Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12
1 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru.
2 Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake.
3 Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;
4 vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.
5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.
7 Mkuu wa matowashi akawapa majina; alimwita Danielii, Belteshaza; na Hanania akamwita Shadraka; na Mishaeli akamwita Meshaki; na Azaria akamwita Abednego.
8 Lakini Danielii aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.
9 Basi Mungu alimjalia Danielii kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.
10 Mkuu wa matowashi akamwambia Danielii, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa changu mbele ya mfalme.
11 Ndipo Danielii akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria,
12 Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe.
13 Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona.
14 Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.
15 Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme.
16 Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
17 Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto.
18 Hata mwisho wa siku zile alizoziagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza.
19 Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.
20 Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.
21 Tena, Danielii huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi.
1 Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha.
2 Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme.
3 Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake.
4 Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonyesha tafsiri yake.
5 Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa.
6 Bali kama mkinionyesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionyesheni ile ndoto na tafsiri yake.
7 Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonyesha tafsiri yake.
8 Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka.
9 Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionyesha tafsiri yake.
10 Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo.
11 Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili.
12 Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli.
13 Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danielii na wenzake ili wauawe.
14 Ndipo Danielii kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli;
15 alijibu, akamwambia Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danielii habari ile.
16 Basi Danielii akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile.
17 Ndipo Danielii akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake;
18 ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danielii na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.
19 Ndipo Danielii alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danielii akamhimidi Mungu wa mbinguni.
20 Danielii akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake.
21 Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa;
22 yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake.
23 Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme.
24 Basi Danielii akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonyesha mfalme ile tafsiri.
25 Ndipo Arioko akamwingiza Danielii mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri.
26 Mfalme akajibu, akamwambia Danielii, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake.
27 Danielii akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;
28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;
29 Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.
30 Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.
31 Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.
32 Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba;
33 miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo.
34 Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.
35 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.
36 Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.
37 Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu;
38 na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.
39 Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.
40 Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.
41 Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope.
42 Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.
43 Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.
44 Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.
45 Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.
46 Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danielii, akatoa amri wamtolee Danielii sadaka na uvumba.
47 Mfalme akajibu, akamwambia Danielii, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii.
48 Basi mfalme akamtukuza Danielii, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.
49 Tena, Danielii akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya uliwali wa Babeli; lakini huyo Danielii alikuwa akiketi katika lango la mfalme.
1 Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli.
2 Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha.
3 Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
4 Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi,
5 wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
6 Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.
7 Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
8 Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.
9 Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele.
10 Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu;
11 na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao.
12 Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
13 Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme.
14 Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
15 Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?
16 Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.
17 Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
18 Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
19 Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto.
20 Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
21 Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
22 Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego.
23 Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto.
24 Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.
25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.
26 Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.
27 Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo.
28 Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.
29 Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.
30 Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.
1 Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu.
2 Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu, aliyonitendea Mungu aliye juu.
3 Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.
4 Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi.
5 Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha.
6 Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile.
7 Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake.
8 Bali hatimaye Danielii akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto, nikisema,
9 Ee Belteshaza, mkuu wa waganga, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie njozi za ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake.
10 Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana.
11 Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia.
12 Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.
13 Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni.
14 Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake.
15 Walakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi;
16 moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake.
17 Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge.
18 Mimi, Nebukadreza, nimeiona ndoto hii; na wewe, Ee Belteshaza, eleza tafsiri yake, kwa maana wenye hekima wote wa ufalme wangu hawawezi kunijulisha tafsiri yake; bali wewe waweza, maana roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako.
19 Ndipo Danielii, aliyeitwa jina lake Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akajibu akasema, Ee Belteshaza, ndoto ile isikufadhaishe wala tafsiri yake. Belteshaza akajibu, akasema, Bwana wangu, ndoto hii iwapate wao wakuchukiao, na tafsiri yake iwapate adui zako.
20 Ule mti uliouona, uliokua, ukawa na nguvu, urefu wake ukafika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka dunia yote;
21 ambao majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha wote; ambao chini yake wanyama wa kondeni walikaa, na ndege wa angani walikuwa na makao yao katika matawi yake;
22 ni wewe, Ee mfalme, uliyekua, na kupata nguvu; maana ukuu wako umekua na kufika mpaka mbinguni, na mamlaka yako yamefika mpaka mwisho wa dunia.
23 Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;
24 tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme;
25 ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng'ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.
26 Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.
