Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14
1 Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.
2 Hapo kwanza Bwana aliponena kwa kinywa cha Hosea, Bwana alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha Bwana.
3 Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume.
4 Bwana akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli.
5 Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
6 Akachukua mimba tena, akazaa mtoto mwanamke. Bwana akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama kwa maana sitairehemu nyumba ya Israeli tena,nisije nikawasamehe kwa njia yoyote.
7 Lakini nitairehemu nyumba ya Yuda; nitawaokoa kwa Bwana, Mungu wao; wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa silaha, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi.
8 Basi, akiisha kumwachisha Lo-ruhama, akachukua mimba, akazaa mtoto mwanamume.
9 Bwana akasema, Mwite jina lake Lo-ami kwa maana ninyi si watu wangu,wala mimi sitakuwa MUNGU wenu.
10 Tena itakuwa ya kwamba hesabu ya wana wa Israeli itafanana na mchanga wa bahari, usioweza kupimwa wala kuhesabiwa; tena itakuwa, badala ya kuambiwa, Ninyi si watu wangu, wataambiwa, Ninyi ndio wana wa Mungu aliye hai.
11 Na wana wa Yuda na wana wa Israeli watakusanyika pamoja, nao watajiwekea kichwa kimoja, nao watakwea watoke katika nchi hii; kwa maana siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.
1 Waambieni ndugu zenu wanaume, Ami na ndugu zenu wanawake , Ruhama.
2 Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na ayawekee mbali mambo ya uasherati wake yasiwe mbele ya uso wake, na mambo ya uzinzi wake yasiwe kati ya maziwa yake;
3 nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumfisha kwa kiu;
4 naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi.
5 Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu.
6 Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake.
7 Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa.
8 Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali.
9 Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang'anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake.
10 Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu.
11 Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.
12 Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila.
13 Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema Bwana.
14 Kwa hiyo angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo.
15 Nami nitampa mashamba yake ya mizabibu toka huko, na bonde la Akori kuwa mlango wa tumaini; naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.
16 Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita Ishi
17 Kwa maana nitayaondoa majina ya Mabaali kinywani mwake, wala hawatatajwa tena kwa majina yao.
18 Nami siku hiyo nitafanya agano na wanyama wa mashamba kwa ajili yao, tena na ndege wa angani, tena na wadudu wa nchi; nami nitavivunja upinde na upanga na silaha vitoke katika nchi, nami nitawalalisha salama salimini.
19 Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema.
20 Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana.
21 Tena itakuwa siku hiyo, mimi nitaitika, asema Bwana; nitaziitikia mbingu, nazo zitaiitikia nchi;
22 nayo nchi itaiitikia nafaka na divai na mafuta; nayo yataiitikia Yezreeli.
23 Nami nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitamrehemu yeye asiyepewa rehema; nami nitawaambia wale wasiokuwa watu wangu, Ninyi ndinyi watu wangu; nao watasema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
1 Bwana akaniambia, Enenda tena, mpende mwanamke apendwaye na rafiki yake, naye ni mzinzi; kama vile Bwana awapendavyo wana wa Israeli, ingawa wanaigeukia miungu mingine, na kupenda mikate ya zabibu kavu.
2 Basi nikajinunulia mwanamke huyo kwa vipande kumi na vitano vya fedha, na homeri moja ya shayiri, na nusu ya homeri ya shayiri;
3 nami nilimwambia, Utatawa kwa ajili yangu siku nyingi; hutafanya mambo ya ukahaba, wala hutakuwa mke wa mtu awaye yote; nami nitakuwa hali iyo hiyo kwa ajili yako.
4 Kwa maana wana wa Israeli watakaa siku nyingi bila mfalme, wala mtu mkuu, wala sadaka, wala nguzo, wala naivera, wala kinyago;
5 baada ya hayo wana wa Israeli watarejea, na kumtafuta Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao; nao watamwendea Bwana na wema wake kwa kicho siku za mwisho.
