Mithali

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31

Mithali 1


1 Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.
2 Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu;
3 kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili.
4 Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari;
5 mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.
6 Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao.
7 Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.
8 Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,
9 Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako.
10 Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.
11 Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu;
12 Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni.
13 Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka.
14 Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika.
15 Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.
16 Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu.
17 Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege ye yote.
18 Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe.
19 Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo.
20 Hekima hupaza sauti yake katika njia kuu, Hutoa sauti yake katika viwanja;
21 Hulia penye mikutano mikubwa ya watu, Mahali pa kuyaingilia malango, Ndani ya mji hutamka maneno yake.
22 Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa?
23 Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.
24 Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;
25 Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu;
26 Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo;
27 Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.
28 Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.
29 Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.
30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.
31 Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.
32 Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.
33 Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.

Mithali 2


1 Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;
2 Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;
3 Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;
4 Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;
5 Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.
6 Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;
7 Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;
8 Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.
9 Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.
10 Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;
11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.
12 Ili kukuokoa na njia ya uovu, Na watu wanenao yaliyopotoka;
13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;
14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;
15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao.
16 Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;
17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.
18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.
19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima.
20 Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.
21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.
22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang'olewa.

Mithali 3


1 Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.
2 Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.
3 Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.
8 Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.
9 Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.
11 Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye.
12 Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
13 Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.
14 Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.
15 Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.
16 Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.
17 Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani.
18 Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.
19 Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;
20 Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande.
21 Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara.
22 Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako.
23 Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa.
24 Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.
25 Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.
26 Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
27 Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.
28 Usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe.
29 Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.
30 Usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote.
31 Usimhusudu mtu mwenye jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake.
32 Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri yake ni pamoja na wanyofu.
33 Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.
34 Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.
35 Wenye hekima wataurithi utukufu, Bali kukuzwa kwa wapumbavu ni fedheha.

Mithali 4


1 Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu.
2 Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu.
3 Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu.
4 Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi.
5 Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.
6 Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda.
7 Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.
8 Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia.
9 Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri.
10 Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
11 Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu.
12 Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa.
13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.
14 Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya.
15 Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako.
16 Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu.
17 Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri.
18 Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu.
19 Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho.
20 Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu.
21 Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako.
22 Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.
23 Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
24 Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.
25 Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.
26 Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike;
27 Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.

Mithali 5


1 Mwanangu, sikiliza hekima yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu;
2 Upate kuilinda busara, Na midomo yako iyahifadhi maarifa.
3 Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
4 Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni mkali kama upanga wa makali kuwili.
5 Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu;
6 Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.
7 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala msiache maneno ya kinywa changu.
8 Itenge njia yako mbali naye, Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
9 Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako;
10 Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;
11 Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho, Nyama yako na mwili wako utakapoangamia;
12 Ukasema, Jinsi nilivyochukia maonyo, Na moyo wangu ukadharau kukemewa;
13 Wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu, Wala sikuwategea sikio langu walionifundisha!
14 Nalikuwa karibu na kuingia katika maovu yote, Katikati ya mkutano na kusanyiko.
15 Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako.
16 Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu?
17 Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe.
18 Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako.
19 Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima.
20 Mwanangu! Mbona unashangilia malaya, Na kukikumbatia kifua cha mgeni?
21 Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana, Na mienendo yake yote huitafakari.
22 Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake.
23 Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.

Mithali 6


1 Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepana mikono,
2 Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,
3 Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako.
4 Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia.
5 Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.
6 Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima.
7 Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu,
8 Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
9 Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?
10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!
11 Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.
12 Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu.
13 Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake.
14 Mna upotofu moyoni mwake, hutunga uovu daima, Hupanda mbegu za magomvi.
15 Basi msiba utampata kwa ghafula; Ghafula atavunjika, bila njia ya kupona.
16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.
17 Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;
18 Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;
19 Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.
20 Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako.
21 Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako.
22 Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe.
23 Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima.
24 Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni.
25 Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake.
26 Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani
27 Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe?
28 Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue?
29 Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia.
30 Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa;
31 Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake.
32 Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake.
33 Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.
34 Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipiza kisasi.
35 Hatakubali ukombozi uwao wote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi.

