Obadia

Sura: 1

Obadia 1


1 Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema,Haya,inukeni ninyi;Na tuinuke tupigane naye.
2 Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana.
3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi?
4 Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana.
5 Kama wevi wangekujilia, kama wanyang'anyi wangekujilia usiku, (jinsi ulivyokatiliwa mbali!) Je! Wasingeiba kiasi cha kuwatosha? Kama wachumao zabibu wangekujilia, je! Wasingeacha baadhi ya zabibu, ziokotwe?
6 Jinsi watu wa Esau wanavyotafutwa-tafutwa! Jinsi hazina zake zilizofichwa zinavyoulizwa-ulizwa!
7 Watu wote wa mapatano yako Wamekufukuza, hata mipakani; Wale waliofanya amani nawe Wamekudanganya, na kukushinda; Walao mkate wako wameweka mtego chini yako; Wala hana ufahamu wa hayo ndani yake.
8 Siku hiyo, je! Sitawaangamiza watu wenye akili katika Edomu, na wenye ufahamu katika kilima cha Esau? Asema Bwana.
9 Na mashujaa wako, Ee Temani, watafadhaika, hata iwe kila mtu akatiliwe mbali kwa kuuawa katika kilima cha Esau.
10 Kwa sababu ya udhalimu aliotendwa ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika, nawe utakatiliwa mbali hata milele.
11 Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao.
12 Lakini usiitazame siku ya ndugu yako, siku ya mashaka yake, wala usisimange juu ya wana wa Yuda siku ya kuangamizwa kwao; wala usinene maneno ya kiburi katika siku ya shida yao.
13 Usiingie katika lango la watu wangu, siku ya msiba wao; naam, usiyatazame mateso yao, siku ya msiba wao; wala usitie mikono yako juu ya mali zao, siku ya msiba wao.
14 Wala usisimame penye njia panda, ili kuwakatilia mbali watu wake wakimbiao; wala usiwatoe watu wake waliosalia, katika siku ya dhiki.
15 Kwa maana hiyo siku ya Bwana i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.
16 Kwa maana kama vile mlivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, ndivyo mataifa yote watakavyokunywa daima; naam, watakunywa na kubabaika, nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe.
17 Bali katika mlima Sayuni watakuwako wenye kuokoka, nao utakuwa mtakatifu; na nyumba ya Yakobo watamiliki milki zao.
18 Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa Bwana amesema hayo.
19 Na watu wa Negebu wataumiliki mlima wa Esau; na watu wa Shefela watawamiliki Wafilisti; nao watalimiliki konde la Efraimu, na konde la Samaria, na Benyamini atamiliki Gileadi.
20 Na watu wa jeshi hili la wana wa Israeli waliotekwa, walio kati ya Wakanaani, watamiliki mpaka Sarepta; na hao watu wa Yerusalemu waliotekwa, waliomo Sefaradi, wataimiliki miji ya Negebu.
21 Tena waokozi watakwea juu ya mlima Sayuni ili kuuhukumu mlima wa Esau; na huo ufalme utakuwa ni mali ya Bwana.