Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 41, 42, 43, 44, 45, 46, 47, 48, 49, 50, 51, 52, 53, 54, 55, 56, 57, 58, 59, 60, 61, 62, 63, 64, 65, 66, 67, 68, 69, 70, 71, 72, 73, 74, 75, 76, 77, 78, 79, 80, 81, 82, 83, 84, 85, 86, 87, 88, 89, 90, 91, 92, 93, 94, 95, 96, 97, 98, 99, 100, 101, 102, 103, 104, 105, 106, 107, 108, 109, 110, 111, 112, 113, 114, 115, 116, 117, 118, 119, 120, 121, 122, 123, 124, 125, 126, 127, 128, 129, 130, 131, 132, 133, 134, 135, 136, 137, 138, 139, 140, 141, 142, 143, 144, 145, 146, 147, 148, 149, 150
1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.
4 Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5 Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.
6 Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.
1 Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili?
2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.
3 Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.
4 Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka.
5 Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.
6 Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
7 Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
8 Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.
10 Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
11 Mtumikieni Bwana kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka.
12 Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia.
1 Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia,
2 Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu.
3 Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
4 Kwa sauti yangu namwita Bwana Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu.
5 Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
6 Sitayaogopa makumi elfu ya watu, Waliojipanga juu yangu pande zote.
7 Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu wote; Umewavunja meno wasio haki.
8 Wokovu una Bwana; Baraka yako na iwe juu ya watu wako.
1 Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo; Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; Unifadhili na kuisikia sala yangu.
2 Enyi wanadamu, hata lini utukufu wangu utafedheheka? Je! Mtapenda ubatili na kutafuta uongo?
3 Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo.
4 Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.
5 Toeni dhabihu za haki, Na kumtumaini Bwana.
6 Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
7 Umenitia furaha moyoni mwangu, Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai.
8 Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.
1 Ee Bwana, uyasikilize maneno yangu, Ukuangalie kutafakari kwangu.
2 Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye.
3 Bwana, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia.
4 Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya; Mtu mwovu hatakaa kwako;
5 Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako; Unawachukia wote watendao ubatili.
6 Utawaharibu wasemao uongo; Bwana humzira mwuaji na mwenye hila
7 Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu.
8 Bwana, uniongoze kwa haki yako, Kwa sababu yao wanaoniotea. Uisawazishe njia yako mbele ya uso wangu,
9 Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza.
10 Wewe, Mungu, uwapatilize, Na waanguke kwa mashauri yao. Uwatoe nje kwa ajili ya wingi wa makosa yao, Kwa maana wamekuasi Wewe.
11 Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia.
12 Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana, utamzungushia radhi kama ngao.
1 Bwana, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako.
2 Bwana, unifadhili, maana ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika.
3 Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini?
4 Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
5 Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?
6 Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu.
7 Jicho langu limeharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi.
8 Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa Bwana ameisikia sauti ya kilio changu.
9 Bwana ameisikia dua yangu; Bwana atayatakabali maombi yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.
1 Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
2 Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.
3 Bwana, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya, Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,
4 Ikiwa nimemlipa mabaya Yeye aliyekaa kwangu salama; (Hasha! Nimemponya yeye Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)
5 Basi adui na anifuatie, Na kuikamata nafsi yangu; Naam, aukanyage uzima wangu, Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.
6 Bwana uondoke kwa hasira yako; Ujiinue juu ya jeuri ya watesi wangu; Uamke kwa ajili yangu; Umeamuru hukumu.
7 Kusanyiko la mataifa na likuzunguke, Na juu yake uketi utawale.
8 Bwana atawaamua mataifa, Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao.
9 Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki.
10 Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo.
11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.
12 Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;
13 Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto.
14 Tazama, huyu ana utungu wa uovu, Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.
15 Amechimba shimo, amelichimba chini sana, Akatumbukia katika handaki aliyoifanya!
16 Madhara yake yatamrejea kichwani pake, Na dhuluma yake itamshukia utosini.
17 Nitamshukuru Bwana kwa kadiri ya haki yake; Nitaliimbia jina la Bwana aliye juu.
1 Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;
2 Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
4 Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie?
5 Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima;
6 Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
7 Kondoo, na ng'ombe wote pia; Naam, na wanyama wa kondeni;
8 Ndege wa angani, na samaki wa baharini; Na kila kipitacho njia za baharini.
9 Wewe, MUNGU, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
1 Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
2 Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
3 Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako.
4 Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki.
5 Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele;
6 Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele. Nayo miji yao uliing'oa; Hata kumbukumbu lao limepotea.
7 Bali Bwana atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
8 Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.
9 Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.
10 Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, Bwana hukuwaacha wakutafutao.
11 Mwimbieni Bwana akaaye Sayuni, Yatangazeni kati ya watu matendo yake.
12 Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge.
13 Wewe, Bwana, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti,
14 Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako.
15 Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.
16 Bwana amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake.
17 Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.
18 Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
19 Bwana, usimame, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako.
20 Bwana, uwawekee kitisho, Mataifa na wajijue kuwa ni binadamu.
1 Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?
2 Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
3 Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
4 Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;
5 Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.
6 Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.
7 Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
8 Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.
9 Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.
10 Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.
11 Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.
12 Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.
13 Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?
14 Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.
15 Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.
16 Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake.
17 Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako.
18 Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.
1 Bwana ndiye niliyemkimbilia. Mbona mnaiambia nafsi yangu, Kimbia kama ndege mlimani kwenu?
2 Maana, tazama, wasio haki wanaupinda uta, Wanaitia mishale yao katika upote, Ili kuwapiga gizani wanyofu wa moyo.
3 Kama misingi ikiharibika, Mwenye haki atafanya nini?
4 Bwana yu katika hekalu lake takatifu. Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni, Macho yake yanaangalia; Kope zake zinawajaribu wanadamu.
5 Bwana humjaribu mwenye haki; Bali nafsi yake humchukia asiye haki, Na mwenye kupenda udhalimu.
6 Awanyeshee wasio haki mitego, Moto na kiberiti na upepo wa hari, Na viwe fungu la kikombe chao.
7 Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki, Wanyofu wa moyo watamwona uso wake.
1 Bwana, uokoe, maana mcha Mungu amekoma, Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
2 Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe, Wenye midomo ya kujipendekeza; Husemezana kwa mioyo ya unafiki;
3 Bwana ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;
4 Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda; Midomo yetu ni yetu wenyewe, Ni nani aliye bwana juu yetu?
5 Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.
6 Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.
7 Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi hiki milele.
8 Wasio haki hutembea pande zote, Ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu.
1 Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?
2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?
3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.
4 Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa.
5 Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.
6 Naam, nimwimbie Bwana, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu.
1 Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.
2 Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.
3 Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.
4 Je! Wote wafanyao maovu hawajui? Walao watu wangu kama walavyo mkate, Hawamwiti Bwana.
5 Hapo ndipo walipoingiwa na hofu nyingi, Maana Mungu yupo pamoja na kizazi cha haki.
6 Mnalitia aibu shauri la mtu mnyonge, Bali Bwana ndiye aliye kimbilio lake.
7 Laiti wokovu wa Israeli utoke katika Sayuni! Bwana awarudishapo wafungwa wa watu wake; Yakobo atashangilia, Israeli atafurahi.
1 Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
2 Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake,
3 Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
4 Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.
5 Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.
1 Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.
2 Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako.
3 Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao.
4 Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.
5 Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu.
6 Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.
7 Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
10 Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
11 Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
1 Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.
2 Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.
3 Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,
4 Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
5 Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.
6 Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.
7 Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.
8 Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
9 Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.
10 Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.
11 Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.
12 Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.
13 Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.
14 Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,
15 Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
1 Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.
4 Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili.
6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.
7 Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu.
8 Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao.
9 Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.
10 Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo.
11 Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni.
12 Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto.
13 Bwana alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto.
14 Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya.
15 Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.
16 Alipeleka kutoka juu akanishika, Na kunitoa katika maji mengi.
17 Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.
18 Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini Bwana alikuwa tegemeo langu.
19 Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
20 Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa.
21 Maana nimezishika njia za Bwana, Wala sikumwasi Mungu wangu.
22 Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo.
23 Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu.
24 Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
25 Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;
26 Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.
27 Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili.
28 Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; Bwana Mungu wangu aniangazia giza langu.
29 Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.
30 Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya Bwana imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia.
31 Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu?
32 Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu.
33 Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.
34 Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.
35 Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kuume umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza.
36 Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza.
37 Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe.
38 Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu.
39 Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia chini yangu walioniondokea.
40 Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali.
41 Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita Bwana lakini hakuwajibu,
42 Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani.
43 Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia.
44 Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea.
45 Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka.
46 Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu;
47 Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu.
48 Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri.
49 Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.
50 Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake,Daudi na mzao wake hata milele.
1 Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
2 Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa.
3 Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani.
4 Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema,
5 Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake.
6 Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hari yake Hakuna kitu kilichositirika.
7 Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.
8 Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.
9 Kicho cha Bwana ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa.
10 Ni za kutamanika kuliko dhahabu, Kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, Kuliko sega la asali.
11 Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi.
12 Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri.
13 Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.
14 Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.
1 Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue.
2 Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni.
3 Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako.
4 Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.
5 Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote.
6 Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.
7 Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.
8 Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.
9 Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.
1 Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako, Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
2 Umempa haja ya moyo wake, Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.
3 Maana umemsogezea baraka za heri, Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
4 Alikuomba uhai, ukampa, Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele.
5 Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako, Heshima na adhama waweka juu yake.
6 Maana umemfanya kuwa baraka za milele, Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako.
7 Kwa kuwa mfalme humtumaini Bwana, Na kwa fadhili zake Aliye juu hataondoshwa.
8 Mkono wako utawapata adui zako wote, Mkono wako wa kuume utawapata wanaokuchukia.
9 Utawafanya kuwa kama tanuru ya moto, Wakati wa ghadhabu yako. Bwana atawameza kwa ghadhabu yake, Na moto utawala.
10 Matunda yao utayaharibu na kuyaondoa katika nchi, Na wazao wao katika wanadamu.
11 Madhali walinuia kukutenda mabaya, Waliwaza hila wasipate kuitimiza.
12 Kwa maana utawafanya kukupa kisogo, Kwa upote wa uta wako ukiwaelekezea mishale.
13 Ee Bwana, utukuzwe kwa nguvu zako, Nasi tutaimba na kuuhimidi uweza wako.
1 Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?
2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha.
3 Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.
4 Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.
5 Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.
6 Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu.
7 Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
8 Husema, Umtegemee Bwana; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.
9 Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu.
10 Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu.
11 Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.
12 Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga;
13 Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.
14 Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.
15 Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti
16 Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua mikono na miguu.
17 Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho.
18 Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.
19 Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.
20 Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa.
21 Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu.
22 Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
23 Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni, Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazao wa Israeli.
24 Maana hakulidharau teso la mteswa, Wala hakuchukizwa nalo; Wala hakumficha uso wake, Bali alipomlilia akamsikia.
25 Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao.
26 Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele.
27 Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
28 Maana ufalme una Bwana, Naye ndiye awatawalaye mataifa.
29 Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
30 Wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, Kwa kizazi kitakachokuja,
31 Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.
1 Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
3 Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
5 Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.
6 Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
1 Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.
2 Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
3 Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
4 Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila.
5 Atapokea baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
6 Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.
8 Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita.
9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.
10 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.
1 Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu,
2 Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
3 Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.
4 Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,
5 Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.
6 Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.
7 Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.
8 Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
9 Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake.
10 Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
11 Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi.
12 Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.
13 Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi.
14 Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.
15 Macho yangu humwelekea Bwana daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.
16 Uniangalie na kunifadhili, Maana mimi ni mkiwa na mteswa.
17 Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa katika dhiki zangu.