1 Lisikieni neno la Bwana, enyi wana wa Israeli; kwa maana Bwana ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi.
2 Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu.
3 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa.
4 Walakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani.
5 Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako.
6 Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.
7 Kadiri walivyozidishwa, kwa kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu.
8 Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao.
9 Hata itakuwa, kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.
10 Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa, lakini hawataongezeka; kwa sababu wameacha kumwangalia Bwana.
11 Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu.
12 Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao.
13 Hutoa dhabihu juu ya vilele vya milima, na kufukiza uvumba juu ya vilima, chini ya mialoni na milibua na miela, kwa kuwa uvuli wake ni mwema; kwa sababu hiyo binti zenu huzini, na bibi arusi zenu hufanya uasherati.
14 Sitawaadhibu binti zenu wazinipo, wala bibi arusi zenu wafanyapo uasherati; maana wao wenyewe huenda kando pamoja na wanawake wazinzi, hutoa dhabihu pamoja na makahaba; na watu hawa wasiofahamu wataangamia.
15 Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo Bwana.
16 Kwa maana Israeli ametenda kwa ukaidi, kama ndama mkaidi; sasa je! Bwana atawalisha kama mwana-kondoo katika mahali penye nafasi!
17 Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache.
18 Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu.
19 Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.
1 Sikieni haya, enyi makuhani, sikilizeni, enyi nyumba ya Israeli, tegeni masikio yenu, enyi wa nyumba ya mfalme, kwa kuwa hukumu hii yawahusu ninyi; maana mmekuwa mtego huko Mizpa, na wavu uliotandwa juu ya Tabori.
2 Nao walioasi wameongeza sana ufisadi wao; lakini mimi ndiye awakaripiaye wote pia.
3 Mimi namjua Efraimu, wala Israeli hakufichwa nisimwone; maana sasa, Ee Efraimu, umefanya uzinzi; Israeli ametiwa unajisi.
4 Matendo yao hayatawaacha kumgeukia Mungu wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui Bwana.
5 Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; kwa sababu hiyo, Israeli na Efraimu watajikwaa katika uovu wao. Yuda naye atajikwaa pamoja nao.
6 Watakwenda na makundi yao ya kondoo na ng'ombe wamtafute Bwana; lakini hawatamwona; amejitenga nao.
7 Wametenda kwa hila juu ya Bwana; maana wamezaa wana wageni; sasa mwezi huu uandamao utawala pamoja na mashamba yao.
8 Pigeni tarumbeta katika Gibea, na baragumu katika Rama; pazeni sauti ya hofu katika Beth-Aveni; nyuma yako, Ee Benyamini!
9 Efraimu atakuwa ukiwa siku ya kukemewa; katika kabila za Israeli nimetangaza habari itakayotokea halafu bila shaka.
10 Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji.
11 Efraimu ameonewa, amesetwa katika hukumu, kwa sababu alikuwa radhi kufuata ubatili.
12 Kwa sababu hiyo mimi nimekuwa kama nondo kwa Efraimu, nimekuwa kama ubovu kwa nyumba ya Yuda.
13 Efraimu alipouona ugonjwa wake, na Yuda jeraha yake, ndipo Efraimu alipokwenda kwa Ashuru, akatuma watu kwa mfalme Yarebu; lakini yeye hawezi kuwapoza, wala hatawaponya jeraha yenu.
14 Maana mimi nitakuwa kama simba kwa Efraimu, na kama mwana-simba kwa nyumba ya Yuda; mimi, naam, mimi nitararua, kisha nitakwenda zangu; nitachukulia mbali, wala hapatakuwa na mtu wa kupokonya.
15 Nitakwenda zangu niparudie mahali pangu, hata watakapoungama makosa yao na kunitafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.
1 Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.
2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.
3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.
4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.
5 Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.
6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.
7 Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.
8 Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu.
9 Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana.
10 Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi.
11 Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.
1 Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang'anyi hushambulia nje.
2 Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.
3 Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.
4 Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu.
5 Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.
6 Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.
7 Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
8 Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.
9 Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari.