Mithali 7


1 Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako.
2 Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako.
3 Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4 Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke.
5 Wapate kukulinda na malaya, Na mgeni akubembelezaye kwa maneno yake.
6 Maana katika dirisha la nyumba yangu Nalichungulia katika shubaka yake;
7 Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili,
8 Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake,
9 Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani.
10 Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;
11 Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake.
12 Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia.
13 Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya,
14 Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu;
15 Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona.
16 Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari.
17 Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini.
18 Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.
19 Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali;
20 Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu.
21 Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.
22 Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;
23 Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.
24 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.
25 Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake.
26 Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, jumla ya waliouawa naye ni jeshi kubwa.
27 Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.

Mithali 8


1 Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?
2 Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo.
3 Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, Mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.
4 Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu.
5 Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.
6 Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili.
7 Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu.
8 Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.
9 Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.
10 Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi.
11 Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.
12 Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; Natafuta maarifa na busara.
13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.
14 Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu.
15 Kwa msaada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki.
16 Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.
17 Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18 Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.
19 Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule.
20 Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu.
21 Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.
22 Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale.
23 Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia.
24 Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji.
25 Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa.
26 Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde Wala chanzo cha mavumbi ya dunia;
27 Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari;
28 Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu;
29 Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi;
30 Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake;
31 Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.
32 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; Maana heri hao wazishikao amri zangu.
33 Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae.
34 Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri sikuzote malangoni pangu, Akingoja penye vizingiti vya milango yangu.
35 Maana yeye anionaye mimi aona uzima, Naye atapata kibali kwa Bwana.
36 Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, Na wao wanichukiao hupenda mauti.

Mithali 9


1 Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba;
2 Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia.
3 Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana,
4 Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
5 Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya.
6 Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.
7 Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu.
8 Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda.
9 Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu;
10 Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.
11 Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa.
12 Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako.
13 Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.
14 Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,
15 Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao.
16 Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
17 Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.
18 Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.

Mithali 10


1 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.
2 Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti.
3 Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.
4 Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.
5 Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
6 Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.
7 Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.
8 Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
9 Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.
10 Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
11 Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,
12 Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.
13 Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.
14 Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.
15 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.
16 Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.
17 Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa.
18 Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.
19 Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.
20 Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.
21 Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.
22 Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.
23 Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.
24 Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.
25 Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
26 Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.
27 Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
28 Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.
29 Njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.
30 Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.
31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.
32 Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

Mithali 11


1 Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.
2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.
3 Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.
4 Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.
5 Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.
6 Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.
7 Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.
8 Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.
9 Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.
10 Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.
11 Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.
12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.
13 Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.
14 Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.
15 Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.
16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.
17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake.
18 Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.
19 Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.
20 Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.
21 Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka.
22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.
23 Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.
24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.
25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.
26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.
27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.
28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.
29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.
30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.
31 Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?

Mithali 12


1 Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.
2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.
3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.
4 Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.
5 Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.
6 Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.
7 Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.
8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.
9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.
10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.
11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.
12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.
13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.
15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.
16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.
17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.
24 Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.
25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.
26 Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.
27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.
28 Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.

Mithali 13


1 Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2 Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.
3 Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.
4 Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.
5 Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.
6 Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.
7 Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.
8 Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.
9 Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
10 Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.
11 Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.
13 Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.
14 Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.
15 Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza.
16 Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu.
17 Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya.
18 Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.
19 Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.
20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.
21 Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema.
22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.
23 Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.
24 Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.
25 Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.

Mithali 14


1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
2 Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.
3 Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.
4 Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.
5 Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.
6 Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate; Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.
7 Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.
8 Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9 Wapumbavu huidharau hatia; Bali upo upendeleo kwa wenye haki.
10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake.
11 Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.
12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
13 Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.
14 Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.
15 Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.
16 Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.
17 Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.
18 Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.
19 Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.
20 Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi.
21 Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri.
22 Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.
23 Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.
24 Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.
25 Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya.
26 Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio.
27 Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.
28 Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.
29 Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.
30 Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa.
31 Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.
32 Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.
33 Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.
34 Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.
35 Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.