18 Utazame teso langu na taabu yangu; Unisamehe dhambi zangu zote.
19 Uwatazame adui zangu, maana ni wengi, Wananichukia kwa machukio ya ukali.
20 Unilinde nafsi yangu na kuniponya, Nisiaibike, maana nakukimbilia Wewe.
21 Ukamilifu na unyofu zinihifadhi, Maana nakungoja Wewe.
22 Ee Mungu, umkomboe Israeli, Katika taabu zake zote.
1 Ee Bwana, unihukumu mimi, Maana nimekwenda kwa ukamilifu wangu, Nami nimemtumaini Bwana bila wasiwasi.
2 Ee Bwana, unijaribu na kunipima; Unisafishe mtima wangu na moyo wangu.
3 Maana fadhili zako zi mbele ya macho yangu, Nami nimekwenda katika kweli yako.
4 Sikuketi pamoja na watu wa ubatili, Wala sitaingia mnamo wanafiki.
5 Nimelichukia kusanyiko la watenda mabaya, Wala sitaketi pamoja na watu waovu.
6 Nitanawa mikono yangu kwa kutokuwa na hatia, Na kuizunguka madhabahu yako, Ee Bwana
7 Ili niitangaze sauti ya kushukuru, Na kuzisimulia kazi zako za ajabu.
8 Bwana, nimependa makao ya nyumba yako, Na mahali pa maskani ya utukufu wako.
9 Usiiondoe nafsi yangu pamoja na wakosaji, Wala uhai wangu pamoja na watu wa damu.
10 Mikononi mwao mna madhara, Na mkono wao wa kuume umejaa rushwa.
11 Ila mimi nitakwenda kwa ukamilifu wangu; Unikomboe, unifanyie fadhili.
12 Mguu wangu umesimama palipo sawa; Katika makusanyiko nitamhimidi Bwana.
1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
2 Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka.
3 Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.
4 Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.
5 Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.
6 Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi Bwana.
7 Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.
8 Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.
9 Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
10 Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake.
11 Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;
12 Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi.
13 Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
14 Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
1 Ee Bwana, nitakuita Wewe, mwamba wangu, Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao shimoni, Ikiwa umeninyamalia.
2 Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu pako mikono yangu.
3 Usinikokote pamoja na wasio haki, Wala pamoja na watenda maovu. Wawaambiao jirani zao maneno ya amani, Lakini mioyoni mwao mna madhara.
4 Uwape sawasawa na vitendo vyao, Na kwa kadiri ya ubaya wa kufanya kwao, Uwape sawasawa na kazi ya mikono yao, Uwalipe stahili zao.
5 Maana hawazifahamu kazi za Bwana, Wala matendo ya mikono yake. Atawavunja wala hatawajenga;
6 Na ahimidiwe Bwana. Maana ameisikia sauti ya dua yangu;
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.
8 Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake.
9 Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.
1 Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
2 Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
3 Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi.
4 Sauti ya Bwana ina nguvu; Sauti ya Bwana ina adhama;
5 Sauti ya Bwana yaivunja mierezi; Naam, Bwana aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;
6 Airusha-rusha kama ndama wa ng'ombe; Lebanoni na Sirioni kama mwana-nyati.
7 Sauti ya Bwana yaipasua miali ya moto;
8 Sauti ya Bwana yalitetemesha jangwa; Bwana alitetemesha jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.
10 Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele.
11 Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
2 Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.
3 Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.
4 Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
5 Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.
6 Nami nilipofanikiwa nalisema, Sitaondoshwa milele.
7 Bwana, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika.
8 Ee Bwana, nalikulilia Wewe, Naam, kwa Bwana naliomba dua.
9 Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yataitangaza kweli yako?
10 Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.
11 Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
12 Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.
1 Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,
2 Unitegee sikio lako, uniokoe hima. Uwe kwangu mwamba wa nguvu, Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.
3 Ndiwe genge langu na ngome yangu; Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.
4 Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri, Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
5 Mikononi mwako naiweka roho yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
6 Nawachukia wao washikao yasiyofaa yenye uongo; Bali mimi namtumaini Bwana.
7 Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako, Kwa kuwa umeyaona mateso yangu. Umeijua nafsi yangu taabuni,
8 Wala hukunitia mikononi mwa adui; Miguu yangu umeisimamisha panapo nafasi.
9 Ee Bwana, unifadhili, maana ni katika dhiki, Jicho langu limenyauka kwa masumbufu, Naam, mwili wangu na nafsi yangu.
10 Maana maisha yangu yamekoma kwa huzuni, Na miaka yangu kwa kuugua. Nguvu zangu zinatetemeka kwa uovu wangu, Na mifupa yangu imekauka.
11 Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia.
12 Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
13 Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu.
14 Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
15 Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.
16 Umwangaze mtumishi wako Kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
17 Ee Bwana, nisiaibishwe, maana nimekuita; Waaibishwe wasio haki, wanyamaze kuzimuni.
18 Midomo ya uongo iwe na ububu, Imneneayo mwenye haki maneno ya kiburi, Kwa majivuno na dharau.
19 Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao; Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!
20 Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako; Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.
21 Bwana ahimidiwe; kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.
22 Nami nalisema kwa haraka yangu, Nimekatiliwa mbali na macho yako; Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia.
23 Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake. Bwana huwahifadhi waaminifu, Humlipa atendaye kiburi malipo tele.
24 Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana.
1 Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.
2 Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.
3 Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu mchana kutwa.
4 Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.
5 Nalikujulisha dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu. Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana, Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
6 Kwa hiyo kila mtu mtauwa Akuombe wakati unapopatikana. Hakika maji makuu yafurikapo, Hayatamfikia yeye.
7 Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, Utanizungusha nyimbo za wokovu.
8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.
9 Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.
10 Naye mtu mwovu ana mapigo mengi, Bali amtumainiye Bwana fadhili zitamzunguka.
11 Mfurahieni Bwana; Shangilieni, enyi wenye haki Pigeni vigelegele vya furaha; Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.
1 Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
2 Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
3 Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
4 Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
5 Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.
6 Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
7 Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala.
8 Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.
9 Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.
10 Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu.
11 Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
12 Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
13 Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia.
14 Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani.
15 yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote.
16 Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu.
17 Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.
18 Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.
19 Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.
20 Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
21 Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.
22 Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
1 Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
2 Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
4 Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.
5 Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.
6 Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.
7 Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
8 Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
9 Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
10 Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
11 Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
12 Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?
13 Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.
14 Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.
15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.
16 Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
17 Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.
18 Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.
19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.
20 Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.
21 Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
22 Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
1 Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.
2 Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.
3 Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.
4 Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.
5 Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.
6 Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.
7 Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.
8 Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.
9 Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.
10 Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.
11 Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12 Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa.
13 Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.
14 Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye.
15 Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi.
16 Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno.
17 Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba.
18 Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
19 Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e.
20 Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila.
21 Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona.
22 Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami.
23 Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu.
24 Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize.
25 Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza.
26 Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.
27 Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.
28 Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.
1 Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.
2 Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.
3 Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema.
4 Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii.
5 Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni, Uaminifu wako hata mawinguni.
6 Haki yako ni kama milima ya Mungu, Hukumu zako ni vilindi vikuu, Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.
7 Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
8 Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako, Nawe utawanywesha mto wa furaha zako.
9 Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru.
10 Uwadumishie wakujuao fadhili zako, Na wanyofu wa moyo uaminifu wako.
11 Mguu wa kiburi usinikaribie, Wala mkono wa wasio haki usinifukuze.
12 Huko ndiko walikoanguka wafanyao maovu; Wameangushwa chini wasiweze kusimama.
1 Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili.
2 Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka.
3 Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
4 Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.
5 Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.
6 Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri.
7 Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila.
8 Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, Usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.
9 Maana watenda mabaya wataharibiwa, Bali wamngojao Bwana ndio watakaoirithi nchi.
10 Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.
11 Bali wenye upole watairithi nchi, Watajifurahisha kwa wingi wa amani.
12 Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake.
13 Bwana atamcheka, Maana ameona kwamba siku yake inakuja.
14 Wasio haki wamefuta upanga na kupinda uta, Wamwangushe chini maskini na mhitaji, Na kuwaua wenye mwenendo wa unyofu.
15 Upanga wao utaingia mioyoni mwao wenyewe, Na nyuta zao zitavunjika.
16 Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi.
17 Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali Bwana huwategemeza wenye haki.
18 Bwana anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele.
19 Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba.
20 Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao Bwana watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka.
21 Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.
22 Maana waliobarikiwa na yeye watairithi nchi, Nao waliolaaniwa na yeye wataharibiwa.
23 Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake.
24 Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza.
25 Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.
26 Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.
27 Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele.
28 Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.
29 Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele.
30 Kinywa chake mwenye haki hunena hekima, Na ulimi wake husema hukumu.
31 Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.
32 Mtu asiye haki humvizia mwenye haki, Na kutafuta jinsi ya kumfisha.
33 Bwana hatamwacha mkononi mwake, Wala hatamlaumu atakapohukumiwa.
34 Wewe umngoje Bwana, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona.
35 Nimemwona mtu asiye haki mkali sana, Akijieneza kama mwerezi wa Lebanoni.
36 Nikapita na kumbe! Hayuko, Nikamtafuta wala hakuonekana.
37 Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.
38 Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa.
39 Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
40 Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
1 Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako.
2 Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata.
3 Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu.
4 Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno.
5 Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu.
6 Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika.
7 Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.
8 Nimedhoofika na kuchubuka sana, Nimeugua kwa fadhaa ya moyo wangu.
9 Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako, Kuugua kwangu hakukusitirika kwako.
10 Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.
11 Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali.
12 Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa.
13 Lakini kama kiziwi sisikii, Nami ni kama bubu asiyefumbua kinywa chake.
14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia, Ambaye hamna hoja kinywani mwake.
15 Kwa kuwa nakungoja Wewe, Bwana, Wewe utajibu, Ee Bwana, Mungu wangu.
16 Maana nalisema, Wasije wakanifurahia; Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu.
17 Kwa maana mimi ni karibu na kusita, Na maumivu yangu yako mbele yangu daima.
18 Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu.
19 Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi.
20 Naam, wakilipa mabaya kwa mema, Huwa adui zangu kwa kuwa nalifuata lililo jema.
21 Wewe, Bwana, usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami.
22 Ufanye haraka kunisaidia, Ee Bwana, wokovu wangu.
1 Nalisema, Nitazitunza njia zangu Nisije nikakosa kwa ulimi wangu; Nitajitia lijamu kinywani, Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu.
2 Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya, Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.
3 Moyo wangu ukawa moto ndani yangu, Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka; Nalisema kwa ulimi wangu,
4 Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu.
5 Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri; Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.
6 Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.
7 Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana? Matumaini yangu ni kwako.
8 Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.
9 Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.
10 Uniondolee pigo lako; Kwa uadui wa mkono wako nimeangamia.
11 Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake, Watowesha uzuri wake kama nondo. Kila mwanadamu ni ubatili.
12 Ee Bwana, usikie maombi yangu, Utege sikio lako niliapo, Usiyanyamalie machozi yangu. Kwa maana mimi ni mgeni wako, Msafiri kama baba zangu wote.
13 Uniachilie nikunjuke uso, Kabla sijaondoka nisiwepo tena.
1 Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.
2 Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.
3 Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana
4 Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.
5 Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.
6 Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
7 Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)
8 Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
9 Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.
10 Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.
11 Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.
12 Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha.
13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.
14 Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.
15 Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!
16 Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana.
17 Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.
1 Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu.
2 Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.
3 Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.
4 Nami nalisema, Bwana, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.
5 Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea?
6 Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena.
7 Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.
8 Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena.
9 Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.
10 Lakini Wewe, Bwana, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa.
11 Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda.
12 Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele.
13 Na atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.
1 Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.
2 Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?
3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako.
4 Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.
5 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
6 Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.
7 Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako, Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.
8 Mchana Bwana ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami, Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.
9 Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?
10 Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?
11 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
1 Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, Uniokoe na mtu wa hila asiye haki.
2 Kwa kuwa Wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu; kwa nini umenitupa? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?
3 Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze, Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.
4 Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu.
5 Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.
1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.
2 Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao.
3 Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia.
4 Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.
5 Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.
6 Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.
7 Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.
8 Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.
9 Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu.
10 Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.
11 Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.
12 Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.
13 Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
14 Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.
15 Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika,
16 Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.
17 Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako.
18 Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako.
19 Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.
20 Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;
21 Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.
22 Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa.
23 Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa.
24 Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?
25 Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.
26 Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.
1 Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.
2 Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.
3 Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako.
4 Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha.
5 Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme.
6 Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.
7 Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako.
8 Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.
9 Binti za wafalme wamo Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki. Mkono wako wa kuume amesimama malkia Amevaa dhahabu ya Ofiri.
10 Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.
11 Naye mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.
12 Na binti Tiro analeta kipawa chake, Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.
13 Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu, Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.
14 Atapelekwa kwa mfalme Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri. Wanawali wenzake wanaomfuata, Watapelekwa kwako.
15 Watapelekwa kwa furaha na shangwe, Na kuingia katika nyumba ya mfalme.
16 Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.
17 Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele.
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2 Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
3 Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.
4 Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
5 Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
6 Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka.
7 Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
8 Njoni myatazame matendo ya Bwana, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
9 Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.
