Mhubiri

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12

Mhubiri 1


1 Maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi,mfalme katika Yerusalemu.
2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili.
3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?
4 Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima.
5 Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake.
6 Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.
7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena.
8 Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia.
9 Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua.
10 Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi.
11 Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.
12 Mimi, Mhubiri, nalikuwa Mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
13 Nikatia moyo wangu ili kuyatafuta yote yanayotendeka chini ya mbingu, na kuyavumbua kwa hekima; ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
14 Nimeziona kazi zote zifanywazo chini ya jua; na, tazama, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
15 Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki.
16 Nikatafakari nikisema, Nimejipatia hekima nyingi kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; naam, moyo wangu umeona kwa wingi hekima na maarifa.
17 Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.
18 Yaani, Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni,Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko.

Mhubiri 2


1 Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.
2 Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?
3 Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.
4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;
5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.
7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;
8 tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.
10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.
11 Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
12 Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa.
13 Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza;
14 macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa.
15 Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16 Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!
17 Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
18 Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.
19 Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili.
20 Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua.
21 Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu.
22 Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua?
23 Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili.
24 Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo naliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu.
25 Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi?
26 Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.

Mhubiri 3


1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
2 Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa;
3 Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
4 Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;
5 Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
6 Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;
7 Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;
8 Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.
9 Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?
10 Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake.
11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.
12 Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi, na kufanya mema maadamu wanaishi.
13 Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote.
14 Najua ya kwamba kila kazi aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye.
15 Yale yaliyoko yamekuwako; na hayo yatakayokuwako yamekwisha kuwako; naye Mungu huyatafuta tena mambo yale yaliyopita.
16 Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu.
17 Nikasema moyoni mwangu, Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki; kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi.
18 Nikasema moyoni mwangu, Ni kwa sababu ya wanadamu, ili Mungu awajaribu, nao waone ya kuwa wao wenyewe wafanana na wanyama.
19 Kwa maana linalowatukia wanadamu linawatukia wanyama; jambo moja lawatukia; anavyokufa huyu ndivyo anavyokufa huyu; naam, wote wanayo pumzi moja; wala mwanadamu hana kitu cha kumpita mnyama; kwa maana yote ni ubatili.
20 Wote huendea mahali pamoja; wote hutoka katika mavumbi; na hata mavumbini hurudi tena.
21 Ni nani ajuaye kama roho ya binadamu huenda juu, na kama roho ya mnyama huenda chini?
22 Hivyo nikaona ya kwamba hakuna jema kupita mwanadamu kuzifurahia kazi zake; kwa sababu hili ni fungu lake; kwa maana ni nani atakayemrudisha tena ili ayaone yatakayomfuata baadaye.

Mhubiri 4


1 Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.
2 Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado;
3 naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua.
4 Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.
5 Mpumbavu huikunja mikono yake, Naye hula chakula chake mwenyewe;
6 Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo.
7 Kisha nikarudi tena, na kuona ubatili chini ya jua.
8 Kuna mtu aliye peke yake, wala hana wa pili wake; naam, hana mwana wala ndugu; hata hivyo amali yake haina mwisho, wala macho yake hayashibi utajiri. Basi asema, Ni kwa ajili ya nani nafanya kazi, na kujinyima nafsi yangu mema? Hayo nayo ni ubatili, naam, ni taabu kubwa.
9 Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.
10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!
11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?
12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.
13 Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu.
14 Kwa maana kutoka gerezani alikuja kumiliki; naam, hata katika ufalme wake alizaliwa hali ya umaskini.
15 Nikawaona wote walio hai waendao chini ya jua, ya kwamba walishikamana na huyo kijana, huyo wa pili aliyesimama badala ya yule.
16 Hawakuwa na kikomo hao watu wote, hao wote ambao alikuwa juu yao; lakini hata hivyo wale wafuatao baada yake hawatamfurahia. Hakika hayo pia ni ubatili, na kujilisha upepo.

Mhubiri 5


1 Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya.
2 Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache.
3 Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno.
4 Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.
5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe.
6 Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba umepitiliwa; kwani Mungu akukasirikie sauti yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako?
7 Maana ndivyo ilivyo katika habari za wingi wa ndoto, na ubatili, na maneno mengi; walakini wewe umche Mungu.
8 Ujapokuwa unaona maskini kuonewa, na hukumu na haki kuondolewa kwa jeuri katika jimbo, usilistaajabie jambo hilo; kwa sababu, Aliye juu kuliko walio juu huangalia; Tena wako walio juu kupita hao.
9 Lakini, pamoja na hayo, manufaa ya nchi kwa kila njia ni mfalme anayejibidiisha kwa ajili ya shamba.
10 Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili.
11 Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?
12 Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.
13 Kuna na balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima;
14 na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake.
15 Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake.
16 Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo?
17 Siku zake zote hula gizani, mwenye fadhaa nyingi, mwenye ugonjwa na uchungu.
18 Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake.
19 Tena, kwa habari za kila mwanadamu, ambaye Mungu amempa mali na ukwasi, akamwezesha kula katika hizo, na kuipokea sehemu yake, na kuifurahia amali yake; hiyo ndiyo karama ya Mungu.
20 Kwa kuwa mtu hatazikumbuka mno siku za maisha yake; kwa sababu Mungu humtakabali katika furaha ya moyo wake.

Mhubiri 6


1 Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito;
2 mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu cho chote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani walakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya.
3 Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo;
4 yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza;
5 tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule;
6 naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja?
7 Kazi yote ya binadamu ni kwa kinywa chake, Walakini hata hivyo nafsi yake hashibi.
8 Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai?
9 Heri kuona kwa macho, Kuliko kutanga-tanga kwa tamaa. Hayo nayo ni ubatili, na kujilisha upepo.
10 Na awe kitu cho chote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe.
11 Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini?
12 Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua?

Mhubiri 7


1 Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.
2 Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.
3 Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.
4 Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.
5 Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;
6 Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili.
7 Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu.
8 Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.
9 Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.
10 Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo.
11 Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua.
12 Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.
13 Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?
14 Siku ya kufanikiwa ufurahi, Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lo lote litakalofuata baada yake.
15 Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.
16 Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?
17 Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?
18 Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.
19 Hekima ni nguvu zake mwenye hekima, Zaidi ya wakuu kumi waliomo mjini.
20 Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.
21 Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.
22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine.
23 Mambo hayo yote mimi nimeyahakikisha katika hekima. Nilisema, Mimi nitakuwa na hekima, lakini imefarakana nami.
24 Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?
25 Nikageuka, na moyo wangu ulikazwa katika kujua na kupeleleza, na kuitafuta hekima, na maana ya mambo yaliyoko; ili nifahamu ya kuwa uovu ni upumbavu, na upumbavu ni wazimu.
26 Nami nimeona lililo na uchungu kupita mauti; yaani, mwanamke ambaye moyo wake ni mitego na tanzi, na mikono yake ni kama vifungo; yeye ampendezaye Mungu atamponyoka, bali mwenye dhambi atanaswa na yeye.
27 Tazama, asema Mhubiri, mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha hili na hili, ili kuitafuta jumla;
28 ambayo bado nafsi yangu nikali nikiitafuta, nisiione; mwanamume mmoja katika elfu nimemwona; bali mwanamke mmoja miongoni mwa wote mimi sikumwona.
29 Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi.

Mhubiri 8


1 Ni nani aliye kama mwenye hekima; Naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humng'ariza uso wake, Na ugumu wa uso wake hubadilika.
2 Mimi nasema hivi, Uishike amri ya mfalme; na hiyo kwa sababu umeapa kwa Mungu.
3 Usifanye haraka kutoka mbele ya uso wake; usiendelee kufanya lililo baya; maana yeye hufanya lo lote limpendezalo.
4 Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu; naye ni nani awezaye kumwambia huyo, Wafanya nini?
5 Aishikaye amri hatajua neno baya; Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu.
6 Kwa maana kwa kila shauri kuna wakati na hukumu; kwa sababu mashaka ya mwanadamu yaliyo juu yake ni makubwa;
7 kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa?
8 Hakuna mwenye uwezo juu ya roho aizuie roho; Wala hana mamlaka juu ya siku ya kufa; Wala hakuna kuruhusiwa katika vita vile; Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea.
9 Mambo hayo yote nimeyaona, nikatia moyo wangu katika kila kazi iliyofanyika chini ya jua. Kuna wakati ambapo mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasira yake.
10 Pia nikaona waovu wamezikwa, nao wamefika kaburini; tena waliofanya mema wameondoka katika patakatifu, nao wamesahauliwa mjini. Hayo nayo ni ubatili.
11 Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.
12 Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake;
13 walakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu.
14 Kuna ubatili unaofanyika juu ya nchi, kwamba wako wenye haki nao wapatilizwa kama kwa kazi yao waovu; tena wako waovu, nao wapatilizwa kama kwa kazi yao wenye haki. Nami nikasema ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
15 Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka; na yakuwa hilo likae naye katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.
16 Mimi nilipotia moyo wangu katika kuijua hekima, na kuuona utumishi uliofanyika juu ya nchi, (maana kuna asiyepata usingizi kwa macho yake mchana wala usiku);
17 basi, niliiona kazi yote ya Mungu, ya kuwa haitafutikani na mwanadamu kazi inayofanyika chini ya jua; kwa sababu mwanadamu na akijisumbua kadiri awezavyo kuitafuta, hata hivyo hataiona; naam, zaidi ya hayo, mwenye hekima ajapodhania ya kuwa ataijua, lakini yeye hataweza kuiona.

Mhubiri 9


1 Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyatafuta-tafuta haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; kwamba ni pendo au kwamba ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita.
2 Mambo yote yawatukia wote sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo.
3 Baa hilo ni katika mambo yote yanayofanyika chini ya jua, ya kuwa wote wanalo tukio moja; naam, zaidi ya hayo, mioyo ya wanadamu imejaa maovu, na wazimu umo mioyoni mwao wakati walipo hai, na baadaye huenda kwa wafu.
4 Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa);
5 kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.
6 Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.
7 Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako.
8 Mavazi yako na yawe meupe sikuzote; wala kichwa chako kisikose marhamu.
9 Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.
10 Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.
11 Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.
12 Maana mwanadamu naye hajui wakati wake; kama samaki wanaokamatwa katika nyavu mbaya, na mfano wa ndege wanaonaswa mtegoni, kadhalika wanadamu hunaswa katika wakati mbaya, unapowaangukia kwa ghafula.
13 Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa.
14 Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga.
15 Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini.
16 Ndipo niliposema, Bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.
17 Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu.
18 Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.

Mhubiri 10


1 Mainzi mafu huvundisha marhamu ya mwuza marashi; Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima.
2 Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume; Bali moyo wake mpumbavu upo mkono wa kushoto.
3 Naam, huyo mpumbavu tena, aendapo njiani, hupungukiwa na fahamu zake; hata humwambia kila mtu ya kuwa yeye ni mpumbavu.
4 Roho yake mtawala ikiinuka kinyume chako, Usiondoke mara mahali pako ulipo; Kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo yaliyo makubwa.
5 Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye;
6 ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini.
7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.
8 Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.
9 Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.
10 Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa.
11 Nyoka akiuma asijatumbuizwa, Basi hakuna faida ya mtumbuizi.
12 Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema; Bali midomo ya mpumbavu itammeza nafsi yake.
13 Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari.
14 Tena, upumbavu huongeza maneno; lakini mwanadamu hajui yatakayokuwako; nayo yatakayokuwa baada yake, ni nani awezaye kumweleza?
15 Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja, Maana hajui hata njia ya kuuendea mji.
16 Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana, Na wakuu wako hula asubuhi!
17 Heri kwako, nchi, mfalme wako akiwa mtoto wa watu, Na wakuu wako hula wakati ufaao, Ili makusudi wapate nguvu, wala si kwa ajili ya ulevi.
18 Kwa sababu ya uvivu paa hunepa; Na kwa utepetevu wa mikono nyumba huvuja.
19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote.
20 Usimlaani mfalme, la, hata katika wazo lako; Wala usiwalaani wakwasi chumbani mwako; Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti, Na mwenye mabawa ataitoa habari.

Mhubiri 11


1 Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi.
2 Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane; Maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
3 Mawingu yakiwa yamejaa mvua, Yataimimina juu ya nchi; Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.
4 Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5 Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.
6 Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa,kama ni hii au hii,au kama zote zitafaa sawasawa.
7 Kweli nuru ni tamu, tena ni jambo la kupendeza macho kutazama jua.
8 Naam, mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie yote; lakini na azikumbuke siku zijazo za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Mambo yote yajayo ni ubatili.
9 Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.
10 Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.

Mhubiri 12


1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.
2 Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
3 Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
4 Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa;
5 Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani.
6 Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani;
7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.
8 Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
9 Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.
10 Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.
11 Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.
12 Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.
13 Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.