1 Yakobo, mtumwa wa Mungu, na wa Bwana Yesu Kristo, kwa kabila kumi na mbili waliotawanyika; salamu.
2 Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
3 mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
4 Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.
5 Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.
6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.
9 Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa;
10 bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka.
11 Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.
12 Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.
13 Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.
14 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
15 Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
16 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.
17 Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.
18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
19 Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;
20 kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.
21 Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
22 Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.
24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.
26 Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.
27 Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.
1 Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.
2 Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;
3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,
4 je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?
5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?
6 Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?
7 Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa?
8 Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema.
9 Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.
10 Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.
11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.
12 Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru.
13 Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.
14 Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa?
15 Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki,
16 na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?
17 Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.
18 Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
19 Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.
20 Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?
21 Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu?
22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.
23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.
24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.
25 Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?
26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.
1 Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.
2 Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.
3 Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote.
4 Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha.
5 Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.
6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.
7 Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.
8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.
10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.
11 Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?
12 Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu.
13 N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima.
14 Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli.
15 Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.
16 Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.
17 Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.
18 Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.
1 Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?
2 Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!
3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.
4 Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.
5 Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?
6 Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.
7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.
8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.
9 Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu.
10 Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.
11 Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu.
12 Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?
13 Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida;
14 walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.
15 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.
16 Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya.
17 Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.
1 Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia.
2 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo.
3 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho.
4 Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi.
5 Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo.
6 Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.
7 Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.
8 Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.
9 Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.
10 Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.
11 Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.
12 Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.
13 Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi.
14 Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.
15 Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.
16 Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.
17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.
18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.
19 Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza;
20 jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.