27 Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.
28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.
29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.
30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?
31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.
32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.
33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.
34 Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi;
35 na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?
36 Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi.
37 Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.
1 Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao.
2 Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea.
3 Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea.
4 Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.
5 Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.
6 Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.
7 Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
8 Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.
9 Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa.
10 Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike.
11 Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu;
12 kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danielii huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danielii, naye ataionyesha tafsiri.
13 Ndipo Danielii akaletwa mbele ya mfalme. Na Mfalme akanena, akamwambia Danielii, Je! Wewe ndiwe Danielii yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu?
14 Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako.
15 Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.
16 Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
17 Ndipo Danielii akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.
18 Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu;
19 na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha.
20 Lakini moyo wake ulipoinuliwa, na roho yake ilipokuwa ngumu akatenda kwa kiburi, aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi, nao wakamwondolea utukufu wake.
21 Akafukuzwa mbali na wanadamu, moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng'ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote.
22 Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote.
23 Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza.
24 Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa.
25 Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI.
26 Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.
27 TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.
28 PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.
29 Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danielii mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme.
30 Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.
31 Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.
1 Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;
2 na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danielii alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.
3 Basi Danielii huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.
4 Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danielii kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
5 Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danielii huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.
6 Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.
7 Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.
8 Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.
9 Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.
10 Hata Danielii, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.
11 Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danielii akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.
12 Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.
13 Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danielii, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.
14 Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danielii; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.
15 Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.
16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danielii, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danielii, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.
17 Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danielii.
18 Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.
19 Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.
20 Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danielii kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danielii, Ee Danielii, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?
21 Ndipo Danielii akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele.
22 Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.
23 Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danielii katika lile tundu. Ndipo Danielii akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.
24 Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.
25 Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu.
26 Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danielii; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho.
27 Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danielii na nguvu za simba.
28 Basi Danielii huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi.
1 Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danielii aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.
2 Danielii akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa.
3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.
4 Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.
5 Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.
6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.
7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.
8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.
9 Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao.
10 Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa.
11 Nikatazama wakati huo; kwa sababu ya sauti ya yale maneno makubwa iliyoyasema ile pembe; nalitazama hata mnyama yule akauawa, mwili wake ukaharibiwa, akatolewa ateketezwe kwa moto.
12 Na kwa habari za wale wanyama wengine, walinyang'anywa mamlaka yao; walakini maisha yao yalidumishwa kwa wakati na majira.
13 Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.
14 Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.
15 Basi, mimi Danielii, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha.
16 Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo.
17 Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani.
18 Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele.
19 Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake;
20 na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake.
21 Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda;
22 hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme.
23 Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande.
24 Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu.
25 Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.
26 Lakini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuipoteza na kuiangamiza, hata milele.
27 Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.
28 Huu ndio mwisho wa jambo lile. Nami, Danielii, fikira zangu zilinifadhaisha, na uso wangu ulinibadilika; lakini naliliweka jambo hilo moyoni mwangu.
1 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake mfalme Belshaza maono yalinitokea mimi, naam, mimi Danielii, baada ya hayo yaliyonitokea hapo kwanza.
2 Nami naliona katika maono; ilitukia, nilipoona, nalikuwako huko Shushani ngomeni, katika wilaya ya Elamu; nikaona katika maono, nami nalikuwa karibu na mto Ulai.
3 Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo mume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.
4 Nikamwona huyo kondoo mume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama ye yote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama ye yote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake.
5 Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, beberu akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake.
6 Naye akamwendea huyo kondoo mume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake.
7 Nikamwona akimkaribia kondoo mume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo mume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo mume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyaga-kanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo mume katika mkono wake.
8 Na yule beberu akajitukuza sana; na alipokuwa na nguvu, pembe ile kubwa ilivunjika; na badala yake zikazuka pembe nne mashuhuri zilizoelekea pepo nne za mbinguni.
9 Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri.
10 Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga.
11 Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini.
12 Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.
13 Ndipo nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyagisha patakatifu na jeshi?
14 Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.
15 Ikawa mimi, naam, mimi Danielii, nilipoyaona maono hayo, nalitafuta kuyafahamu, na tazama, alisimama mbele yangu mmoja mfano wa mwanadamu.
16 Nikasikia sauti ya mwanadamu katikati ya mto Ulai, iliyoita na kusema, Gabrieli, mfahamishe mtu huyu maono haya.
17 Basi alipakaribia mahali niliposimama; nami naliogopa alipokaribia, nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia, Fahamu, Ee mwanadamu, kwa maana maono haya ni ya wakati wa mwisho.
