WARUMI

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16

WARUMI 1


1 Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu;
2 ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu;
3 yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili,
4 na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu;
5 ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake;
6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo;
7 kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
8 Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima.
9 Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma,
10 siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu.
11 Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara;
12 yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu.
13 Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine.
14 Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima.
15 Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi.
16 Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.
17 Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
18 Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
19 Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia.
20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru;
21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.
22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;
23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.
24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,
30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,
31 wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.

WARUMI 2


1 Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale.
2 Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo.
3 Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu?
4 Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?
5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,
6 atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;
7 wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele;
8 na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;
9 dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia;
10 bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia;
11 kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.
12 Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria.
13 Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.
14 Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe.
15 Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea;
16 katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.
17 Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu,
18 na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati,
19 na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani,
20 mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati;
21 basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?
22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?
23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?
24 Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa.
25 Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.
26 Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?
27 Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaihalifu torati?
28 Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;
29 bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.

WARUMI 3


1 Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini?
2 Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.
3 Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu?
4 Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu.
5 Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.)
6 Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu?
7 Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi?
8 Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki.
9 Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;
10 kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja.
11 Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu.
12 Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.
13 Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.
14 Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.
15 Miguu yao ina mbio kumwaga damu.
16 Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao.
17 Wala njia ya amani hawakuijua.
18 Kumcha Mungu hakupo machoni pao.
19 Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu;
20 kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.
21 Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;
22 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;
23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;
25 ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.
26 apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.
27 Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.
28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
29 Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia;
30 kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo.
31 Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.

WARUMI 4


1 Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili?
2 Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu.
3 Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.
4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6 Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
7 Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.
9 Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.
10 Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa.
11 Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki;
12 tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.
13 Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.
14 Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
15 Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.
16 Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote;
17 (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.
18 Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.
19 Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara.
20 Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;
21 huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.
22 Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
23 Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake;
24 bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu;
25 ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

WARUMI 5


1 Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
2 ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.
3 Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;
5 na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
6 Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu.
7 Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema.
8 Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.
9 Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.
10 Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.
11 Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.
12 Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;
13 maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria;
14 walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja.
15 Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
16 Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki.
17 Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.
18 Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima.
19 Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.
20 Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi;
21 ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.

WARUMI 6


1 Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?
2 Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?
3 Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.
5 Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;
6 mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;
7 kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.
8 Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye;
9 tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.
10 Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu.
11 Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
12 Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;
13 wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki.
14 Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.
15 Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha!
16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.
17 Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake;
18 na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki.
19 Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa.
20 Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki.
21 Ni faida gani basi mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti.
22 Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.
23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

WARUMI 7


1 Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai?
2 Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume.
3 Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.
4 Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.
5 Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.
6 Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
7 Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.
8 Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa.
9 Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa.
10 Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti.
11 Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua.
12 Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.
13 Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno.
14 Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.
15 Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda.
16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.
17 Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu
18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.
19 Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.
20 Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
21 Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya.
22 Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani,
23 lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.
24 Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25 Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.

WARUMI 8


1 Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.
2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.
3 Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;
4 ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.
5 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.
6 Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.
7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
8 Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.
10 Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.
11 Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.
12 Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili,
13 kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.
14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.
15 Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.
16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;
17 na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.
19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;
21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.
23 Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu.
24 Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho?
25 Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.
26 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
27 Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.
28 Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
29 Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.
30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.
31 Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?
32 Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
33 Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
36 Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.
37 Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

WARUMI 9


1 Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu,
2 ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.
3 Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili;
4 ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake;
5 ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.
6 Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli.
7 Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa;
8 yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao.
9 Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana.
10 Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu,
11 (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye),
12 aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo.
13 Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
14 Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!
15 Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye.
16 Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.
17 Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.
18 Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.
19 Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?
20 La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?
22 Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;
23 tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;
24 ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia?
25 Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu.
26 Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai.
27 Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema, Hesabu ya wana wa Israeli,ijapokuwa ni kama mchanga wa bahari,ni mabaki yao tu watakaookolewa.
28 Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata.
29 Tena kama Isaya alivyotangulia kunena, Kama Bwana wa majeshi asingalituachia uzao, Tungalikuwa kama Sodoma, tungalifananishwa na Gomora.
30 Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki; lakini ni ile haki iliyo ya imani;
31 bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikilia ile sheria.
32 Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo,
33 kama ilivyoandikwa, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye hatatahayarika.