10 Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi.
11 Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
1 Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.
2 Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
3 Atawatiisha watu wa nchi chini yetu, Na mataifa chini ya miguu yetu.
4 Atatuchagulia urithi wetu, Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda.
5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu.
6 Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni.
7 Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili.
8 Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.
9 Wakuu wa watu wamekusanyika, Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu. Maana ngao za dunia zina Mungu, Ametukuka sana.
1 Bwana ndiye aliye mkuu, Na mwenye kusifiwa sana. Katika mji wa Mungu wetu, Katika mlima wake mtakatifu.
2 Kuinuka kwake ni mzuri sana, Ni furaha ya dunia yote. Mlima Sayuni pande za kaskazini, Mji wa Mfalme mkuu.
3 Mungu katika majumba yake Amejijulisha kuwa ngome.
4 Maana, tazama, wafalme walikusanyika; Walipita wote pamoja.
5 Waliona, mara wakashangaa; Wakafadhaika na kukimbia.
6 Papo hapo tetemeko liliwashika, Utungu kama wa mwanamke azaaye.
7 Kwa upepo wa mashariki Wavunja jahazi za Tarshishi.
8 Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona, Katika mji wa Bwana wa majeshi. Mji wa Mungu wetu; Mungu ataufanya imara hata milele.
9 Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu, Katikati ya hekalu lako.
10 Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu, Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki;
11 Na ufurahi mlima Sayuni. Binti za Yuda na washangilie Kwa sababu ya hukumu zako.
12 Tembeeni katika Sayuni, Uzungukeni mji, Ihesabuni minara yake,
13 Tieni moyoni boma zake, Yafikirini majumba yake, Mpate kuwaambia kizazi kitakachokuja.
14 Kwa maana ndivyo alivyo MUNGU, Mungu wetu. Milele na milele Yeye ndiye atakayetuongoza.
1 Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.
2 Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja.
3 Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara.
4 Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi
5 Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
6 Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao;
7 Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,
8 (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;)
9 ili aishi sikuzote asilione kaburi.
10 Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao.
11 Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Hao waliotaja mashamba yao Kwa majina yao wenyewe.
12 Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao.
13 Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao.
14 Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu.
15 Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha.
16 Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
18 Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema,
19 Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele.
20 Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.
1 Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake.
2 Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika.
3 Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote.
4 Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake.
5 Nikusanyieni wacha Mungu wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
6 Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
7 Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena, Mimi nitakushuhudia, Israeli; Mimi ndimi niliye MUNGU, Mungu wako.
8 Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
9 Sitatwaa ng'ombe katika nyumba yako, Wala beberu katika mazizi yako.
10 Maana kila hayawani ni wangu, Na makundi juu ya milima elfu.
11 Nawajua ndege wote wa milima, Na wanyama wote wa mashamba ni wangu
12 Kama ningekuwa na njaa singekuambia, Maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.
13 Je! Nile nyama ya mafahali! Au ninywe damu ya mbuzi!
14 Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
15 Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
16 Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.
19 Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.
20 Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.
21 Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.
22 Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.
23 Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
1 Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu.
2 Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.
3 Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
4 Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.
5 Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
6 Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,
7 Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji
8 Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi.
9 Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote.
10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
11 Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
12 Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
13 Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.
14 Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako.
15 Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
16 Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
17 Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.
18 Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu.
19 Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako.
1 Kwa nini kujisifia uovu, Ewe jabari? Wema wa Mungu upo sikuzote.
2 Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila
3 Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli.
4 Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila.
5 Lakini Mungu atakuharibu hata milele; Atakuondolea mbali; Atakunyakua hemani mwako; Atakung'oa katika nchi ya walio hai.
6 Nao wenye haki wataona; Wataingiwa na hofu na kumcheka;
7 Kumbe! Huyu ndiye mtu yule, Asiyemfanya Mungu kuwa nguvu zake. Aliutumainia wingi wa mali zake, Na kujifanya hodari kwa madhara yake.
8 Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.
9 Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha Mungu wako.
1 Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye mema.
2 Toka mbinguni MUNGU aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.
3 Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.
4 Je! Wafanyao maovu hawajui? Walao watu wangu kama walavyo mkate, Hawakumwita MUNGU.
5 Hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hofu, Maana Mungu ameitawanya mifupa yake aliyekuhusuru. Umewatia aibu, Kwa sababu MUNGU amewadharau.
6 Laiti wokovu wa Israeli utoke katika Sayuni! MUNGU awarudishapo wafungwa wa watu wake; Yakobo atashangilia, Israeli atafurahi.
1 Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe, Na kwa uweza wako unifanyie hukumu.
2 Ee Mungu, uyasikie maombi yangu, Uyasikilize maneno ya kinywa changu.
3 Kwa maana wageni wamenishambulia; Watu watishao wananitafuta nafsi yangu; Hawakumweka Mungu mbele yao.
4 Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu.
5 Atawarudishia adui zangu ubaya wao; Uwaangamize kwa uaminifu wako.
6 Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema.
7 Kwa kuwa limeniokoa na kila taabu; Na jicho langu limeridhika Kwa kuwatazama adui zangu.
1 Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.
2 Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga nikilalama na kuugua.
3 Kwa sababu ya sauti ya adui, Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu. Kwa maana wananitupia uovu, Na kwa ghadhabu wananiudhi.
4 Moyo wangu unaumia ndani yangu, Na hofu za mauti zimeniangukia.
5 Hofu na tetemeko limenijia, Na hofu kubwa imenifunikiza.
6 Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.
7 Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.
8 Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.
9 Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao, Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.
10 Mchana na usiku huzunguka kutani mwake; Uovu na taabu zimo ndani yake;
11 Tamaa mbaya zimo ndani yake; Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.
12 Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione.
13 Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.
14 Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.
15 Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.
16 Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa;
17 Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.
18 Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu, Maana walioshindana nami walikuwa wengi.
19 Mungu atasikia na kuwajibu; Ndiye Yeye akaaye tangu milele. Mageuzi ya mambo hayawapati hao, Kwa hiyo hawamchi Mungu.
20 Amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye, Amelihalifu agano lake.
21 Kinywa chake ni laini kuliko siagi, Bali moyo wake ni vita. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, Bali hayo ni panga wazi.
22 Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.
23 Nawe, Ee Mungu, utawatelemsha, Walifikilie shimo la uharibifu; Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao, Bali mimi nitakutumaini Wewe.
1 Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza, Mchana kutwa ananionea akileta vita.
2 Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa, Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi.
3 Siku ya hofu yangu nitakutumaini Wewe;
4 Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?
5 Mchana kutwa wanapotosha maneno yangu, Mawazo yao yote ni juu yangu kunitakia mabaya.
6 Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.
7 Je! Wataokoka kwa uovu wao? Ee Mungu, uwaangamize kwa hasira yako.
8 Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;
10 Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
11 Nimemtumaini Mungu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
12 Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu; Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
13 Maana umeniponya nafsi yangu na mauti; Je! Hukuizuia miguu yangu isianguke? Ili nienende mbele za Mungu Katika nuru ya walio hai.
1 Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita.
2 Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu anitimiziaye mambo yangu.
3 Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake
4 Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
6 Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake!
7 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi,
8 Amka, utukufu wangu. Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.
9 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
10 Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.
11 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
1 Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?
2 Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.
3 Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.
4 Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.
5 Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.
6 Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.
7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.
8 Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,
9 Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.
10 Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.
11 Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.
1 Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
2 Uniponye nao wafanyao maovu, Uniokoe na watu wa damu.
3 Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; Wenye nguvu wamenikusanyikia; Ee Bwana, si kwa kosa langu, Wala si kwa hatia yangu.
4 Bila kosa langu huenda mbio, hujiweka tayari; Uamke uonane nami, na kutazama.
5 Na Wewe, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, uamke. Uwapatilize mataifa yote; Usiwarehemu waovu wafanyao uovu hata mmoja.
6 Wakati wa jioni hurudi, hulia kama mbwa, Na kuzunguka-zunguka mjini.
7 Tazama, kwa vinywa vyao huteuka, Midomoni mwao mna panga, Kwa maana ni nani asikiaye?
8 Na Wewe, Bwana, utawacheka, Utawadhihaki mataifa yote.
9 Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu
10 Mungu wa fadhili zangu atanitangulia, Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu.
11 Usiwaue, watu wangu wasije wakasahau; Uwatawanye kwa uweza wako, Na kuwaangamiza, Ee Bwana, ngao yetu.
12 Kwa dhambi ya kinywa chao, Na kwa neno la midomo yao, Wanaswe kwa kiburi chao, Kwa ajili ya kulaani na uongo wasemao.
13 Uwakomeshe kwa hasira, Uwakomeshe watoweke, Wajue ya kuwa Mungu atawala katika Yakobo, Na hata miisho ya dunia.
14 Wakati wa jioni hurudi, hulia kama mbwa, Na kuzunguka-zunguka mjini.
15 Watatanga-tanga hao wakitafuta chakula; Wasiposhiba watakesha usiku kucha.
16 Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi, Nitaziimba fadhili zako kwa furaha. Kwa kuwa ndiwe uliyekuwa ngome yangu, Na makimbilio siku ya shida yangu.
17 Ee nguvu zangu, nitakuimbia kwa furaha, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu, Mungu wa fadhili zangu.
1 Ee Mungu, umetutupa na kututawanya, Umekuwa na hasira, uturudishe tena.
2 Umeitetemesha nchi na kuipasua, Upaponye palipobomoka, maana inatikisika.
3 Umewaonyesha watu wako mazito, Na kutunywesha mvinyo ya kutuyumbisha.
4 Umewapa wakuogopao bendera, Ili itwekwe kwa ajili ya kweli.
5 Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, utuitikie.
6 Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.
7 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,
8 Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.
9 Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?
10 Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?
11 Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai.
12 Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.
1 Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu.
2 Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda.
3 Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.
4 Nitakaa katika hema yako milele, Nitaikimbilia sitara ya mbawa zako
5 Maana Wewe, Mungu, umezisikia nadhiri zangu. Umewapa urithi wao waliogopao jina lako.
6 Utaziongeza siku za mfalme, Miaka yake itakuwa kama vizazi vingi.
7 Atakaa mbele za Mungu milele, Ziagize fadhili na kweli zimhifadhi.
8 Ndivyo nitakavyoliimbia jina lako daima, Ili niondoe nadhiri zangu kila siku.
1 Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake.
2 Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.
3 Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka,
4 Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani.
5 Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake.
6 Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.
7 Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; Mwamba wa nguvu zangu, Na kimbilio langu ni kwa Mungu.
8 Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.
9 Hakika binadamu ni ubatili, Na wenye cheo ni uongo, Katika mizani huinuka; Wote pamoja ni hafifu kuliko ubatili.
10 Msiitumainie dhuluma, Wala msijivune kwa unyang'anyi; Mali izidipo msiiangalie sana moyoni.
11 Mara moja amenena Mungu; Mara mbili nimeyasikia haya, Ya kuwa nguvu zina Mungu,
12 Na fadhili ziko kwako, Ee Bwana; Maana ndiwe umlipaye kila mtu Sawasawa na haki yake.
1 Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
2 Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.
3 Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.
4 Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
5 Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
6 Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.
7 Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
8 Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
9 Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiharibu, Wataingia pande za nchi zilizo chini.
10 Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwa-mwitu.
11 Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.
1 Mungu, uisikie sauti yangu katika malalamiko yangu; Unilinde uhai wangu na hofu ya adui.
2 Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;
3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu,
4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi.
5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona?
6 Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa.
7 Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa.
8 Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa.
9 Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya Mungu, Na kuyafahamu matendo yake.
10 Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia, Na wote wenye moyo wa adili watajisifu.
1 Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.
2 Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.
3 Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu.
4 Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako.
5 Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana,
6 Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi.
7 Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa;
8 Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.
9 Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.
10 Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.
11 Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.
12 Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha.
13 Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.
1 Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
2 Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake.
3 Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako.
4 Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako.
5 Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;
6 Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko mlikomfurahia.
7 Atawala kwa uweza wake milele; Macho yake yanaangalia mataifa; Waasio wasijitukuze nafsi zao.
8 Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu, Itangazeni sauti ya sifa zake;
9 Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai, Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.
10 Kwa maana umetupima, Ee Mungu, Umetujaribu inavyojaribiwa fedha.
11 Ulituingiza ndani ya wavu, Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea.
12 Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi.