10 Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia Bwana, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.
11 Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.
12 Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.
13 Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.
14 Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.
15 Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.
16 Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.
1 Tia baragumu kinywani mwako. Kama tai, anakuja juu ya nyumba ya Bwana; kwa sababu wamelihalifu agano langu, wameiasi sheria yangu.
2 Watanililia, Mungu wangu, sisi Israeli tunakujua.
3 Israeli ameyatupa yaliyo mema; adui watamfuatia.
4 Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali.
5 Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia?
6 Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande.
7 Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza.
8 Israeli amemezwa; sasa wamo miongoni mwa mataifa kama chombo kisichopendeza.
9 Kwa maana wamekwea kwenda Ashuru, mfano wa punda wa mwituni aliye peke yake; Efraimu ameajiri wapenzi.
10 Naam, ijapokuwa waajiri kati ya mataifa, sasa nitawakusanya; nao wanaanza kupunguka kwa sababu ya mzigo wa mfalme wa wakuu.
11 Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake.
12 Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni.
13 Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.
14 Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitapeleka moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.
1 Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka.
2 Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia.
3 Hawatakaa katika nchi ya Bwana; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula kinajisi katika Ashuru.
4 Hawatammiminia Bwana divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya Bwana.
5 Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa idi, na katika siku ya karamu ya Bwana?
6 Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao.
7 Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa.
8 Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwinda ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui.
9 Wamejiharibu mno, kama katika siku za Gibea; ataukumbuka uovu wao, atazilipiza dhambi zao.
10 Mimi nalimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami naliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, wakati wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda.
11 Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba.
12 Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang'anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha.
13 Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake.
14 Wape, Ee Bwana; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu.
15 Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko naliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi.
16 Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana.
17 Mungu wangu atawatupilia mbali, kwa sababu hawakumsikiliza; nao watakuwa watu wa kutanga-tanga kati ya mataifa.
1 Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri.
2 Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao.
3 Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi Bwana; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini?
4 Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.
5 Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-Aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka.
6 Nayo itachukuliwa Ashuru, iwe zawadi kwa mfalme Yarebu; Efraimu atapata aibu, na Israeli atalionea haya shauri lake mwenyewe.
7 Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji.
8 Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni.
9 Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; ili vita vilivyokuwa juu ya wana wa uovu visiwapate katika Gibea.
10 Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili.
11 Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atavunja madongoa yake.
12 Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta Bwana, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.
13 Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako.
14 Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjika-vunjika pamoja na watoto wake.
15 Hivyo ndivyo Betheli atakavyowatenda ninyi, kwa sababu ya ubaya wenu mwingi; wakati wa mapambazuko mfalme wa Israeli atakatiliwa mbali kabisa.
1 Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.
2 Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga.
3 Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya.
4 Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao.
5 Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea.
6 Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe.
7 Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza.
8 Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuponya, Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu ? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja.
9 Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.
10 Watakwenda kumfuata Bwana, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka.
11 Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema Bwana.
12 Efraimu amenizinga kwa maneno ya uongo, na nyumba ya Israeli kwa udanganyifu; na Yuda hata sasa anasita-sita kwa Mungu, na kwake aliye Mtakatifu, naye ni mwaminifu.
1 Efraimu hujilisha upepo, na kuandamana na upepo wa mashariki; haachi kuongeza uongo na uharibifu; nao wafanya agano na Ashuru, na mafuta huchukuliwa kwenda Misri.
2 Bwana naye ana mateto na Yuda, naye atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake; kwa kadiri ya matendo yake atamlipa.
3 Tumboni alimshika ndugu yake kisigino; Na alipokuwa mtu mzima alikuwa na uwezo kwa Mungu;
4 Naam, alikuwa na uwezo juu ya malaika Akashinda; alilia, na kumsihi; Alimwona huko Betheli, naye akasema nasi huko;
5 Naam, Bwana, Mungu wa majeshi; Bwana ndilo kumbukumbu lake.
6 Basi, mrudie Mungu wako; shika fadhili na hukumu; ukamngojee Mungu wako daima.
7 Ni mchuuzi, mizani ya udanganyifu i mkononi mwake; anapenda kudhulumu.
8 Naye Efraimu alisema, Kweli nimekuwa tajiri, nimejipatia mali nyingi; katika kazi zangu zote hawataona kwangu uovu wo wote uliokuwa dhambi.