Mithali 15


1 Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.
2 Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.
3 Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.
4 Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.
5 Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.
6 Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.
7 Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.
8 Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.
9 Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.
10 Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.
11 Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?
12 Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.
13 Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.
14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.
15 Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.
16 Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.
17 Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.
18 Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.
19 Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.
20 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.
21 Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.
22 Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.
23 Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!
24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.
25 Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.
26 Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.
27 Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.
28 Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.
29 Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.
30 Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.
31 Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.
32 Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.
33 Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

Mithali 16


1 Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.
2 Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huzipima roho za watu.
3 Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.
4 Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.
5 Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu.
6 Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu.
7 Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye.
8 Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake.
10 Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme; Kinywa chake hakitakosa katika hukumu.
11 Mizani ya haki na vitanga vyake ni vya Bwana; Mawe yote ya mfukoni ni kazi yake.
12 Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo; Maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki.
13 Midomo ya haki ni furaha ya wafalme; Nao humpenda yeye asemaye yaliyo sawa.
14 Hasira ya mfalme ni kama wajumbe wa mauti; Lakini mtu mwenye hekima ataituliza.
15 Kuna uhai katika nuru ya uso wa mfalme, Na fadhili zake ni kama wingu la masika.
16 Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.
17 Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake.
18 Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.
19 Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.
20 Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye Bwana ana heri.
21 Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara; Utamu wa maneno huongeza elimu.
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao; Bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao.
23 Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake.
24 Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani.
25 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
26 Nafsi yake mfanya kazi hujifanyia kazi; Maana kinywa chake humtia bidii.
27 Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao.
28 Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki.
29 Mtu mkali humshawishi mwenzake; Humwongoza katika njia isiyo njema.
30 Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; Aikazaye midomo yake hutokeza mabaya.
31 Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki.
32 Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.
33 Kura hutupwa katika mikunjo ya nguo; Lakini hukumu zake zote ni za Bwana.

Mithali 17


1 Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.
2 Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.
3 Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali Bwana huijaribu mioyo.
4 Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara.
5 Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu.
6 Wana wa wana ndio taji ya wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao.
7 Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.
8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa.
9 Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki.
10 Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.
11 Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.
12 Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.
13 Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.
14 Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.
15 Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa Bwana.
16 Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu?
17 Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
18 Aliyepungukiwa na akili hupana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini mbele ya mwenzake.
19 Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu.
20 Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotofu huanguka katika misiba.
21 Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha.
22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.
23 Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu.
24 Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia.
25 Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa.
26 Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si kwema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao.
27 Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara.
28 Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.

Mithali 18


1 Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.
2 Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu.
3 Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama.
4 Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima.
5 Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni.
6 Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo.
7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake.
8 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.
9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu.
10 Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.
11 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.
12 Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.
13 Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.
14 Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?
15 Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.
16 Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.
17 Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.
18 Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu.
19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.
20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.
21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.
22 Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana.
23 Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali.
24 Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.

Mithali 19


1 Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu.
2 Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi.
3 Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya Bwana.
4 Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake.
5 Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka.
6 Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.
7 Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka.
8 Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema.
9 Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia.
10 Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu.
11 Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa.
12 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani.
13 Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.
14 Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.
15 Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.
16 Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa.
17 Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.
18 Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.
19 Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena.
20 Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho.
21 Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.
22 Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.
23 Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya.
24 Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka kinywani pake.
25 Mpige mwenye mzaha, na mjinga atapata busara; Mwonye mwenye ufahamu, naye atatambua maarifa.
26 Apotezaye mali za babaye na kumfukuza mamaye, Ni mwana aaibishaye, na kuleta lawama.
27 Mwanangu, acha kusikia mafundisho, Ukitaka tu kuyaasi maneno ya maarifa.
28 Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu.
29 Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu.