13 Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu;
14 Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni.
15 Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.
16 Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
17 Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu.
18 Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia.
19 Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.
20 Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.
1 Mungu na atufadhili na kutubariki, Na kutuangazia uso wake.
2 Njia yake ijulike duniani, Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
3 Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.
4 Mataifa na washangilie, Naam, waimbe kwa furaha, Maana kwa haki utawahukumu watu, Na kuwaongoza mataifa walioko duniani.
5 Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.
6 Nchi imetoa mazao yake MUNGU, Mungu wetu, ametubariki.
7 Mungu atatubariki sisi; Miisho yote ya dunia itamcha Yeye.
1 Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake.
2 Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.
3 Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha.
4 Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake.
5 Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu.
6 Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.
7 Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani,
8 Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.
9 Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
10 Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
11 Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;
12 Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia; Na mwanamke akaaye nyumbani agawa nyara.
13 Kwa nini kulala mazizini arukapo hua, Mbawa zake ziking'aa kama fedha Na manyoya yake kama dhahabu?
14 Mwenyezi Mungu alipotawanya wafalme huko, Kulinyesha theluji katika Salmoni.
15 Ni mlima wa Mungu mlima Bashani, Ni mlima mrefu mlima Bashani.
16 Enyi milima mirefu, kwani kuutazama kwa wivu Mlima alioutamani Mungu akae juu yake? Naam, Bwana atakaa juu yake milele.
17 Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu.
18 Wewe umepaa juu, umeteka mateka, Umepewa vipawa katikati ya wanadamu; Naam, hata na wakaidi, Bwana Mungu akae nao.
19 Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu.
20 Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.
21 Naam, Mungu atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa.
22 Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari;
23 Uuchovye mguu wako katika damu ya adui zako, Na ulimi wa mbwa zako upate sehemu yake.
24 Ee Mungu, wameiona miendo yako; Miendo ya Mungu wangu, Mfalme wangu, katika patakatifu
25 Waimbaji hutangulia, nyuma yao wapigao vinanda, Kati ya wanawali wapiga matari.
26 Mhimidini Mungu katika mikutano, Bwana katika makusanyiko ya Israeli.
27 Yuko Benyamini mdogo, mtawala wao; Wakuu wa Yuda, kundi lao; Wakuu wa Zabuloni; Wakuu wa Naftali.
28 Ee Mungu, uziamuru nguvu zako; Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
29 Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu Wafalme watakuletea hedaya.
30 Mkemee mnyama wa manyasini; Kundi la mafahali, na ndama za watu; Hata wanyenyekee na kuleta vipande vya fedha, Uwatawanye watu wapendao vita.
31 Masheki watakuja kutoka Misri, Kushi itamnyoshea Mungu mikono yake mara.
32 Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu, Msifuni Bwana kwa nyimbo.
33 Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele; Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
34 Mhesabieni Mungu nguvu; Enzi yake i juu ya Israeli; Na nguvu zake zi mawinguni.
35 Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako. Ndiye Mungu wa Israeli; Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo. Na ahimidiwe Mungu.
1 Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.
2 Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha.
3 Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu.
4 Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.
5 Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu.
6 Wanaokungoja Wewe wasiaibishwe, Kwa ajili yangu, Bwana, MUNGU wa majeshi. Wanaokutafuta Wewe wasifedheheshwe, Kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.
7 Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
9 Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
10 Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu.
11 Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao.
12 Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.
13 Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao; Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.
14 Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.
15 Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze, Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.
16 Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.
17 Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi.
18 Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie.
19 Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote.
20 Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.
21 Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.
22 Meza yao mbele yao na iwe mtego; Naam, wakiwa salama na iwe tanzi.
23 Macho yao yatiwe giza wasione, Na viuno vyao uvitetemeshe daima.
24 Uimwage ghadhabu yako juu yao, Na ukali wa hasira yako uwapate.
25 Matuo yao na yawe ukiwa, Pasiwe na mtu wa kukaa hemani mwao.
26 Maana wanamwudhi mtu uliyempiga Wewe, Wanasimulia maumivu ya hao uliowatia jeraha.
27 Uwaongezee uovu juu ya uovu, Wala wasiingie katika haki yako.
28 Na wafutwe katika chuo cha uhai, Wala pamoja na wenye haki wasiandikwe.
29 Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua.
30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.
31 Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng'ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato.
32 Walioonewa watakapoona watafurahi; Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
33 Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake.
34 Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake.
35 Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda, Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.
36 Wazao wa watumishi wake watairithi, Nao walipendao jina lake watakaa humo.
1 Ee Mungu, uniokoe, Ee Bwana, unisaidie hima.
2 Waaibike, wafedheheke, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.
3 Warudi nyuma, na iwe aibu yao, Wanaosema, Ewe! Ewe!
4 Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Mungu.
5 Nami ni maskini na mhitaji, Ee Mungu, unijilie kwa haraka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Bwana, usikawie.
1 Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele.
2 Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.
3 Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.
4 Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,
5 Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu.
6 Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima.
7 Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.
8 Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa.
9 Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.
10 Kwa maana adui zangu wananiamba, Nao wanaoniotea roho yangu hushauriana.
11 Wakisema, Mungu amemwacha, Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.
12 Ee Mungu, usiwe mbali nami; Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.
13 Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.
14 Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote.
15 Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
16 Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.
17 Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
18 Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako.
19 Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?
20 Wewe, uliyetuonyesha mateso mengi, mabaya, Utatuhuisha tena. Utatupandisha juu tena Tokea pande za chini ya nchi.
21 Laiti ungeniongezea ukuu! Urejee tena na kunifariji moyo.
22 Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu. Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.
23 Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo, Na nafsi yangu uliyoikomboa.
24 Ulimi wangu nao utasimulia Haki yako mchana kutwa. Kwa maana wameaibishwa, Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.
1 Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, Na mwana wa mfalme haki yako.
2 Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
3 Milima itawazalia watu amani, Na vilima navyo kwa haki.
4 Atawahukumu walioonewa wa watu, Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea.
5 Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua, Na wakati wa kung'aa mwezi kizazi hata kizazi.
6 Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa, Kama manyunyu yainyweshayo nchi.
7 Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
8 Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia.
9 Wakaao jangwani na wainame mbele zake; Adui zake na warambe mavumbi.
10 Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi; Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
11 Naam, wafalme wote na wamsujudie; Na mataifa yote wamtumikie.
12 Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
13 Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
14 Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu, Na damu yao ina thamani machoni pake.
15 Basi na aishi; Na wampe dhahabu ya Sheba; Na wamwombee daima; Na kumbariki mchana kutwa.
16 Na uwepo wingi wa nafaka Katika ardhi juu ya milima; Matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni, Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.
17 Jina lake na lidumu milele, Pindi ling'aapo jua jina lake liwe na wazao; Mataifa yote na wajibariki katika yeye, Na kumwita heri.
18 Na ahimidiwe Bwana, Mungu, Mungu wa Israeli, Atendaye miujiza Yeye peke yake;
19 Jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.
20 Maombi ya Daudi mwana wa Yese yamekwisha.
1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao.
2 Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza.
3 Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.
4 Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu.
5 Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu.
6 Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo.
7 Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.
8 Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.
9 Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani.
10 Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao.
11 Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
12 Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.
13 Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa.
14 Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi.
15 Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.
16 Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu;
17 Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao.
18 Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika.
19 Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho.
20 Ee Bwana, kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao.
21 Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma,
22 Nalikuwa kama mjinga, sijui neno; Nalikuwa kama mnyama tu mbele zako.
23 Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika mkono wa kuume.
24 Utaniongoza kwa shauri lako, Na baadaye utanikaribisha kwa utukufu.
25 Ni nani niliye naye mbinguni, Wala duniani sina cha kupendeza ila Wewe.
26 Mwili wangu na moyo wangu hupunguka, Bali Mungu ni mwamba wa moyo wangu Na sehemu yangu milele.
27 Maana wajitengao nawe watapotea; Umewaangamiza wote waliokuacha Wewe.
28 Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; Nimefanya kimbilio kwa Bwana MUNGU, Niyahubiri matendo yako yote.
1 Ee Mungu, mbona umetutupa milele? Kwa nini hasira yako inatoka moshi Juu ya kondoo wa malisho yako?
2 Ulikumbuke kusanyiko lako, Ulilolinunua zamani. Ulilolikomboa liwe kabila ya urithi wako, Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.
3 Upainulie miguu yako palipoharibika milele; Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.
4 Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako; Wameweka bendera zao ziwe alama.
5 Wanaonekana kama watu wainuao mashoka, Waikate miti ya msituni.
6 Na sasa nakishi yake yote pia Wanaivunja-vunja kwa mashoka na nyundo.
7 Wamepatia moto patakatifu pako; Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.
8 Walisema mioyoni mwao, Na tuwaangamize kabisa; Mahali penye mikutano ya Mungu Wamepachoma moto katika nchi pia.
9 Hatuzioni ishara zetu, wala sasa hakuna nabii, Wala kwetu hakuna ajuaye, hata lini?
10 Ee Mungu, mtesi atalaumu hata lini? Adui alidharau jina lako hata milele?
11 Mbona unaurudisha mkono wako, Naam, mkono wako wa kuume, Uutoe kifuani mwako, Ukawaangamize kabisa.
12 Lakini Mungu ni mfalme wangu tokea zamani, Afanyaye mambo ya wokovu katikati ya nchi.
13 Wewe umeipasua bahari kwa nguvu zako, Umevivunja vichwa vya nyangumi juu ya maji.
14 Wewe uliviseta vichwa vya lewiathani, Awe chakula cha watu wa jangwani.
15 Wewe ulitokeza chemchemi na kijito; Wewe ulikausha mito yenye maji sikuzote.
16 Mchana ni wako, usiku nao ni wako, Ndiwe uliyeufanya mwanga na jua.
17 Wewe uliiweka mipaka yote ya dunia, Kaskazi na kusi Wewe ulizitengeneza.
18 Ee Bwana, uyakumbuke hayo, adui amelaumu, Na watu wapumbavu wamelidharau jina lako.
19 Usimpe mnyama mkali nafsi ya hua wako; Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
20 Ulitafakari agano; Maana mahali penye giza katika nchi Pamejaa makao ya ukatili.
21 Aliyeonewa asirejee ametiwa haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.
22 Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.
23 Usiisahau sauti ya watesi wako, Ghasia yao wanaokuondokea inapaa daima.
1 Ee Mungu, twakushukuru. Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.
2 Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki.
3 Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.
4 Naliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe.
5 Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi.
6 Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima.
7 Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu.
8 Maana mkononi mwa Bwana mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa.
9 Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.
10 Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.
1 Katika Yuda Mungu amejulikana, Katika Israeli jina lake ni kuu.
2 Kibanda chake pia kiko Salemu, Na maskani yake iko Sayuni.
3 Huko ndiko alikoivunja mishale ya uta, Ngao, na upanga, na zana za vita.
4 Wewe U mwenye fahari na adhama, Toka milima ya mateka.
5 Wametekwa wenye moyo thabiti; Wamelala usingizi; Wala hawakuiona mikono yao Watu wote walio hodari.
6 Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, Gari na farasi wameshikwa na usingizi mzito.
7 Wewe ndiwe utishaye, naam, Wewe; Naye ni nani awezaye kusimama ufanyapo hasira?
8 Toka mbinguni ulitangaza hukumu; Nchi iliogopa, ikakaa kimya.
9 Mungu aliposimama ili kuhukumu Na kuwaokoa wapole wa dunia wote pia.
10 Maana hasira ya binadamu itakusifu, Masalio ya hasira utajifunga kama mshipi.
11 Wekeni nadhiri, mkaziondoe Kwa Bwana, Mungu wenu. Wote wanaomzunguka wamletee hedaya, Yeye astahiliye kuogopwa.
12 Yeye huzikata roho za wakuu; Na kuwatisha wafalme wa dunia.
1 Nimpazie Mungu sauti yangu, Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.
2 Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana; Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea; Nafsi yangu ilikataa kufarijika.
3 Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika; Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.
4 Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike; Naliona mashaka nisiweze kunena.