18 Basi alipokuwa akisema nami, nalishikwa na usingizi mzito na uso wangu uliielekea nchi; lakini alinigusa, akanisimamisha wima.
19 Akaniambia, Tazama, nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa.
20 Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi.
21 Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.
22 Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake.
23 Na wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosao watakapotimia, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama.
24 Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu.
25 Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono.
26 Na maono ya hizo nyakati za jioni na asubuhi yaliyosemwa ni kweli; lakini wewe yafunike maono hayo; maana ni ya wakati ujao baada ya siku nyingi.
27 Na mimi, Danielii, nikazimia, nikaugua siku kadha wa kadha; kisha nikaondoka, nikatenda shughuli za mfalme; nami naliyastajabia yale maono, ila hakuna aliyeyafahamu.
1 Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo;
2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.
3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.
4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;
5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako;
6 wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi.
7 Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa.
8 Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.
9 Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi;
10 wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
11 Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa sababu tumemtenda dhambi.
12 Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya Yerusalemu.
13 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba Bwana, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake.
14 Basi Bwana ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake.
15 Na sasa, Ee Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu.
16 Ee Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka.
17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.
18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.
19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.
20 Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;
21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.
22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.
23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.
24 Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu.
25 Basi ujue na kufahamu, ya kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani zake masihi aliye mkuu; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati za taabu.
26 Na baada ya yale majuma sitini na mawili, masihi atakatiliwa mbali, naye atakuwa hana kitu; na watu wa mkuu atakayekuja watauangamiza mji, na patakatifu; na mwisho wake utakuwa pamoja na gharika, na hata mwisho ule vita vitakuwapo; ukiwa umekwisha kukusudiwa.
27 Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.
1 Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danielii, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo.
2 Katika siku zile mimi, Danielii, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.
4 Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli;
5 naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi;
6 mwili wake pia ulikuwa kama zabarajadi safi, na uso wake mfano wa umeme, na macho yake kama taa za moto, na mikono yake na miguu yake rangi yake kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti ya maneno yake kama sauti ya umati wa watu.
7 Nami, Danielii, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha.
8 Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu.
9 Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi.
10 Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu.
11 Akaniambia, Ee Danielii, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka.
12 Ndipo akaniambia, Usiogope, Danielii; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako.
13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.
14 Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado.
15 Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu.
16 Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikusaziwa nguvu.
17 Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu.
18 Kisha mmoja mfano wa mwanadamu akanigusa tena, akanitia nguvu.
19 Akasema, Ee mtu upendwaye sana, usiogope; amani na iwe kwako, uwe na nguvu, naam, uwe na nguvu. Aliposema nami nikapata nguvu, nikasema, Ee Bwana wangu, na aseme Bwana wangu; kwa maana umenitia nguvu.
20 Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja.
21 Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.
1 Tena mimi, katika mwaka wa kwanza wa Dario, Mmedi, mimi nalisimama nimthibitishe na kumtia nguvu.
2 Nami sasa nitakuonyesha yaliyo kweli. Tazama, watasimama wafalme watatu katika Uajemi; naye mfalme wa nne atakuwa tajiri kuliko hao wote; naye atakapopata nguvu kwa utajiri wake, atawachochea wote juu ya ufalme wa Uyunani.
3 Na mfalme hodari atasimama, atakayetawala kwa mamlaka kubwa, na kutenda apendavyo.
4 Naye atakaposimama, ufalme wake utavunjika, na kugawanyika katika pepo nne za mbinguni; lakini hautakuwa wa uzao wake, wala hautakuwa kama mamlaka yake ambayo alitawala kwayo; kwa maana ufalme wake utang'olewa, hata kwa ajili ya wengine zaidi ya hao.
5 Na mfalme wa kusini atakuwa hodari; na mmoja wa wakuu wake atakuwa hodari kuliko yeye, naye atakuwa na mamlaka; mamlaka yake itakuwa mamlaka kubwa.
6 Na baada ya miaka kadha wa kadha watashirikiana; kwa kuwa binti wa mfalme wa kusini atakuja kwa mfalme wa kaskazini, ili kufanya mapatano naye; lakini hatakuwa na nguvu za mkono wake sikuzote; wala mfalme yule hatasimama, wala mkono wake; lakini yule binti atatolewa, na hao waliomleta, na yeye aliyemzaa, na yeye aliyemtia nguvu, zamani zile.