Mithali 20


1 Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima.
2 Utisho wa mfalme ni kama ngurumo ya simba; Amkasirishaye huitendea dhambi nafsi yake.
3 Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana.
4 Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu.
5 Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; Lakini mtu mwenye ufahamu atayateka.
6 Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata?
7 Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake.
8 Mfalme aketiye katika kiti cha hukumu, Huyapepeta mabaya yote kwa macho yake.
9 Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu?
10 Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali, Vyote viwili ni chukizo kwa Bwana.
11 Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili.
12 Sikio lisikialo, na jicho lionalo, Bwana ndiye aliyeyafanya yote mawili.
13 Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.
14 Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu.
15 Dhahabu iko, na marijani tele; Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani.
16 Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni.
17 Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe.
18 Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita.
19 Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana.
20 Amlaaniye babaye au mamaye, Taa yake itazimika katika giza kuu.
21 Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa.
22 Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa.
23 Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa Bwana; Tena mizani ya hila si njema.
24 Mwenendo wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?
25 Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari.
26 Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki; Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao.
27 Pumzi ya mwanadamu ni taa ya Bwana; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake.
28 Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme, Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili.
29 Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi.
30 Machubuko ya fimbo husafisha uovu, Na mapigo hufikilia ndani ya mtima.

Mithali 21


1 Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.
2 Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo.
3 Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka.
4 Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi.
5 Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.
6 Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.
7 Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.
8 Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.
9 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
10 Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake.
11 Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.
12 Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.
13 Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.
14 Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.
15 Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.
16 Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa.
17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.
18 Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.
19 Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.
20 Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.
21 Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima.
22 Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.
23 Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.
24 Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.
25 Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.
26 Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.
27 Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!
28 Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.
29 Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.
30 Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana.
31 Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.

Mithali 22


1 Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu.
2 Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili.
3 Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.
4 Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.
5 Miiba na mitego huwa katika njia ya mshupavu; Yeye aitunzaye nafsi yake atakuwa mbali nayo.
6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.
7 Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.
8 Yeye apandaye uovu atavuna msiba, Na fimbo ya ghadhabu yake itakoma.
9 Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake.
10 Mtupe nje mwenye dharau, na ugomvi utatoka; Naam, fitina na fedheha zitakoma.
11 Apendaye usafi wa moyo, na neema ya midomo; Mfalme atakuwa rafiki yake.
12 Macho ya Bwana humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini.
13 Mtu mvivu husema, Simba yuko nje; Nitauawa katika njia kuu.
14 Kinywa cha malaya ni shimo refu; Anayechukiwa na Bwana atatumbukia ndani yake.
15 Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.
16 Yeye awaoneaye maskini ili kuongeza mapato, Naye ampaye tajiri, hupata hasara.
17 Tega sikio lako uyasikie maneno ya wenye hekima, na kuuelekeza moyo wako kwa maarifa yangu;
18 maana ni vizuri kuyahifadhi ndani yako, hali yakithibitika pamoja midomoni mwako.
19 Ili matumaini yako uyaweke kwa Bwana, leo nimekujulisha wewe haya, naam, wewe.
20 Je! Sikukuandikia mambo makuu juu ya mashauri na juu ya maarifa;
21 ili kukujulisha hakika ya maneno ya kweli, uwarudishie wakutumao maneno ya kweli?
22 Usimnyang'anye maskini, kwa kuwa ni maskini; Wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni;
23 Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka.
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi;
25 Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego.
26 Usiwe mmoja wao wawekao rehani; Au walio wadhamini kwa deni za watu;
27 Kama huna kitu cha kulipa; Kwani ukaondolee kitanda chako chini yako?
28 Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani, Uliowekwa na baba zako.
29 Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.