5 Nalifikiri habari za siku za kale, Miaka ya zamani zilizopita.
6 Nakumbuka wimbo wangu usiku, Nawaza moyoni mwangu, Roho yangu ikatafuta.
7 Je! Bwana atatupa milele na milele? Hatatenda fadhili tena kabisa?
8 Rehema zake zimekoma hata milele? Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?
9 Mungu amesahau fadhili zake? Amezuia kwa hasira rehema zake?
10 Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo; Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kuume wake Aliye juu.
11 Nitayakumbuka matendo ya Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.
12 Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako.
13 Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?
14 Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.
15 Kwa mkono wako umewakomboa watu wako, Wana wa Yakobo na Yusufu.
16 Ee Mungu, yale maji yalikuona, Yale maji yalikuona, yakaogopa. Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,
17 Mawingu yakamwaga maji. Mbingu nazo zikatoa sauti, Mishale yako nayo ikatapakaa.
18 Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli; Umeme uliuangaza ulimwengu. Nchi ilitetemeka na kutikisika;
19 Njia yako ilikuwa katika bahari. Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu; Hatua zako hazikujulikana.
20 Uliwaongoza watu wako kama kundi, Kwa mkono wa Musa na Haruni.
1 Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
2 Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale.
3 Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia.
4 Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.
5 Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao,
6 Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao
7 Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake.
8 Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.
9 Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita.
10 Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake;
11 Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha.
12 Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani.
13 Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu.
14 Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto.
15 Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi.
16 Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito.
17 Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu.
18 Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.
19 Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?
20 Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama?
21 Hivyo Bwana aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli.
22 Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake.
23 Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni;
24 Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni.
25 Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.
26 Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake.
27 Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari.
28 Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao.
29 Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani;
30 Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao
31 Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.
32 Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.
33 Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha.
34 Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
35 Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao.
36 Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
37 Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
38 Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote.
39 Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi.
40 Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani!
41 Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.
42 Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.
43 Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani.
44 Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa.
45 Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.
46 Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.
47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.
48 Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.
49 Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya.
50 Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;
51 Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.
52 Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani.
53 Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao.
54 Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.
55 Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.
56 Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake.
57 Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa.
58 Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao.
59 Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa.
60 Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;
61 Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi.
62 Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake.
63 Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64 Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza.
65 Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;
66 Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele.
67 Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu.
68 Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda.
69 Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele.
70 Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo.
71 Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.
72 Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.
1 Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako, Wamelinajisi hekalu lako takatifu. Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.
2 Wameziacha maiti za watumishi wako Ziwe chakula cha ndege wa angani. Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi.
3 Wamemwaga damu yao kama maji Pande zote za Yerusalemu, Wala hapakuwa na mzishi.
4 Tumekuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
5 Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele? Wivu wako utawaka kama moto?
6 Ukali wako uwamwagie mataifa wasiokujua, Na falme za hao wasioliitia jina lako.
7 Kwa maana wamemla Yakobo, Na matuo yake wameyaharibu.
8 Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu, Rehema zako zije kutulaki hima, Kwa maana tumedhilika sana.
9 Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie, Kwa ajili ya utukufu wa jina lako. Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.
10 Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao? Kisasi cha damu ya watumishi wako iliyomwagika Kijulike kati ya mataifa machoni petu.
11 Kuugua kwake aliyefungwa Na kuingie mbele zako. Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako Uwahifadhi wana wa mauti.
12 Uwalipe jirani zetu mara saba vifuani mwao Laumu zao walizokulaumu, Ee Bwana.
13 Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele; Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.
1 Wewe uchungaye Israeli, usikie, Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
2 Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe.
3 Ee Mungu, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
4 Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?
5 Umewalisha mkate wa machozi, Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.
6 Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.
7 Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
8 Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.
9 Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.
10 Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.
11 Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.
12 Kwa nini umezibomoa kuta zake, Wakauchuma wote wapitao njiani?
13 Nguruwe wa msituni wanauharibu, Na hayawani wa kondeni wanautafuna.
14 Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi, Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
15 Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.
16 Umechomwa moto; umekatwa; Kwa lawama ya uso wako wanapotea.
17 Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume; Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;
18 Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma; Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
19 Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.
1 Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha, Mshangilieni Mungu wa Yakobo.
2 Pazeni zaburi, pigeni matari, Kinubi chenye sauti nzuri, na kinanda.
3 Pigeni panda mwandamo wa mwezi, Wakati wa mbalamwezi, sikukuu yetu.
4 Kwa maana ni sheria kwa Israeli, Ni hukumu ya Mungu wa Yakobo.
5 Aliamuru iwe ushuhuda katika Yusufu, Alipoondoka juu ya nchi ya Misri; Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
6 Nimelitenga bega lake na mzigo, Mikono yake ikaachana na kikapu.
7 Katika shida uliniita nikakuokoa; Nalikuitikia katika sitara ya radi; Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
8 Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya, Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza;
9 Usiwe na mungu mgeni ndani yako; Wala usimsujudie mungu mwingine.
10 Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, Niliyekupandisha toka nchi ya Misri; Fumbua sana kinywa chako nami nitakijaza.
11 Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka.
12 Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao.
13 Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
14 Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;
15 Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele.
16 Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani.
1 Mungu asimama katika kusanyiko la Mungu; Katikati ya miungu anahukumu.
2 Hata lini mtahukumu kwa dhuluma, Na kuzikubali nyuso za wabaya?
3 Mfanyieni hukumu maskini na yatima; Mtendeeni haki aliyeonewa na fukara;
4 Mwokoeni maskini na mhitaji; Mwopoeni mikononi mwa wadhalimu.
5 Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani; Misingi yote ya nchi imetikisika.
6 Mimi nimesema, Ndinyi miungu, Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
7 Lakini mtakufa kama wanadamu, Mtaanguka kama mmoja wa wakuu.
8 Ee Mungu, usimame, uihukumu nchi, Maana Wewe utawarithi mataifa yote.
1 Ee Mungu, usistarehe, Ee Mungu, usinyamae, wala usitulie.
2 Maana adui zako wanafanya ghasia, Nao wakuchukiao wameviinua vichwa vyao.
3 Juu ya watu wako wanafanya hila, Na kushauriana juu yao uliowaficha.
4 Wamesema, Njoni, tuwakatilie mbali wasiwe taifa, Na jina la Israeli halitakumbukwa tena.
5 Maana wanashauriana kwa moyo mmoja, Juu yako wanafanyana agano.
6 Hema za Edomu, na Waishmaeli, Na Moabu, na Wahagari,
7 Gebali, na Amoni, na Amaleki, Na Filisti, nao wanaokaa Tiro,
8 Ashuri naye amepatana nao, Wamewasaidia wana wa Lutu.
9 Uwatende kama Midiani, kama Sisera, Kama Yabini, penye kijito Kishoni.
10 Ambao waliangamizwa Endori; Wakawa samadi juu ya nchi.
11 Uwafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, Na masheki yao wote kama Zeba na Zalmuna.
12 Ambao Walisema, Na tutamalaki makao ya Mungu.
13 Ee Mungu, uwafanye kama mavumbi ya kisulisuli, Mithili ya makapi mbele ya upepo,
14 Kama moto uteketezao msitu, Kama miali ya moto iiwashayo milima,
15 Ndivyo utakavyowafuatia kwa tufani yako, Na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.
16 Uwajaze nyuso zao fedheha; Wakalitafute jina lako, Bwana.
17 Waaibike, wafadhaike milele, Naam, watahayarike na kupotea.
18 Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.
1 Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi!
2 Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai.
3 Shomoro naye ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kioto, Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu.
4 Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima.
5 Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
6 Wakipita kati ya bonde la Vilio, Hulifanya kuwa chemchemi, Naam, mvua ya vuli hulivika baraka
7 Huendelea toka nguvu hata nguvu, Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
8 Bwana, Mungu wa majeshi, uyasikie maombi yangu, Ee Mungu wa Yakobo, usikilize,
9 Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi wako.
10 Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu.
11 Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.
12 Ee Bwana wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.
1 Bwana, umeiridhia nchi yako, Umewarejeza mateka wa Yakobo.
2 Umeusamehe uovu wa watu wako, Umezisitiri hatia zao zote.
3 Umeiondoa ghadhabu yako yote, Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.
4 Mungu wa wokovu wetu, uturudishe, Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.
5 Je! Utatufanyia hasira hata milele? Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi?
6 Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha, Watu wako wakufurahie?
7 Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
8 Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena.
9 Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, Utukufu ukae katika nchi yetu.
10 Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana.
11 Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni.
12 Naam, Bwana atatoa kilicho chema, Na nchi yetu itatoa mazao yake.
13 Haki itakwenda mbele zake, Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
1 Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji
2 Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3 Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
4 Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
5 Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.
6 Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu.
7 Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia.
8 Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako.
9 Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako;
10 Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako.
11 Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;
12 Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.
13 Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.
14 Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.
15 Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
16 Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.
17 Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.
1 Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.
2 Bwana ayapenda malango ya Sayuni Kuliko maskani zote za Yakobo.
3 Umetajwa kwa mambo matukufu, Ee Mji wa Mungu.
4 Nitataja Rahabu na Babeli Miongoni mwao wanaonijua. Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi; Huyu alizaliwa humo.
5 Naam, mintarafu Sayuni itasemwa, Huyu na huyu alizaliwa humo. Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara.
6 Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa, Huyu alizaliwa humo.
7 Waimbao na wachezao na waseme, Visima vyangu vyote vimo mwako.
1 Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako.
2 Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.
3 Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu.
4 Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.
5 Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.
6 Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.
7 Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.
8 Wanijuao umewatenga nami; Umenifanya kuwa chukizo kwao; Nimefungwa wala siwezi kutoka.
9 Jicho langu limefifia kwa ajili ya mateso Bwana, nimekuita kila siku; Nimekunyoshea Wewe mikono yangu.
10 Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi?
11 Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu?
12 Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?
13 Lakini mimi nimekulilia Wewe, Bwana, Na asubuhi maombi yangu yatakuwasilia.
14 Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako?
15 Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika.
16 Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza.
17 Yamenizunguka kama maji mchana kutwa, Yamenisonga yote pamoja.
18 Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani.
1 Fadhili za Bwana nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
2 Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
3 Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
4 Wazao wako nitawafanya imara milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
5 Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
6 Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana? Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika?
7 Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
8 Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka.
9 Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.
10 Ndiwe uliyemseta Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao.
11 Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake.
12 Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako.
13 Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kuume umetukuka.
14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako.
15 Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
16 Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa.
17 Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka.
18 Maana ngao yetu ina Bwana, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.
19 Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, Ukasema, nimempa aliye hodari msaada; Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.
20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
21 Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu.
22 Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.
23 Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia.
24 Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
25 Nitaweka mkono wake juu ya bahari, Na mkono wake wa kuume juu ya mito.
26 Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
27 Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
28 Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake.
29 Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
30 Wanawe wakiiacha sheria yangu, Wasiende katika hukumu zangu,
31 Wakizihalifu amri zangu, Wasiyashike maagizo yangu,
32 Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo.
33 Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye, Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.
34 Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.
35 Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu, Hakika sitamwambia Daudi uongo,
36 Wazao wake watadumu milele, Na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu.
37 Kitathibitika milele kama mwezi; Shahidi aliye mbinguni mwaminifu.
38 Walakini Wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi wako.
39 Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umeinajisi taji yake na kuitupa chini.
40 Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu.
41 Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amekuwa laumu kwa jirani zake;
42 Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia.
43 Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani.
44 Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini.
45 Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu.
46 Ee Bwana, hata lini? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto?
47 Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu!
48 Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?
49 Bwana, zi wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?
50 Ee Bwana, ukumbuke, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi.
51 Ambayo adui zako wamesimanga, Ee Bwana, Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako.
52 Na ahimidiwe Bwana milele. Amina na Amina.
1 Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, Kizazi baada ya kizazi.
2 Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
3 Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
4 Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku.
5 Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo.
6 Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.
7 Maana tumetoweshwa kwa hasira yako, Na kwa ghadhabu yako tumefadhaishwa.
8 Umeyaweka maovu yetu mbele zako, Siri zetu katika mwanga wa uso wako.
9 Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite.
10 Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.
11 Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako?
12 Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.
13 Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.
14 Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
15 Utufurahishe kwa kadiri ya siku ulizotutesa, Kama miaka ile tuliyoona mabaya.
16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao.
17 Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti, Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.
1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
2 Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.
3 Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.
4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.
5 Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana,
6 Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,
7 Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.
8 Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.
9 Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.
10 Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.
11 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.
1 Ni neno jema kumshukuru Bwana, Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.
2 Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku.
3 Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi.
4 Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
5 Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6 Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.
