na Meshulamu, wa wana wa Wakohathi, ili kuihimiza kazi; na wengine katika Walawi, wote waliokuwa wastadi wa kupiga vinanda.
13 Tena walikuwa juu ya wachukuzi wa mizigo, wakawahimiza wote waliotenda kazi ya huduma yo yote; na miongoni mwa Walawi kulikuwa na waandishi, na wasimamizi, na mabawabu.
14 Nao walipotoa ile fedha iliyoletwa nyumbani mwa Bwana, Hilkia kuhani akakiona kitabu cha torati ya Bwana iliyotolewa kwa mkono wa Musa.
15 Akajibu Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, Kitabu cha torati nimekiona nyumbani mwa Bwana. Hilkia akampa Shafani kile kitabu.
16 Shafani akampelekea mfalme hicho kitabu, tena akampasha mfalme habari, akisema, Yote waliyokabidhiwa watumishi wako, wayafanya.
17 Nao wameimimina fedha iliyoonekana nyumbani mwa Bwana, nayo wameitia mikononi mwa wasimamizi, na mikononi mwa watenda kazi.
18 Shafani mwandishi akamweleza mfalme, akisema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akasoma ndani yake mbele ya mfalme.
19 Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya torati, aliyararua mavazi yake.
20 Mfalme akawaamuru Hilkia, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Abdoni, mwana wa Mika, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme, kusema,
21 Nendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa hao waliosalia wa Israeli na wa Yuda, katika habari za maneno ya kitabu kilichoonekana; maana ghadhabu ya Bwana ni nyingi iliyomwagika juu yetu, kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la Bwana, kutenda sawasawa na yote yaliyoandikwa kitabuni humo.
22 Basi Hilkia, na hao waliotumwa na mfalme, wakamwendea Hulda nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tohathi, mwana wa Hasra, mtunza mavazi; (naye alikuwa akikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili); wakasema naye kama hayo.
23 Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,
24 Bwana asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda;
25 kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike.
26 Lakini mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza Bwana, mtamwambia hivi, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kwa habari ya maneno uliyoyasikia,
27 kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema Bwana.
28 Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari.
29 Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.
30 Akapanda mfalme nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, na makuhani na Walawi, na watu wote, wakubwa kwa wadogo; naye akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana nyumbani mwa Bwana.
31 Akasimama mfalme mahali pake, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuzishika amri zake, na shuhuda zake, na sheria zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, kuyatenda maneno ya agano yaliyoandikwa kitabuni humo.
32 Akawafanya wote walioonekana katika Yerusalemu na Benyamini walikubali. Na wenyeji wa Yerusalemu wakafanya sawasawa na agano la Mungu, Mungu wa baba zao.
33 Naye Yosia akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi zote zilizokuwa milki ya wana wa Israeli, akawafanya wote walioonekana katika Israeli kutumika, naam, wamtumikie Bwana, Mungu wao. Siku zake zote hawakuacha kumfuata Bwana, Mungu wa baba zao.
1 Naye Yosia akamfanyia Bwana pasaka huko Yerusalemu; wakachinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.
2 Akawasimamisha makuhani katika malinzi yao, akawatia moyo kufanya utumishi wa nyumba ya Bwana.
3 Akawaambia Walawi, waliowafundisha Israeli wote, waliotakasika kwa Bwana, Wekeni sanduku takatifu katika nyumba aliyoijenga Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli; hamtakuwa tena na mzigo mabegani; sasa mtumikieni Bwana, Mungu wenu, na watu wake Israeli.
4 Mkajiweke tayari kwa kadiri ya nyumba za baba zenu, kwa zamu zenu, kama alivyoandika Daudi mfalme wa Israeli, na kama alivyoandika Sulemani mwanawe.
5 Mkasimame katika patakatifu, kama walivyogawanyika ndugu zenu, wana wa watu, kufuata nyumba za mababa, kadiri ya mgawanyiko wa kila nyumba ya baba, ya Walawi.
6 Mkachinje pasaka, mkajitakase, mkawatengenezee ndugu zenu, kutenda sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Musa.
7 Tena Yosia akawapa wana wa watu, matoleo ya makundi, wana-kondoo na wana-mbuzi, yote yawe kwa ajili ya matoleo ya pasaka, wote waliokuwako, wakipata thelathini elfu, na ng'ombe elfu tatu; hao walitoka katika mali za mfalme.
8 Na wakuu wake wakawapa watu, na makuhani na Walawi matoleo ya hiari. Hilkia na wana na Yehieli, wakubwa wa nyumba ya Mungu, wakawapa makuhani, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu mbili na mia sita, na ng'ombe mia tatu.
9 Konania naye, na Shemaya, na Nethaneli, ndugu zake, na Hashabia, na Yeieli, na Yozabadi, wakuu wa Walawi, wakawapa Walawi, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu tano, na ng'ombe mia tano.
10 Hivyo huduma ikatengenezwa, wakasimama makuhani mahali pao, na Walawi kwa zamu zao, kama alivyoamuru mfalme.
11 Wakachinja pasaka, nao makuhani wakamimina damu waliyopokea mikononi mwao, Walawi wakachuna.
12 Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape wana wa watu, kama walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, ili wamtolee Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo.
13 Wakaioka moto pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote.
14 Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni.
15 Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.
16 Basi huduma yote ya Bwana ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana, kama alivyoamuru mfalme Yosia.
17 Wana wa Israeli waliokuwapo wakafanya pasaka wakati ule, na sikukuu ya mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
18 Wala haikufanyika pasaka kama ile katika Israeli tangu siku za nabii Samweli; wala wafalme wa Israeli hawakufanya hata mmoja wao pasaka kama ile Yosia aliyoifanya, pamoja na makuhani, na Walawi, na Yuda wote na Israeli waliokuwapo, na wenyeji wa Yerusalemu.
19 Katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Yosia ikafanyika pasaka hiyo.
20 Baada ya hayo yote, alipokwisha Yosia kulitengeneza hekalu, Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana Karkemishi karibu na Frati; naye Yosia akatoka juu yake.
21 Lakini yeye akatuma kwake wajumbe, kusema, Ni nini niliyo nayo mimi na wewe, Ee mfalme wa Yuda? Sikuja juu yako leo, lakini juu ya nyumba niliyo na vita nayo; naye Mungu ameniamuru nifanye haraka; acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu.
22 Walakini Yosia hakukubali kumgeuzia uso mbali, akajibadilisha apate kupigana naye, asiyasikilize maneno ya Neko, yaliyotoka kinywani kwa Mungu, akaja kupigana bondeni mwa Megido.
23 Nao wapiga upinde wakampiga Yosia; naye mfalme akawaambia watumishi wake, Niondoeni; kwani nimejeruhiwa sana.
24 Basi watumishi wake wakamtoa garini, wakamtia katika gari la pili alilokuwa nalo, wakamleta Yerusalemu; naye akafa, akazikwa makaburini mwa babaze. Wakamlilia Yosia Yuda wote na Yerusalemu.
25 Naye Yeremia akamlilia Yosia; na waimbaji wote waume kwa wake wakamtaja Yosia katika maombolezo yao, hata leo; hata wakayafanya kuwa ada kwa Israeli; nayo, tazama, yameandikwa katika maombolezo.
26 Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na matendo yake mema, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya Bwana,
27 na mambo yake, ya kwanza na ya mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
1 Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme katika Yerusalemu badala ya babaye.
2 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu.
3 Naye mfalme wa Misri akamwondoa katika Yerusalemu, akaitoza nchi talanta mia za fedha, na talanta moja ya dhahabu.
4 Mfalme wa Misri akamtawaza Eliakimu nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu. Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye, akamchukua mpaka Misri.
5 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake.
6 Juu yake akakwea Nebukadreza,
7 Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya Bwana mpaka Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.
8 Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na machukizo yake aliyoyafanya, nayo yaliyoonekana kwake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda; na Yekonia
9 Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
10 Mwaka ulipokwisha, Nebukadreza akatuma wajumbe, akamchukua mpaka Babeli; pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Bwana; akamtawaza Sedekia nduguye awe mfalme juu ya Yuda na Yerusalemu.
11 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;
12 akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake; wala hakujinyenyekesha mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Bwana.
13 Tena akamwasi mfalme Nebukadreza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini akajifanyia shingo ngumu, akajitia moyo nguvu asimgeukie Bwana, Mungu wa Israeli.
14 Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.
15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;
16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.
18 Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.
19 Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani.
20 Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;
21 ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini.
22 Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,
23 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.