Mithali 23


1 Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala, Mwangalie sana yeye aliye mbele yako.
2 Tena ujitie kisu kooni, Kama ukiwa mlafi.
3 Usivitamani vyakula vyake vya anasa; Kwa maana ni vyakula vya hila.
4 Usijitaabishe ili kupata utajiri; Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe.
5 Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni.
6 Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa;
7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.
8 Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea.
9 Usiseme masikioni mwa mpumbavu; Maana atadharau hekima ya maneno yako.
10 Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani; Wala usiingie katika mashamba ya yatima;
11 Kwa sababu mkombozi wao ana nguvu; Atawatetea juu yako.
12 Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa.
13 Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.
14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu.
15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima, Moyo wangu utafurahi, naam, moyo wangu;
16 Naam, viuno vyangu vitafurahi, Midomo yako inenapo maneno mema.
17 Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi; Bali mche Bwana mchana kutwa;
18 Maana bila shaka iko thawabu; Na tumaini lako halitabatilika.
19 Sikia, mwanangu, uwe na hekima, Na kuuongoza moyo wako katika njia njema.
20 Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa.
21 Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu.
22 Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee.
23 Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu.
24 Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia.
25 Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa.
26 Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.
27 Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.
28 Naam, huotea kama mnyang'anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu.
29 Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu?
30 Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika.
31 Usiitazame mvinyo iwapo ni nyekundu; Iitiapo bilauri rangi yake, ishukapo taratibu;
32 Mwisho wake huuma kama nyoka; Huchoma kama fira.
33 Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka.
34 Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari; Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti.
35 Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; Wamenipiga wala sina habari; Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena.

Mithali 24


1 Usiwahusudu watu waovu, Wala usitamani kuwa pamoja nao;
2 Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma, Na midomo yao huongea madhara.
3 Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika,
4 Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.
5 Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;
6 Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.
7 Kwa mpumbavu hekima haipatikani; Hafumbui kinywa chake langoni.
8 Mtu afikiriye kutenda maovu, Watu watamwita mtundu;
9 Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.
10 Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.
11 Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.
12 Ukisema, Sisi hatukujua hayo; Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye? Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye? Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?
13 Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo.
14 Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika.
15 Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki; Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika;
16 Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.
17 Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;
18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake.
19 Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya;
20 Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika.
21 Mwanangu, mche Bwana, na mfalme; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;
22 Maana msiba wao utatokea kwa ghafula; Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao.
23 Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili. Kupendelea watu katika hukumu si kwema.
24 Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki; Kabila za watu watamlaani, taifa watamchukia.
25 Bali kwao wakemeao furaha itakuwako; Na baraka ya kufanikiwa itawajilia.
26 Aibusu midomo atoaye jawabu la haki.
27 Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.
28 Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu, Wala usidanganye kwa midomo yako.
29 Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake.
30 Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.
31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.
32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.
33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi!
34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.

Mithali 25


1 Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili.
2 Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.
3 Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.
4 Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;
5 Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki.
6 Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme; Wala usisimame mahali pa watu wakuu;
7 Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho,
8 Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.
9 Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;
10 Yeye asikiaye asije akakutukana; Na aibu yako isiondoke.
11 Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.
12 Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.
13 Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno; Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao; Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.
14 Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.
15 Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa; Na ulimi laini huvunja mfupa.
16 Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; Usije ukashiba na kuitapika.
17 Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia.
18 Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali.
19 Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka.
20 Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi.
21 Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa;
22 Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu.
23 Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu.
24 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
25 Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali.
26 Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa.
27 Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu.
28 Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.

Mithali 26


1 Kama theluji wakati wa joto, na mvua wakati wa mavuno; Kadhalika heshima haimpasi mpumbavu.
2 Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.
3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, Na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu.
4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.
5 Umjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Asije akawa mwenye hekima machoni pake.
6 Apelekaye ujumbe kwa mkono wa mpumbavu Hujikata miguu, na kunywa hasara.
7 Miguu yake achechemeaye huwa dhaifu; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.
8 Kama mfuko wa vito katika chungu ya mawe; Kadhalika mtu amheshimuye mpumbavu.
9 Kama mwiba uingiao katika mkono wa mlevi; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.
10 Fundi stadi hufanyiza vitu vyote; Bali amwajiriye mpumbavu ni kama awaajiriye watu wapitao.
11 Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika mpumbavu afanya upumbavu tena.
12 Je! Wamwona mtu mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
13 Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu.
14 Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake.
15 Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake.
16 Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, Kuliko watu saba wawezao kutoa sababu.
17 Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; Ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake.
18 Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti;
19 Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu?
20 Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.
21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, Na kama kuni juu ya moto; Ndivyo mtu mgomvi achocheavyo uadui.
22 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.
23 Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha.
24 Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake.
25 Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake.
26 Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko.
27 Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.
28 Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