7 Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;
8 Bali Wewe, Bwana, U Mtukufu hata milele.
9 Maana hao adui zako, Ee Bwana, Hao adui zako watapotea, Na watendao maovu watatawanyika wote pia.
10 Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati, Nimepakwa mafuta mabichi.
11 Na jicho langu limewatazama walioniotea, Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia.
12 Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13 Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
15 Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.
1 Bwana ametamalaki, amejivika adhama, Bwana amejivika, na kujikaza nguvu. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
2 Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani; Wewe ndiwe uliye tangu milele.
3 Ee Bwana, mito imepaza, Mito imepaza sauti zake, Mito imepaza uvumi wake.
4 Kupita sauti ya maji mengi, maji makuu, Kupita mawimbi ya bahari yaumkayo, Bwana Aliye juu ndiye mwenye ukuu.
5 Shuhuda zako ni amini sana; Utakatifu ndio uifaao nyumba yako, Ee Bwana, milele na milele.
1 Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze,
2 Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao.
3 Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?
4 Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi?
5 Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako;
6 Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima.
7 Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.
8 Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?
9 Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?
10 Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue?
11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.
12 Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako;
13 Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.
14 Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake,
15 Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.
16 Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu?
17 Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya.
18 Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
19 Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu.
20 Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria?
21 Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia.
22 Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia.
23 Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza.
1 Njoni, tumwimbie Bwana, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
2 Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu.
6 Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
7 Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
8 Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani.
9 Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu.
10 Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile, Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo, Hawakuzijua njia zangu.
11 Nikaapa kwa hasira yangu Wasiingie rahani mwangu.
1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana, nchi yote.
2 Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
3 Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake.
4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
5 Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
6 Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.
7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
8 Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.
9 Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
10 Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike, Atawahukumu watu kwa adili.
11 Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
12 Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
13 Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.
1 Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, Visiwa vingi na vifurahi.
2 Mawingu na giza vyamzunguka, Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
3 Moto hutangulia mbele zake, Nao huwateketeza watesi wake pande zote.
4 Umeme wake uliuangaza ulimwengu, Nchi ikaona ikatetemeka.
5 Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana, Mbele za Bwana wa dunia yote.
6 Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake.
7 Na waaibishwe wote waabuduo sanamu, Wajivunao kwa vitu visivyofaa; Enyi miungu yote, msujuduni Yeye.
8 Sayuni imesikia na kufurahi, Binti za Yuda walishangilia, Kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana.
9 Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote; Umetukuka sana juu ya miungu yote.
10 Enyi mmpendao Bwana, uchukieni uovu; Huwalinda nafsi zao watauwa wake, Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.
11 Nuru imemzukia mwenye haki, Na furaha wanyofu wa moyo.
12 Enyi wenye haki, mmfurahieni Bwana, Na kulishukuru jina lake takatifu.
1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
2 Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
3 Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
4 Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
5 Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
6 Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
7 Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
8 Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha.
9 Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.
1 Bwana ametamalaki, mataifa wanatetemeka; Ameketi juu ya makerubi, nchi inatikisika.
2 Bwana katika Sayuni ni mkuu, Naye ametukuka juu ya mataifa yote.
3 Na walishukuru jina lake kuu la kuhofiwa; Ndiye mtakatifu.
4 Nguvu za mfalme nazo zapenda hukumu; Wewe ndiwe uliyeithibitisha adili; Ulifanya hukumu na haki katika Yakobo.
5 Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni penye kiti cha miguu yake; Ndiye mtakatifu.
6 Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia;
7 Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao. Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa.
8 Ee Bwana, Mungu wetu, ndiwe uliyewajibu; Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe Ingawa uliwapatiliza matendo yao.
9 Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.
1 Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
2 Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba;
3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
4 Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake;
5 Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
1 Rehema na hukumu nitaziimba, Ee Bwana, nitakuimbia zaburi.
2 Nitaiangalia njia ya unyofu; Utakuja kwangu lini? Nitakwenda kwa unyofu wa moyo Ndani ya nyumba yangu.
3 Sitaweka mbele ya macho yangu Neno la uovu. Kazi yao waliopotoka naichukia, Haitaambatana nami.
4 Moyo wa ukaidi utaondoka kwangu, Lililo ovu sitalijua.
5 Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye.
6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, Hao wakae nami. Yeye aendaye katika njia kamilifu, Ndiye atakayenitumikia.
7 Hatakaa ndani ya nyumba yangu Mtu atendaye hila. Asemaye uongo hatathibitika Mbele ya macho yangu.
8 Asubuhi hata asubuhi nitawaharibu Wabaya wote wa nchi. Niwatenge wote watendao uovu Na mji wa Bwana.
1 Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.
2 Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.
3 Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga.
4 Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka, Naam, ninasahau kula chakula changu.
5 Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu.
6 Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani, Na kufanana na bundi wa mahameni.
7 Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro Aliye peke yake juu ya nyumba.
8 Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu Huapa kwa kunitaja mimi.
9 Maana nimekula majivu kama chakula, Na kukichanganya kinywaji changu na machozi.
10 Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako; Maana umeniinua na kunitupilia mbali.
11 Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa, Nami ninanyauka kama majani.
12 Bali Wewe, Bwana utaketi ukimiliki milele, Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.
13 Wewe mwenyewe utasimama, Na kuirehemu Sayuni, Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia, Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.
14 Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake, Na kuyaonea huruma mavumbi yake.
15 Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
16 Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake,
17 Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao.
18 Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
19 Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
20 Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
21 Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni, Na sifa zake katika Yerusalemu,
22 Pindi mataifa watapokusanyika pamoja, Falme nazo ili kumtumikia Bwana.
23 Amezipunguza nguvu zangu njiani; Amezifupisha siku zangu.
24 Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.
25 Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika.
27 Lakini Wewe U Yeye yule; Na miaka yako haitakoma.
28 Wana wa watumishi wako watakaa, Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.
3 Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,
4 Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,
5 Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;
6 Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
7 Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.
8 Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
9 Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele.
10 Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
12 Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
14 Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
15 Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.
16 Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko! Na mahali pake hapatalijua tena.
17 Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana;
18 Maana, wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.
19 Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.
21 Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
22 Mhimidini Bwana, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Wewe, Bwana, Mungu wangu, Umejifanya mkuu sana; Umejivika heshima na adhama.
2 Umejivika nuru kama vazi; Umezitandika mbingu kama pazia;
3 Na kuziweka nguzo za orofa zake majini. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, Na kwenda juu ya mabawa ya upepo,
4 Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.
5 Uliiweka nchi juu ya misingi yake, Isitikisike milele.
6 Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi, Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.
7 Kwa kukemea kwako yakakimbia, Kwa sauti ya radi yako yakaenda zake kasi,
8 Yakapanda milima, yakatelemka mabondeni, Mpaka mahali ulipoyatengenezea.
9 Umeweka mpaka yasiupite, Wala yasirudi kuifunikiza nchi.
10 Hupeleka chemchemi katika mabonde; Zapita kati ya milima;
11 Zamnywesha kila mnyama wa kondeni; Punda mwitu huzima kiu yao.
12 Kandokando hukaa ndege wa angani; Kati ya matawi hutoa sauti zao.
13 Huinywesha milima toka orofa zake; Nchi imeshiba mazao ya kazi zako.
14 Huyameesha majani kwa makundi, Na maboga kwa matumizi ya mwanadamu; Ili atoe chakula katika nchi,
15 Na divai imfurahishe mtu moyo wake. Aung'aze uso wake kwa mafuta, Na mkate umburudishe mtu moyo wake.
16 Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17 Ndimo ndege wafanyamo vitundu vyao, Na korongo, misunobari ni nyumba yake.
18 Milima mirefu ndiko waliko mbuzi wa mwitu, Na magenge ni kimbilio la wibari.
19 Aliufanya mwezi kwa ajili ya nyakati, Jua latambua kuchwa kwake.
20 Wewe hufanya giza, kukawa usiku, Ndipo atambaapo kila mnyama wa mwitu.
21 Wana-simba hunguruma wakitaka mawindo, Ili kutafuta chakula chao kwa Mungu.
22 Jua lachomoza, wanakwenda zao, Na kujilaza mapangoni mwao.
23 Mwanadamu atoka kwenda zake kazini, Na kwenye utumishi wake mpaka jioni.
24 Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.
25 Bahari iko kule, kubwa na upana, Ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, Viumbe hai vidogo kwa vikubwa.
26 Ndimo zipitamo merikebu, Ndimo alimo lewiathani uliyemwumba acheze humo.
27 Hao wote wanakungoja Wewe, Uwape chakula chao kwa wakati wake.
28 Wewe huwapa, Wao wanakiokota; Wewe waukunjua mkono wako, Wao wanashiba mema;
29 Wewe wauficha uso wako, Wao wanafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao,
30 Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
31 Utukufu wa Bwana na udumu milele; Bwana na ayafurahie matendo yake.
32 Aitazama nchi, inatetemeka; Aigusa milima, inatoka moshi.
33 Nitamwimbia Bwana maadamu ninaishi; Nitamshangilia Mungu wangu nikiwa hai;
34 Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake; Mimi nitamfurahia Bwana.
35 Wenye dhambi waangamizwe katika nchi, Watendao ubaya wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake.
2 Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.
3 Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
4 Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote.
5 Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya, Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.
6 Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7 Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake.
8 Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
9 Agano alilofanya na Ibrahimu, Na uapo wake kwa Isaka.
10 Alilomthibitishia Yakobo liwe amri, Na Israeli liwe agano la milele.
11 Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani, Iwe urithi wenu mliopimiwa.
12 Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa, Naam, watu wachache na wageni ndani yake,
13 Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa, Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine.
14 Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.
15 Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.
16 Akaiita njaa iijilie nchi, Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
17 Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani.
18 Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma.
19 Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu.
20 Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia.
21 Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote.
22 Awafunge masheki wake kama apendavyo, Na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Israeli naye akaingia Misri, Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.
24 Akawajalia watu wake wazae sana, Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.
25 Akawageuza moyo wawachukie watu wake, Wakawatendea hila watumishi wake.
26 Akamtuma Musa, mtumishi wake, Na Haruni ambaye amemchagua.
27 Akaweka mambo ya ishara zake kati yao, Na miujiza katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza, kukafunga giza, Wala hawakuyaasi maneno yake.
29 Aliyageuza maji yao yakawa damu, Akawafisha samaki wao.
30 Nchi yao ilijaa vyura, Vyumbani mwa wafalme wao.
31 Alisema, kukaja makundi ya mainzi, Na chawa mipakani mwao mwote.
32 Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe, Na moto wa miali katika nchi yao.
33 Akaipiga mizabibu yao na mitini yao, Akaivunja miti ya mipaka yao.
34 Alisema, kukaja nzige, Na tunutu wasiohesabika;
35 Wakaila miche yote ya nchi yao, Wakayala matunda ya ardhi yao.
36 Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi, Malimbuko ya nguvu zao.
37 Akawatoa hali wana fedha na dhahabu, Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka, Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.
39 Alitandaza wingu liwe funiko, Na moto utoe nuru usiku.
40 Walipotaka akaleta kware, Akawashibisha chakula cha mbinguni.
41 Akaufunua mwamba, kukabubujika maji, Yakapita pakavuni kama mto.
42 Maana alilikumbuka neno lake takatifu, Na Ibrahimu, mtumishi wake.
43 Akawatoa watu wake kwa shangwe, Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.
44 Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu;
45 Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake. Haleluya.
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana, Kuzihubiri sifa zake zote?
3 Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote.
4 Ee Bwana, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako,
5 Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako.
6 Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu, Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
7 Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu.
8 Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu.
9 Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda.
10 Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao.
11 Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao.
12 Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.
13 Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake.
14 Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani.
15 Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao.
16 Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa Bwana.
17 Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu.
18 Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya.
19 Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
20 Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani.
21 Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri.
22 Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
23 Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.
24 Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake.
25 Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya Bwana.
26 Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani,
27 Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali.
28 Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu.
29 Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia.
30 Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa.
31 Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.
32 Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao,
33 Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.
34 Hawakuwaharibu watu wa nchi Kama Bwana alivyowaambia;
35 Bali walijichanganya na mataifa, Wakajifunza matendo yao.
36 Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao.
37 Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.
38 Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.
39 Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao.
40 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake.
41 Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala.
42 Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.