7 Lakini katika chipukizi la mizizi yake atasimama mmoja mahali pake atakayeliendesha jeshi la askari, naye ataingia katika ngome ya mfalme wa kaskazini, na kuwatenda mambo, na kuwashinda;
8 na miungu yao, pamoja na sanamu zao, na vyombo vyao vizuri vya fedha na dhahabu atavichukua mpaka Misri; kisha atajizuia miaka kadha wa kadha asimwendee mfalme wa kaskazini.
9 Naye huyo ataingia katika ufalme wa mfalme wa kusini, lakini atarudi mpaka nchi yake mwenyewe.
10 Na wanawe watafanya vita, na kukusanya mkutano wa majeshi makuu; watakaokuja na kufurika na kupita katikati; nao watarudi na kufanya vita mpaka penye ngome yake.
11 Na mfalme wa kusini ataingiliwa na ghadhabu, naye atatoka na kupigana naye, yaani, na mfalme wa kaskazini; naye atapanga jeshi kubwa; na jeshi hilo litawekwa mikononi mwake.
12 Atakapokwisha kuchukua lile jeshi, moyo wake utatukuzwa; naye atawaangusha makumi elfu; lakini hataongezewa nguvu.
13 Kwa maana mfalme wa kaskazini atarudi, naye atapanga jeshi kubwa kuliko lile la kwanza; naye hakika atakuja mwisho wa zamani zile, yaani, baada ya miaka kadha wa kadha, pamoja na jeshi kubwa na mali nyingi.
14 Na zamani zile watu wengi watasimama ili kumpinga mfalme wa kusini; pia, wenye jeuri miongoni mwa watu wako watajiinua ili kuyathibitisha maono; lakini wataanguka.
15 Basi mfalme wa kaskazini atakuja, na kufanya kilima, na kuupiga mji wenye maboma; na silaha za kusini hazitaweza kumpinga, wala watu wake wateule, wala hapatakuwa na nguvu za kumpinga.
16 Maana ajaye kupigana naye atatenda kadiri apendavyo, wala hapana mtu atakayesimama mbele yake; naye atasimama katika nchi ya uzuri, na uharibifu utakuwa mkononi mwake.
17 Naye atakaza uso wake ili aje pamoja na nguvu zote za ufalme wake, naye atafanya mapatano naye; naye atatenda kadiri apendavyo; naye atampa binti wa watu ili amharibu; lakini hilo halitasimama wala kumfaa.
18 Baada ya hayo atauelekeza uso wake kwenye visiwa, naye atavipiga visiwa vingi; lakini mkuu mmoja ataikomesha aibu iliyoletwa na yeye; naam, aibu yake hiyo atamrudishia mwenyewe.
19 Ndipo atauelekeza uso wake kwenye ngome za nchi yake mwenyewe; lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
20 Ndipo badala yake atasimama mmoja, atakayepitisha mwenye kutoza ushuru kati ya utukufu wa ufalme wake; lakini katika muda wa siku chache ataangamizwa, si kwa hasira, wala si katika vita.
21 Kisha badala yake atasimama mmoja, mtu astahiliye kudharauliwa, ambaye hawakumpa heshima ya ufalme; naye atakuja wakati wa amani, naye ataupata ufalme kwa kujipendekeza.
22 Na wale wenye silaha mfano wa gharika watagharikishwa mbele yake, na kuvunjika, naam, mkuu wa maagano pia.
23 Na baada ya maagano atatenda kwa hila; maana atapanda, naye atakuwa hodari pamoja na watu wadogo.
24 Wakati wa amani atapaingia mahali palipofanikiwa sana pa wilaya hiyo; naye atatenda mambo ambayo baba zake hawakuyatenda, wala babu zake; atatawanya kati yao mawindo, na mateka, na mali; naam, atatunga hila zake juu ya ngome, hata wakati ulioamriwa.
25 Naye atachochea nguvu zake na ushujaa wake juu ya huyo mfalme wa kusini kwa jeshi kubwa; na mfalme wa kusini atafanya vita kwa jeshi kubwa mno lenye nguvu nyingi; lakini hatasimama; maana watatunga hila juu yake.