Mithali 27


1 Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.
2 Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.
3 Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili.
4 Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu.
5 Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika.
6 Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana.
7 Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.
8 Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake.
9 Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake.
10 Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali.
11 Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye.
12 Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.
13 Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya.
14 Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.
15 Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;
16 Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta.
17 Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.
18 Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.
19 Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake.
20 Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi.
21 Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake.
22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka.
23 Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako.
24 Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi?
25 Manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana, Na maboga ya milimani hukusanyika.
26 Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba
27 Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.

Mithali 28


1 Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2 Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa
3 Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.
4 Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao.
5 Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote.
6 Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.
7 Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.
8 Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.
9 Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo.
10 Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema.
11 Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.
12 Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha.
13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.
14 Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.
15 Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.
16 Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.
17 Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.
18 Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.
19 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.
20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.
21 Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.
22 Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.
23 Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.
24 Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.
25 Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa.
26 Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.
27 Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.
28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

Mithali 29


1 Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.
2 Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.
3 Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.
4 Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.
5 Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.
6 Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya; Bali mwenye haki huimba na kufurahi.
7 Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.
8 Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.
9 Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.
10 Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu; Bali wenye haki humtunza nafsi yake.
11 Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.
12 Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.
13 Maskini na mdhalimu hukutana pamoja; Bwana huwatia nuru macho yao wote wawili.
14 Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu; Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.
15 Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.
16 Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.
17 Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako.
18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
19 Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno; Maana ajapoyafahamu hataitika.
20 Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
21 Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.
22 Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.
23 Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.
24 Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe; Asikia maapizo, wala hana neno.
25 Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.
26 Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu; Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa Bwana
27 Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki; Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.

Mithali 30


1 Maneno ya Aguri bin Yake; mausia mtu huyu aliyomwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.
2 Hakika nimekuwa kama mnyama, wala si mtu; Wala sina ufahamu wa mwanadamu;
3 Wala sikujifunza hekima; Wala sina maarifa ya kumjua Mtakatifu.
4 Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini? Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake? Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?
5 Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.
6 Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.
7 Mambo haya mawili nimekuomba; Usininyime [matatu] kabla sijafa.
8 Uniondolee ubatili na uongo; Usinipe umaskini wala utajiri; Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.
9 Nisije nikashiba nikakukana, Nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana nikaiba, Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.
10 Usimchongee mtumwa kwa bwana wake; Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.
11 Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao; Wala hawambariki mama yao.
12 Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao.
13 Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana.
14 Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.
15 Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!
16 Kuzimu; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!
17 Jicho la mtu amdhihakiye babaye, Na kudharau kumtii mamaye; Kunguru wa bondeni wataling'oa, Na vifaranga vya tai watalila.
18 Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu, Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.
19 Mwendo wa tai katika hewa; Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba; Mwendo wa merikebu katikati ya bahari; Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.
20 Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu; Hula, akapangusa kinywa chake, Akasema, Sikufanya uovu.
21 Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka, Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia.
22 Mtumwa apatapo kuwa mfalme; Mpumbavu ashibapo chakula;
23 Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo; Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.
24 Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana.
25 Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari.
26 Wibari ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba.
27 Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi.
28 Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme.
29 Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri.
30 Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;
31 Jimbi aendaye tambo; na beberu; Na mfalme ambaye haasiki.
32 Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako.
33 Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.

Mithali 31


1 Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake.
2 Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?
3 Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.
4 Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?
5 Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.
6 Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini.
7 Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake.
8 Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao;
9 Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao.
10 Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.
11 Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.
12 Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.
13 Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
14 Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali.
15 Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.
16 Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
17 Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu.
18 Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku.
19 Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
20 Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.
21 Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
22 Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
23 Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.
24 Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.
25 Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.
26 Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.
27 Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.
28 Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema,
29 Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.
30 Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.
31 Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.