43 Mara nyingi aliwaponya, Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao, Wakadhilika katika uovu wao.
44 Lakini aliyaangalia mateso yao, Aliposikia kilio chao.
45 Akawakumbukia agano lake; Akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake;
46 Akawajalia kuhurumiwa Na watu wote waliowateka.
47 Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako.
48 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Watu wote na waseme, Amina. Haleluya.
1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.
3 Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.
4 Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa.
5 Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.
6 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
7 Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.
8 Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
9 Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema.
10 Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,
11 Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu.
12 Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.
13 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
14 Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao.
15 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
16 Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.
17 Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.
18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti.
19 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
20 Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.
21 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
22 Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.
23 Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi,
24 Hao huziona kazi za Bwana, Na maajabu yake vilindini.
25 Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake.
26 Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya.
27 Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea.
28 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.
29 Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza.
30 Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.
31 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.
32 Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee.
33 Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu.
34 Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa.
35 Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.
36 Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa.
37 Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.
38 Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao.
39 Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni.
40 Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.
41 Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo.
42 Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.
43 Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.
1 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba, nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu.
2 Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.
3 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
4 Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
6 Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, uniitikie.
7 Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,
9 Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.
10 Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?
11 Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?
12 Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai.
13 Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.
1 Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze,
2 Kwa maana wamenifumbulia kinywa; Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo.
3 Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure.
4 Badala ya upendo wangu wao hunishitaki, Ijapokuwa naliwaombea.
5 Wamenichukuza mabaya badala ya mema, Na chuki badala ya upendo wangu.
6 Uweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki asimame mkono wake wa kuume.
7 Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi.
8 Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine.
9 Wanawe na wawe yatima, Na mkewe na awe mjane.
10 Kutanga na watange wanawe na kuomba, Watafute chakula mbali na mahame yao.
11 Mdai na anase vitu vyote alivyo navyo, Wageni na wateke mapato ya kazi yake.
12 Asiwe na mtu wa kumfanyia fadhili, Wala mtu wa kuwahurumia yatima wake.
13 Wazao wake waangamizwe, Jina lao likafutwe katika kizazi cha pili.
14 Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za Bwana, Na dhambi ya mamaye isifutwe.
15 Ziwe mbele za Bwana daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
16 Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo,
17 Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye,
18 Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake.
19 Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima.
20 Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya.
21 Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe.
22 Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.
23 Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka, Ninapeperushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.
25 Nami nalikuwa laumu kwao, Wanionapo hutikisa vichwa vyao.
26 Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe sawasawa na fadhili zako.
27 Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo.
28 Wao walaani, bali Wewe utabariki, Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi.
29 Washitaki wangu watavikwa fedheha, Watajivika aibu yao kama joho.
30 Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano.
31 Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake.
1 Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
2 Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako;
3 Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako.
4 Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.
5 Bwana yu mkono wako wa kuume; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake.
6 Atahukumu kati ya mataifa, Ataijaza nchi mizoga; Ataseta kichwa katika nchi nyingi.
7 Atakunywa maji ya mto njiani; Kwa hiyo atakiinua kichwa chake.
1 Haleluya Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
2 Matendo ya Bwana ni makuu, Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
3 Kazi yake ni heshima na adhama, Na haki yake yakaa milele.
4 Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
5 Amewapa wamchao chakula; Atalikumbuka agano lake milele.
6 Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake, Kwa kuwapa urithi wa mataifa.
7 Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini,
8 Yamethibitika milele na milele, Yamefanywa katika kweli na adili.
9 Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa.
10 Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.
1 Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.
2 Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
3 Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.
4 Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki.
5 Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki.
6 Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele.
7 Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
8 Moyo wake umethibitika hataogopa, Hata awaone watesi wake wameshindwa.
9 Amekirimu, na kuwapa maskini, Haki yake yakaa milele, Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
10 Asiye haki ataona na kusikitika, Atasaga meno yake na kuyeyuka, Tamaa ya wasio haki itapotea.
1 Haleluya. Enyi watumishi wa Bwana, sifuni, Lisifuni jina la Bwana.
2 Jina la Bwana lihimidiwe Tangu leo na hata milele.
3 Toka maawio ya jua hata machweo yake Jina la Bwana husifiwa.
4 Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote, Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
5 Ni nani aliye mfano wa Bwana, Mungu wetu aketiye juu;
6 Anyenyekeaye kutazama, Mbinguni na duniani?
7 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
8 Amketishe pamoja na wakuu, Pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, Awe mama ya watoto mwenye furaha.
1 Haleluya. Israeli alipotoka Misri, Na Yakobo katika watu wa lugha ya kigeni.
2 Yuda ilikuwa patakatifu pake, Israeli milki yake.
3 Bahari iliona ikakimbia, Yordani ilirudishwa nyuma.
4 Milima iliruka kama kondoo waume, Vilima kama wana-kondoo.
5 Ee bahari, una nini, ukimbie? Yordani, urudi nyuma?
6 Enyi milima, mruke kama kondoo waume? Enyi vilima, kama wana-kondoo?
7 Tetemeka, Ee nchi, mbele za uso wa Bwana, Mbele za uso wa Mungu wa Yakobo.
8 Augeuza mwamba kuwa ziwa la maji, Jiwe gumu kuwa chemchemi.
1 Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako, Kwa ajili ya uaminifu wako.
2 Kwa nini mataifa kusema, Yuko wapi Mungu wao?
3 Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda.
4 Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,
7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
8 Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.
9 Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
10 Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
11 Enyi mmchao Bwana, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
12 Bwana ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni,
13 Atawabariki wamchao Bwana, Wadogo kwa wakubwa.
14 Bwana na awaongeze ninyi, Ninyi na watoto wenu.
15 Na mbarikiwe ninyi na Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
16 Mbingu ni mbingu za Bwana, Bali nchi amewapa wanadamu.
17 Sio wafu wamsifuo Bwana, Wala wo wote washukao kwenye kimya;
18 Bali sisi tutamhimidi Bwana, Tangu leo na hata milele.
1 Haleluya. Nampenda Bwana kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu.
2 Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.
3 Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni;
4 Nikaliitia jina la Bwana. Ee Bwana, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu.
5 Bwana ni mwenye neema na haki, Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema.
6 Bwana huwalinda wasio na hila; Nalidhilika, akaniokoa.
7 Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako, Kwa kuwa Bwana amekutendea ukarimu.
8 Maana umeniponya nafsi yangu na mauti, Macho yangu na machozi, Na miguu yangu na kuanguka.
9 Nitaenenda mbele za Bwana Katika nchi za walio hai.
10 Naliamini, kwa maana nitasema, Mimi naliteswa sana.
11 Mimi nalisema kwa haraka yangu, Wanadamu wote ni waongo.
12 Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
13 Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la Bwana;
14 Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, Naam, mbele ya watu wake wote.
15 Ina thamani machoni pa Bwana Mauti ya wacha Mungu wake.
16 Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako, Umevifungua vifungo vyangu.
17 Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina la Bwana;
18 Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, Naam, mbele ya watu wake wote.
19 Katika nyua za nyumba ya Bwana, Ndani yako, Ee Yerusalemu.
1 Haleluya. Enyi mataifa yote, msifuni Bwana, Enyi watu wote, mhimidini.
2 Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu, Na uaminifu wa Bwana ni wa milele.
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
3 Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
4 Wamchao Bwana na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
5 Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi.
6 Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
7 Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa.
8 Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu.
9 Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.
10 Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
11 Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
12 Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali.
13 Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini Bwana akanisaidia.
14 Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu.
15 Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
16 Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
17 Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
18 Bwana ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife.
19 Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru Bwana.
20 Lango hili ni la Bwana, Wenye haki ndio watakaoliingia.
21 Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu.
22 Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23 Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.
24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.
25 Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
26 Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
27 Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu.
28 Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.
29 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
1 Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.
2 Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.
3 Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake.
4 Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana.
5 Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako.
6 Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote.
7 Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako
8 Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa
9 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
10 Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
12 Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.
13 Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako.
14 Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi.
15 Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako.
16 Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.
17 Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
18 Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
19 Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.
20 Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati.
21 Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
22 Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
23 Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
24 Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu.
25 Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.
26 Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.
27 Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako.
28 Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
29 Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako.
30 Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
31 Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe.
32 Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu.
33 Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho.
34 Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
35 Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo.
36 Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa.
37 Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.
38 Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako.
39 Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema.
40 Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako.
41 Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
42 Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako.
43 Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako.
44 Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele.
45 Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
46 Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu.
47 Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.
48 Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.
49 Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha.
50 Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.
51 Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako.
52 Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji.
53 Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako.
54 Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu.
55 Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako.
56 Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
57 Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.
58 Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.
59 Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.
60 Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.
61 Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.
62 Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.
63 Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.
64 Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.
65 Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.
66 Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.
67 Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako.
68 Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako.
69 Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.
70 Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako.
71 Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.
72 Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
73 Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.
74 Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako.
75 Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
76 Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
77 Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.
78 Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako.
79 Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako.
80 Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.
81 Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako.
82 Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji?
83 Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako.
84 Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?
85 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.
86 Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie.
87 Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako.
88 Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
89 Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele.
90 Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.
91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu.
93 Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha.
94 Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako.
95 Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako.
96 Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno.
97 Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
98 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote.
99 Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
100 Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.
101Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako.
102 Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.
103 Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.
104 Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
106Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.
107Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.
108 Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.
109 Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.
110 Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.
111 Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.
112 Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.
113 Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda.
114 Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea.
115 Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
116 Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
117 Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima.
118 Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo.
119 Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako.
121 Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
122 Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee.
123Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako.
124 Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.
125 Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako.
126 Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
127 Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
128 Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.
129 Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.
130 Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.
131 Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako.
132 Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.
133 Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki.
134 Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako.
135 Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.
136 Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako.
137 Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.
138 Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.
139 Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.
140 Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.
141 Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako.
142 Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.
143 Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu.
144 Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi.
145 Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako.
146 Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako.
147 Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.
148 Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako.
149 Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako.
150 Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako.
151 Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli.
152 Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele.
153 Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.
154 Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.
155 Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.
156 Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.
157 Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.
158 Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.
159 Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.
160 Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
161 Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.
162 Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi.
163 Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda.
164 Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.
165 Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.
166 Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda.
167 Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno.
168 Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.
169 Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako.
170 Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako.
171 Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.
172 Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki.
173 Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako.
174 Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.
175 Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie.
176 Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.
1 Katika shida yangu nalimlilia Bwana Naye akaniitikia.
2 Ee Bwana, uiponye nafsi yangu Na midomo ya uongo na ulimi wa hila.
3 Akupe nini, akuzidishie nini, Ewe ulimi wenye hila?
4 Mishale ya mtu hodari iliyochongoka, Pamoja na makaa ya mretemu.
5 Ole wangu mimi! Kwa kuwa nimekaa katika Mesheki; Na kufanya maskani yangu Katikati ya hema za Kedari.
6 Nafsi yangu imekaa siku nyingi, Pamoja naye aichukiaye amani.
7 Mimi ni wa amani; Bali ninenapo, wao huelekea vita.
1 Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
3 Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye;
4 Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.
5 Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
6 Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.
7 Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.
8 Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.
1 Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.
2 Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
3 Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana,
4 Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana; Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana.
5 Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya mbari ya Daudi.
6 Utakieni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao;
7 Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako.
8 Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe.
9 Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu, Nikutafutie mema.
1 Nimekuinulia macho yangu, Wewe uketiye mbinguni.
2 Kama vile macho ya watumishi Kwa mkono wa bwana zao Kama macho ya mjakazi Kwa mkono wa bibi yake; Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu, Hata atakapoturehemu.
3 Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi, Kwa maana tumeshiba dharau.
4 Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha, Na dharau ya wenye kiburi.
1 Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa,
2 Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia.
3 Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu
4 Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu;
5 Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.
6 Na ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao.
7 Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
8 Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi.
1 Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.
2 Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele.
3 Kwa maana fimbo ya udhalimu Haitakaa juu ya fungu la wenye haki; Wenye haki wasije wakainyosha Mikono yao kwenye upotovu.
4 Ee Bwana, uwatendee mema walio wema, Nao walio wanyofu wa moyo.
5 Bali wao wanaozigeukia njia zao zilizopotoka, Bwana atawaondoa pamoja na watenda maovu. Amani ikae na Israeli.
1 Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, Tulikuwa kama waotao ndoto.
2 Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu.
3 Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.
4 Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, Kama vijito vya Kusini.
5 Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha.
6 Ingawa mtu anakwenda zake akilia, Azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, Aichukuapo miganda yake.
1 Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.