WARUMI 10


1 Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.
2 Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.
3 Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.
4 Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.
5 Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo.
6 Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini),
7 au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)
8 Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.
9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.
11 Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.
12 Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;
13 kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!
16 Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?
17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
18 Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
19 Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha.
20 Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia.
21 Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.

WARUMI 11


1 Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini.
2 Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,
3 Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.
4 Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.
5 Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema.
6 Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema.
7 Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito.
8 Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo.
9 Na Daudi asema, Meza yao na iwe tanzi na mtego, Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao;
10 Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote.
11 Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.
12 Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao?
13 Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu,
14 nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao.
15 Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?
16 Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.
17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,
18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.
19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.
20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.
21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe.
22 Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.
23 Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.
24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?
25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.
28 Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu.
29 Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.
30 Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao;
31 kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema.
32 Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.
33 Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!
34 Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake?
35 Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena?
36 Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.

WARUMI 12


1 Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.
2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
3 Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.
4 Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;
5 Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.
6 Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;
7 ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;
8 mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.
9 Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.
10 Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;
11 kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;
12 kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;
13 kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.
14 Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.
15 Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.
16 Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.
17 Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.
18 Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.
19 Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
20 Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.
21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

WARUMI 13


1 Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.
3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo.
7 Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima.
8 Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.
9 Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
10 Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.
11 Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini
12 Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.
13 Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.
14 Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.

WARUMI 14


1 Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.
2 Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga.
3 Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali.
4 Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
6 Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu.
7 Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake.
8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.
9 Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.
10 Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
11 Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu.
12 Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.
13 Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha.
14 Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.
15 Na ndugu yako akiingia huzuni kwa sababu ya chakula, umeacha kwenda katika upendo. Kwa chakula chako usimharibu mtu yule ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.
16 Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya.
17 Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.
18 Kwa kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena hukubaliwa na wanadamu.
19 Basi kama ni hivyo, na mfuate mambo ya amani na mambo yafaayo kwa kujengana.
20 Kwa ajili ya chakula usiiharibu kazi ya Mungu. Kweli, vyote ni safi; bali ni vibaya kwa mtu alaye na kujikwaza.
21 Ni vyema kutokula nyama wala kunywa divai wala kutenda neno lo lote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa.
22 Ile imani uliyo nayo uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiyejihukumu nafsi yake katika neno lile analolikubali.
23 Lakini aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia, kwa maana hakula kwa imani. Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.

WARUMI 15


1 Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe.
2 Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe.
3 Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi.
4 Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini.
5 Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu;
6 ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7 Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.
8 Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu;
9 tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako.
10 Na tena anena, Furahini,Mataifa,pamoja na watu wake.
11 Na tena, Enyi Mataifa yote,msifuni Bwana; Enyi watu wote,mhimidini.
12 Na tena Isaya anena, Litakuwako shina la Yese, Naye aondokeaye kuwatawala Mataifa; Ndiye Mataifa watakayemtumaini.
13 Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.
14 Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana.
15 Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu,
16 ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu.
18 Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo,
19 kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu;
20 kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine;
21 bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.
22 Ndiyo sababu nalizuiwa mara nyingi nisije kwenu.
23 Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu;
24 wakati wo wote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo.
25 Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu;
26 maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini.
27 Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili.
28 Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania.
29 Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo.
30 Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu;
31 kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;
32 nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.
33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.

WARUMI 16


1 Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea;
2 kwamba mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu; mkamsaidie katika neno lo lote atakalohitaji kwenu; kwa sababu yeye naye amekuwa msaidizi wa watu wengi, akanisaidia mimi pia.
3 Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu;
4 waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.
5 Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo.
6 Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu.
7 Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.
8 Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana.
9 Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu.
10 Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika Kristo. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo.
11 Nisalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana.
12 Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana.
13 Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na mamaye, aliye mama yangu pia.
14 Nisalimieni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma, na ndugu walio pamoja nao.
15 Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote walio pamoja nao.
16 Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yawasalimu.
17 Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.
18 Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.
19 Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.
20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]
21 Timotheo, mtenda kazi pamoja nami, awasalimu, na Lukio, na Yasoni, na Sosipatro, jamaa zangu.
22 Mimi Tertio, niliyeandika waraka huu, nawasalimu katika Bwana.
23 Gayo, mwenyeji wangu na wa Kanisa lote pia awasalimu. Erasto, wakili wa mji, awasalimu, na Kwarto, ndugu yetu.
24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.]
25 Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele,
26 ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii, ikajulikana na mataifa yote kama alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani.
27 Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina.