TITO

Sura: 1, 2, 3

TITO 1


1 Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa;
2 katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;
3 akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu;
4 kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.
5 Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;
6 ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii.
7 Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU;asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu.
8 bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake;
9 akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.
10 Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao.
11 Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.
12 Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu.
13 Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani;
14 wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli.
15 Vitu vyote ni safi kwa hao walio safi; lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia.
16 Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.

TITO 2


1 Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima;
2 ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi.
3 Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;
4 ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;
5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.
6 Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi;
7 katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu,
8 na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.
9 Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu,
10 wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.
11 Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
12 nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;
13 tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
14 ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.
15 Nena maneno hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.

TITO 3


1 Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema;
2 wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.
3 Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.
4 Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;
5 si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;
6 ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;
7 ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.
8 Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu.
9 Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.
10 Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae;
11 ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.
12 Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi kuja kwangu huku Nikopoli; kwa maana huku nimekusudia kukaa wakati wa baridi.
13 Zena, yule mwana-sheria, na Apolo, uwasafirishe kwa bidii, wasipungukiwe na cho chote.
14 Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.
15 Watu wote walio pamoja nami wakusalimu. Tusalimie wale watupendao katika imani. Neema na iwe pamoja nanyi nyote.