2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi.
3 Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, Uzao wa tumbo ni thawabu.
4 Kama mishale mkononi mwa shujaa, Ndivyo walivyo wana wa ujanani.
5 Heri mtu yule Aliyelijaza podo lake hivyo. Naam, hawataona aibu Wanaposema na adui langoni.
1 Heri kila mtu amchaye Bwana, Aendaye katika njia yake.
2 Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema.
3 Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako.
4 Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
5 Bwana akubariki toka Sayuni; Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako;
6 Naam, ukawaone wana wa wanao. Amani ikae na Israeli.
1 Mara nyingi wamenitesa tangu ujana wangu, Israeli na aseme sasa,
2 Mara nyingi wamenitesa tangu ujana wangu, Lakini hawakuniweza.
3 Wakulima wamelima mgongoni mwangu, Wamefanya mirefu mifuo yao.
4 Bwana ndiye mwenye haki, Amezikata kamba zao wasio haki.
5 Na waaibishwe, warudishwe nyuma, Wote wanaoichukia Sayuni.
6 Na wawe kama majani ya darini Yanyaukayo kabla hayajamea.
7 Ambayo mvunaji haujazi mkono wake, Wala mfunga miganda kifua chake.
8 Wala hawasemi wapitao, Amani ya Bwana ikae nanyi, Twawabariki kwa jina la Bwana.
1 Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
2 Bwana, uisikie sauti yangu. Masikio yako na yaisikilize Sauti ya dua zangu.
3 Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
4 Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe.
5 Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja, Na neno lake nimelitumainia.
6 Nafsi yangu inamngoja Bwana, Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, Naam, walinzi waingojao asubuhi.
7 Ee Israeli, umtarajie Bwana; Maana kwa Bwana kuna fadhili, Na kwake kuna ukombozi mwingi.
8 Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote.
1 Bwana, moyo wangu hauna kiburi, Wala macho yangu hayainuki. Wala sijishughulishi na mambo makuu, Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.
2 Hakika nimeituliza nafsi yangu, Na kuinyamazisha. Kama mtoto aliyeachishwa Kifuani mwa mama yake; Kama mtoto aliyeachishwa, Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu.
3 Ee Israeli, umtarajie Bwana, Tangu leo na hata milele.
1 Bwana, umkumbukie Daudi Taabu zake zote alizotaabika.
2 Ndiye aliyemwapia Bwana, Akaweka nadhiri kwa Shujaa wa Yakobo.
3 Sitaingia hemani mwa nyumba yangu, Wala sitapanda matandiko ya kitanda changu;
4 Sitaacha macho yangu kuwa na usingizi, Wala kope zangu kusinzia;
5 Hata nitakapompatia Bwana mahali, Na Shujaa wa Yakobo maskani.
6 Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata, Katika konde la Yearimu tuliiona.
7 Na tuingie katika maskani yake, Tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake.
8 Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako, Wewe na sanduku la nguvu zako.
9 Makuhani wako na wavikwe haki, Watauwa wako na washangilie.
10 Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako, Usiurudishe nyuma uso wa masihi
11 Bwana amemwapia Daudi neno la kweli, Hatarudi nyuma akalihalifu, Baadhi ya wazao wa mwili wako Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
12 Wanao wakiyashika maagano yangu, Na shuhuda nitakazowafundisha; Watoto wao nao wataketi Katika kiti chako cha enzi milele.
13 Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni, Ameitamani akae ndani yake.
14 Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele, Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani.
15 Hakika nitavibariki vyakula vyake Wahitaji wake nitawashibisha chakula.
16 Na makuhani wake nitawavika wokovu, Na watauwa wake watashangilia.
17 Hapo nitamchipushia Daudi pembe, Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
18 Adui zake nitawavika aibu, Bali juu yake taji yake itasitawi.
1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.
2 Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake.
3 Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.
1 Tazama, enyi watumishi wa Bwana, Mhimidini Bwana, nyote pia. Ninyi mnaosimama usiku Katika nyumba ya Bwana.
2 Painulieni patakatifu mikono yenu, Na kumhimidi Bwana.
3 Bwana akubariki toka Sayuni, Aliyezifanya mbingu na nchi.
1 Haleluya. Lisifuni jina la Bwana, Enyi watumishi wa Bwana, sifuni.
2 Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu.
3 Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza.
4 Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa.
5 Maana najua mimi ya kuwa Bwana ni mkuu, Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote.
6 Bwana amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote.
7 Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika hazina zake.
8 Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama.
9 Alipeleka ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote.
10 Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu;
11 Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani.
12 Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake.
13 Ee Bwana, jina lako ni la milele, Bwana, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi.
14 Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumishi wake.
15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
16 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
17 Zina masikio lakini hazisikii, Wala hamna pumzi vinywani mwake.
18 Wazifanyao watafanana nazo, Na kila mmoja anayezitumainia.
19 Enyi mlango wa Israeli, mhimidini Bwana; Enyi mlango wa Haruni, mhimidini Bwana;
20 Enyi mlango wa Lawi, mhimidini Bwana; Ninyi mnaomcha Bwana, mhimidini Bwana.
21 Na ahimidiwe Bwana toka Sayuni, Akaaye Yerusalemu. Haleluya.
1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
3 Mshukuruni Bwana wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
4 Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
5 Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
6 Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
7 Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
8 Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
9 Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
10 Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
11 Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
12 Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
13 Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
14 Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
15 Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
16 Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
17 Yeye aliyewapiga wafalme wakuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
18 Akawaua wafalme mashuhuri; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
19 Sihoni, mfalme wa Waamori; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
20 Na Ogu, mfalme wa Bashani; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
21 Akaitoa nchi yao iwe urithi; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
22 Urithi wa Israeli mtumishi wake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
24 Akatuokoa na watesi wetu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
25 Kila chenye mwili akipa chakula chake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
26 Mshukuruni Mungu wa mbingu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.
1 Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
2 Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu.
3 Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.
4 Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?
5 Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau.
6 Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.
7 Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini!
8 Ee binti Babeli, uliye karibu na kuangamia, Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi.
9 Heri yeye atakayewakamata wadogo wako, Na kuwaseta wao juu ya mwamba.
1 Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
2 Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote.
3 Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
4 Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
5 Naam, wataziimba njia za Bwana, Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.
6 Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
7 Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
8 Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.
1 Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
2 Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
3 Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.
4 Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.
5 Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako.
6 Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.
7 Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;
10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.
13 Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
14 Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,
15 Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi;
16 Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.
17 Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!
18 Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.
19 Ee Mungu, laiti ungewafisha waovu! Enyi watu wa damu, ondokeni kwangu;
20 Kwa maana wakuasi kwa ubaya, Adui zako wakutaja jina lako bure.
21 Je! Bwana nisiwachukie wanaokuchukia? Nisikirihike nao wakuasio?
22 Nawachukia kwa ukomo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu.
23 Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
24 Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.
1 Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.
2 Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.
3 Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao.
4 Ee Bwana, unilinde na mikono ya mtu asiye haki; Unihifadhi na mtu wa jeuri; Waliowaza kuzipotosha hatua zangu.
5 Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando ya njia; Wameniwekea matanzi.
6 Nimemwambia Bwana, Ndiwe Mungu wangu; Ee Bwana, uisikie sauti ya dua zangu.
7 Ee MUNGU Bwana, nguvu za wokovu wangu, Umenifunika kichwa changu siku ya vita.
8 Ee Bwana, usimpe asiye haki tamaa zake, Usiifanikishe hila yake, wasije wakajiinua.
9 Nao wainuapo vichwa watu wanaonizunguka, Madhara ya midomo yao yawafunike.
10 Makaa ya moto yawaangukie, watupwe motoni, Na katika mashimo, wasipate kusimama tena.
11 Msingiziaji hatawekwa imara katika nchi, Mtu wa jeuri, uovu humwinda kumwangamiza.
12 Najua ya kuwa Bwana atamfanyia mnyonge hukumu, Na wahitaji haki yao.
13 Hakika wenye haki watalishukuru jina lako, Wenye adili watakaa mahali ulipo Wewe.
1 Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.
2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.
4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa.
5 Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.
6 Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.
7 Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.
8 Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.
9 Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu.
10 Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.
1 Kwa sauti yangu nitamlilia Bwana, Kwa sauti yangu nitamwomba Bwana dua.
2 Nitafunua mbele zake malalamiko yangu, Shida yangu nitaitangaza mbele zake.
3 Nilipozimia roho uliyajua mapito yangu; Katika njia niendayo wamenifichia mtego.
4 Utazame mkono wa kuume ukaone, Kwa maana sina mtu anijuaye. Makimbilio yamenipotea, Hakuna wa kunitunza roho.
5 Bwana, nimekuita nikasema, Ndiwe kimbilio langu, Fungu langu katika nchi ya walio hai.
6 Ukisikilize kilio changu, Kwa maana nimedhilika sana. Uniponye nao wanaonifuatia, Kwa maana wao ni hodari kuliko mimi.
7 Uitoe nafsi yangu kifungoni. Nipate kulishukuru jina lako. Wenye haki watanizunguka, Kwa kuwa Wewe unanikirimu.
1 Ee Bwana, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, Kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako.
2 Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.
3 Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani.
4 Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umesituka.
5 Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako.
6 Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame.
7 Ee Bwana, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni
8 Unifanye kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unijulishe njia nitakayoiendea, Kwa maana nakuinulia nafsi yangu.
9 Ee Bwana, uniponye na adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche.
10 Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze kwenye nchi sawa,
11 Ee Bwana, unihuishe kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni;
12 Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako.
1 Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.
2 Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu.
3 Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie?
4 Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho.
5 Bwana, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi.
6 Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe.
7 Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni.
8 Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.
9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
10 Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu.
11 Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo.
12 Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu.
13 Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu.
14 Ng'ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu.
15 Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye Bwana kuwa Mungu wao.
1 Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele.
2 Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele.
3 Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani.
4 Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu.
5 Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu.
6 Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako.
7 Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako.
8 Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
9 Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
10 Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
11 Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako.
12 Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
13 Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
14 Bwana huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.
15 Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake.
16 Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.
17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
18 Bwana yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu.
19 Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
20 Bwana huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza.
21 Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.
1 Haleluya. Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
2 Nitamsifu Bwana muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.
3 Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.
4 Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea.
5 Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
6 Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. Huishika kweli milele,
7 Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa;
8 Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki;
9 Bwana huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha.
10 Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.
1 Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
2 Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
3 Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao.
4 Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.
5 Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka.
6 Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri.
7 Mwimbieni Bwana kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi.
8 Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani.
9 Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.
10 Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mtu.
11 Bwana huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.
12 Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
13 Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, Amewabariki wanao ndani yako.
14 Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, Akushibishaye kwa unono wa ngano.
15 Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana.
16 Ndiye atoaye theluji kama sufu, Huimwaga barafu yake kama majivu,
17 Hutupa mvua ya mawe kama makombo, Mbele ya baridi yake ni nani awezaye kusimama?
18 Hulituma neno lake na kuviyeyusha, Huuvumisha upepo wake, maji yakatiririka.
19 Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake.
20 Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Haleluya.
1 Haleluya. Msifuni Bwana kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote.
3 Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga.
4 Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu.
5 Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.
6 Amevithibitisha hata milele na milele, Ametoa amri wala haitapita.
7 Msifuni Bwana kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote.
8 Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake.
9 Milima na vilima vyote, Miti yenye matunda na mierezi yote.
10 Hayawani, na wanyama wafugwao, Vitambaavyo, na ndege wenye mbawa.
11 Wafalme wa dunia, na watu wote, Wakuu, na makadhi wote wa dunia.
12 Vijana waume, na wanawali, Wazee, na watoto;
13 Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu.
14 Naye amewainulia watu wake pembe, Sifa za watauwa wake wote; Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. Haleluya.
1 Haleluya. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
2 Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya, Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
3 Na walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa matari na kinubi wamwimbie.
4 Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
5 Watauwa na waushangilie utukufu, Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
6 Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao, Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.
7 Ili kufanya kisasi juu ya mataifa, Na adhabu juu ya kabila za watu.
8 Wawafunge wafalme wao kwa minyororo, Na wakuu wao kwa pingu za chuma.
9 Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa; Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Haleluya.
1 Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake.
2 Msifuni kwa matendo yake makuu; Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
3 Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;
4 Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;
5 Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
6 Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.