9 Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za karamu ya idi.
10 Tena nimenena na hao manabii, nami nimeongeza maono, na kwa utumishi wa manabii nimetumia mifano.
11 Je! Gileadi ni uovu? Wamekuwa ubatili tu; huko Gilgali hutoa dhabihu za ng'ombe; naam, madhabahu zao zimekuwa kama chungu katika matuta ya mashamba.
12 Na Yakobo alikimbia mpaka Padan-Aramu, Na Israeli alitumika apate mke; Ili apate mke alichunga kondoo.
13 Na kwa nabii Bwana alimtoa Israeli katika Misri, Na kwa mkono wa nabii alihifadhiwa.
14 Efraimu amenitia hasira kali sana; kwa sababu hiyo damu yake itaachwa juu yake, na Bwana wake atamrudishia lawama yake.
1 Efraimu aliponena, palikuwa na tetemeko; alijitukuza katika Israeli; Lakini alipokosa katika Baali, alikufa.
2 Na sasa wanazidi kufanya dhambi, nao wamejifanyizia sanamu kwa fedha yao, naam, sanamu kwa kadiri ya akili zao; zote pia ni kazi ya mafundi; nao huzitaja hivi, Wanaume watoao dhabihu na wazibusu ndama.
3 Kwa sababu hiyo watakuwa kama wingu la asubuhi, na kama umande utowekao upesi, kama makapi yaliyopeperushwa na tufani sakafuni, na kama moshi utokao katika bomba.
4 Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu nchi ya Misri; wala hutamjua mungu mwingine ila mimi; wala zaidi ya mimi hakuna Mwokozi.
5 Mimi nalikujua katika jangwa, katika nchi yenye kiu nyingi.
6 Kwa kadiri ya malisho yao, kwa kadiri iyo hiyo walishiba; walishiba na moyo wao ukatukuka; ndiyo sababu wamenisahau mimi.
7 Basi nimekuwa kama simba kwao; kama chui nitavizia njiani;
8 nitakutana nao kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake; nami nitararua nyama ya mioyo yao; na huko nitawala kama simba; huyo mnyama mkali atawararua.
9 Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli, ya kuwa wewe u kinyume changu mimi, kinyume cha msaada wako.
10 Yuko wapi sasa mfalme wako, apate kukuokoa katika miji yako yote? Na hao waamuzi wako, uliowanena hivi, Nipe mfalme na wakuu?
11 Nimekupa mfalme katika hasira yangu, nikamwondoa katika ghadhabu yangu.
12 Uovu wa Efraimu umefungwa kwa kukazwa; dhambi yake imewekwa akiba.
13 Utungu wa mwanamke mwenye mimba utampata; yeye ni mwana asiye na akili; maana wakati umewadia, ambao haimpasi kukawia mahali wapenyapo watoto.
14 Nitawakomboa na nguvu za kaburi; nitawaokoa na mauti; ewe mauti, ya wapi mapigo yako? Ewe kaburi, ku wapi kuharibu kwako? Kujuta kutafichwa na macho yangu.
15 Ajapokuwa yeye ni mwenye kuzaa sana kati ya ndugu zake, upepo wa mashariki utakuja, hiyo pumzi ya Bwana itokayo upande wa nyikani, na kijito chake cha maji kitakauka, na chemchemi yake itakaushwa; yeye atateka nyara hazina ya vyombo vyote vipendezavyo.
16 Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatambuliwa.
1 Ee Israeli, mrudie Bwana, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako.
2 Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng'ombe.
3 Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema.
4 Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha.
5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni.
6 Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni.
7 Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.
8 Efraimu atasema, Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako.
9 Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.