26 Naam, walao sehemu ya chakula chake watamwangamiza, na jeshi lake litagharikishwa; na wengi wataanguka wameuawa.
27 Na katika habari za wafalme hao wawili, mioyo yao watanuia kutenda madhara, nao watasema uongo walipo pamoja mezani; lakini hilo halitafanikiwa; maana mwisho utatokea wakati ulioamriwa.
28 Ndipo atakaporudi mpaka nchi yake mwenye utajiri mwingi; na moyo wake utakuwa kinyume cha hilo agano takatifu; naye atafanya kama apendavyo, na kurudi mpaka nchi yake.
29 Kwa wakati ulioamriwa atarudi, na kuingia upande wa kusini; lakini wakati wa mwisho mambo hayatakuwa kama yalivyokuwa wakati wa kwanza.
30 Maana merikebu za Kitimu zitakuja kupigana naye; basi atavunjika moyo, naye atarudi na kulighadhibikia hilo agano takatifu; na kutenda kadiri apendavyo; naam, atarudi, na kuwasikiliza walioacha hilo agano takatifu.
31 Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, nao watalisimamisha chukizo la uharibifu.
32 Na wao wafanyao maovu juu ya hilo agano atawapotosha kwa maneno ya kujipendekeza; lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.
33 Na hao walio wenye hekima katika watu watafundisha wengi; hata hivyo wataanguka kwa upanga, na kwa moto, na kwa kufungwa, na kwa kutekwa nyara, siku nyingi.
34 Basi watakapoanguka, watasaidiwa kwa msaada kidogo; lakini wengi wataambatana nao kwa maneno ya kujipendekeza.
35 Na baadhi yao wenye hekima wataanguka, ili kuwatakasa, na kuwasafisha, na kuwafanya weupe, hata wakati wa mwisho; kwa maana ni kwa wakati ulioamriwa, ambao haujaja.
36 Naye mfalme atafanya kama apendavyo; naye atajitukuza na kujiadhimisha juu ya kila mungu, naye atanena maneno ya ajabu juu ya Mungu wa miungu, naye atafanikiwa mpaka ghadhabu itakapotimia; maana yaliyokusudiwa yatafanyika.
37 Wala hataijali miungu ya baba zake; wala yeye aliyetamaniwa na wanawake; wala hatamjali mungu awaye yote; maana atajitukuza mwenyewe juu ya wote.
38 Lakini katika mahali pake atamheshimu mungu wa ngome; na mungu ambaye baba zake hawakumjua atamheshimu, kwa dhahabu, na fedha, na vito vya thamani, na vitu vipendezavyo.
39 Naye ataziteka nyara ngome zenye nguvu kwa msaada wa mungu mgeni; na yeye atakayemkubali atamwongeza kwa utukufu; naye atawapa kumiliki wengi; naye ataigawa nchi kwa rushwa,
40 na wakati wa mwisho mfalme wa kusini atashindana naye; na mfalme wa kaskazini atamshambulia kama upepo wa kisulisuli, pamoja na magari ya vita, na wapanda farasi, na merikebu nyingi; naye ataingia katika nchi hizo, na kufurika na kupita katikati.
41 Tena ataingia katika hiyo nchi ya uzuri, na nchi nyingi zitapinduliwa; lakini nchi hizi zitaokolewa na mkono wake, Edomu, na Moabu, na wakuu wa watu wa Amoni.
42 Naye ataunyosha mkono wake juu ya nchi hizo, hata na nchi ya Misri haitaokoka.
43 Lakini atakuwa na nguvu juu ya hazina za dhahabu na fedha, na juu ya vitu vyote vya Misri vyenye thamani; na Walibia na Wakushi watafuata nyayo zake.
44 Lakini habari zitokazo mashariki na kaskazini zitamfadhaisha; naye atatoka kwa ghadhabu nyingi, ili kuharibu, na kuwaondolea mbali watu wengi.
45 Naye ataweka hema zake za kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa uzuri; lakini ataifikilia ajali yake, wala hakuna atakayemsaidia.
1 Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.
2 Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.
3 Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.
4 Lakini wewe, Ee Danielii, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.
5 Ndipo mimi, Danielii, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.
6 Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?
7 Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa.
8 Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?
9 Akasema, Enenda zako, Danielii; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.
10 Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.
11 Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.
12 Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.
13 Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.