Malaki

Sura: 1, 2, 3, 4

Malaki 1


1 Ufunuo wa neno la Bwana kwa Israeli kwa mkono wa Malaki
2 Nimewapenda ninyi, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema Bwana; ila nimempenda Yakobo;
3 bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani.
4 Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwa-pondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; Bwana wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha; na watu watawaita, Mpaka wa uovu, na, Watu ambao Bwana anawaghadhabikia milele.
5 Na macho yenu ninyi yataona, nanyi mtasema, Bwana ndiye mkuu kupita mpaka wa Israeli.
6 Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani?
7 Mnatoa chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu Nanyi mwasema, Sisi tumekutia unajisi kwa jinsi gani? Kwa sababu mwasema, Meza ya Bwana ni kitu cha kudharauliwa.
8 Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi.
9 Na sasa, nawasihi, ombeni fadhili za Mungu, ili atupe neema; ikiwa jambo hili limetoka katika mikono yenu; je! Atawakubali nafsi zenu? Asema Bwana wa majeshi.
10 Laiti angekuwapo kwenu mtu mmoja wa kuifunga milango; msije mkawasha moto bure madhabahuni pangu! Sina furaha kwenu, asema Bwana wa majeshi, wala sitakubali dhabihu yo yote mikononi mwenu.
11 Kwa maana tokea maawio ya jua hata machweo yake jina langu ni kuu katika Mataifa; na katika kila mahali unatolewa uvumba na dhabihu safi kwa jina langu; maana jina langu ni kuu katika Mataifa, asema Bwana wa majeshi.
12 Lakini ninyi mnalitia unajisi, kwa kuwa mwasema, Meza ya Bwana imetiwa unajisi; na matunda yake, yaani, nyama yake, hudharauliwa.
13 Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.
14 Lakini na alaaniwe mtu mwenye kudanganya, ambaye katika kundi lake ana mume, akaweka nadhiri, ila amtolea Bwana kitu kilicho na kilema; kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa.

Malaki 2


1 Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi.
2 Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni.
3 Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo
4 Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema Bwana wa majeshi.
5 Agano langu naye lilikuwa agano la uhai na amani; nami nikampa ili aogope, naye akaniogopa, akalicha jina langu.
6 Sheria ya kweli ilikuwa kinywani mwake, wala udhalimu haukuonekana midomoni mwake; alikwenda pamoja nami katika amani na unyofu, na kuwageuza wengi hata wakaacha uovu.
7 Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi.
8 Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema Bwana wa majeshi.
9 Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria.
10 Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?
11 Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa Bwana aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni.
12 Bwana atamtenga mtu atendaye hayo, yeye aliye macho, na yeye ajibuye, atamtenga na hema za Yakobo, pia atamtenga yeye amtoleaye Bwana wa majeshi dhabihu.
13 Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya Bwana kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia.
14 Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako.
15 Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana.
16 Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.
17 Mmemchokesha Bwana kwa maneno yenu. Lakini ninyi mwasema, Tumemchokesha kwa maneno gani? Kwa kuwa mwasema, Kila atendaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, naye huwafurahia watu hao, au, Mungu mwenye kuhukumu yuko wapi?

Malaki 3


1 Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.
2 Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo;
3 naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki.
4 Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
5 Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi.
6 Kwa kuwa mimi, Bwana, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.
7 Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?
8 Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.
9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.
10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.
12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.
13 Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?
15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.
17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.
18 Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia.

Malaki 4


1 Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi.
2 Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini.
3 Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu; katika siku ile niifanyayo, asema Bwana wa majeshi.
4 Ikumbukeni torati ya Musa, mtumishi wangu, niliyomwamuru huko Horebu kwa ajili ya Israeli wote, naam, amri na hukumu.
5 Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya.
6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.